January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UVIKO-19 siyo kikwazo cha kushiriki Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Imeelezwa kuwa UVIKO-19 siyo kikwazo kwa yoyote kushiriki kwa nafasi yake katika sensa ya mwaka 2022 kwani kulingana na maendeleo ya ugonjwa huo Makarani na Watendaji wote katika sensa hii watazingatia tahadhari zote zinazoelekezwa na wataalamu wa Afya ili kutowaambukiza wananchi au kuambukizwa na wananchi wakati wa zoezi la sensa.

Hayo yameelezwa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kupitia kipeperushi chao elekezi kuhusu maswali ambayo huulizwa mara kwa mara wakati wa sensa

Aidha NBS imewataka watu wote kutoa ushirikiano wa kutosha kwa karani wa sensa pale atakapotembelea katika kaya kwa kujibu maswali yote atakayouliza kwa usahihi;

“Ukiulizwa swali na hujalielewa au hujasikia vizuri, unayo haki ya kumuomba karani arudie kuuliza au kutoa ufafanuzi ili uweze kutoa jibu sahihi kulingana na swali lililoulizwa”

Pia Ofisi ya Taifa ya Takwimu imesema ni muhimu kwa mkuu wa kaya kuhakikisha anachukua taarifa zote muhimu kwa mkuu Kama umri, elimu, jinsia, hali ya ndoa, umiliki wa vitambulisho vya Taifa, shughuli za kiuchumi za watu wote waliolala katika Kaya yake usiku wa kuamkia siku ya sensa ili aweze kukumbuka wakati karani atakalotembelea katika kaya.

Mbali na hayo, NBS imefafanua jinsi sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 itakavyofanyika;

“Siku ya sensa karani wa sensa akiongozana na Mwenyekiti au kiongozi wa serikali ya Mtaa au kitongoji/Shehia atafika katika Kaya akiwa na kitambulisho cha Karani wa Sensa na Dodoso la Sensa lililowekwa katika kifaa cha kielektroniki kiitwacho kishikwambi (Tablet) na kuuliza maswali ambayo yatajibiwa na mkuu wa Wilaya”

Ofisi ya Taifa ya Takwimu imesema, Ikiwa Mkuu wa Kaya ambaye ana taarifa za kutosha kuhusiana na Kaya na watu wote waliolala ndani ya Kaya husika usiku wa kuamkia siku ya sensa anaweza kujibu maswali ya sensa kwa niaba yake.

Sensa ya mwaka 2022 Kama zilivyo sensa zilizopita itafanyika nchi nzima na itahusisha watu wote watakaolala ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.