December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UVCCM Tanga wapata viongozi wapya

Na Yusuph Mussa, Korogwe

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Tanga umepata viongozi wapya baada ya Ramadhan Omar kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti, huku Bi-Umra Sekiboko akichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa.

Ni kwenye uchaguzi uliofanyika Novemba 16, 2022 wilayani Korogwe, huku Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi akiwa ni Edward Mpogolo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Akitangaza matokeo hayo, Mpogolo alisema Omar alipata kura 472, huku Faraha Mvumo akishika nafasi ya pili kwa kupata kura 214, na Said Hassan akiambulia 46.

Kwenye nafasi ya Ujumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa, Sekiboko alipata kura 340, huku mshindani wake baada ya kura kurudiwa, Ismail Saleh akipata kura 317.

Bi-Umrah Sekiboko, anafuata nyayo za dada yake ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga, Husna Sekiboko ambaye aliwahi kushika nafasi hiyo ya Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa kutoka Mkoa wa Tanga.

Kwenye nafasi ya kutafuta Mjumbe wa Mkutano Mkuu Vijana Taifa, Ibrahim Shehiza alipata ushindi kwa kura 317, na kuwabwaga Hija Mpole aliyepata kura 239, na Martin Nkupe kura 80.

Katika kutafuta Mwakilishi wa Vijana kwenda Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Tanga, Sekiboko aling’ara tena baada ya kuchaguliwa kwa kura 310, na kumshinda Hafsati Seng’ung’una aliyepata kura 174.

Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa UVCCM Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro Edward Mpogolo akizungumza na Wajumbe kabla ya kuanza shughuli za uchaguzi, uliofanyika Novemba 16, 2022 kwenye Wilaya ya Korogwe. (Picha na Yusuph Mussa).
Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa UVCCM Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro Edward Mpogolo (kulia) akizungumza na Wajumbe (hawapo pichani) kabla ya Wajumbe wa Wilaya ya Lushoto hawajaanza kupiga kura. Wilaya ya Lushoto inafahamika kama Jimbo la Florida nchini Marekani, kwani kura zake za wajumbe ambao wapo 163, ndiyo wengi kwa Mkoa wa Tanga. Lakini waliofika kwenye uchaguzi huo Novemba 16, 2022 ni 153. Uchaguzi huo umefanyika Wilaya ya Korogwe. Wengine kwenye picha ni wagombea wa nafasi ya Ujumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa akiwemo Bi-umrah Juma Sekiboko (wa pili kulia) akiwa na wenzake watatu. (Picha na Yusuph Mussa).
Wajumbe wa UVCCM Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wakiwa kwenye mstari wa kupiga kura. Wilaya ya Lushoto inafahamika kama Jimbo la Florida nchini Marekani, kwani kura zake za wajumbe ambao wapo 163, ndiyo wengi kwa Mkoa wa Tanga, na ndiyo wanaoamua matokeo kwa kiasi kikubwa. Lakini waliofika kwenye uchaguzi wa Novemba 16, 2022 ni 153. Uchaguzi huo unafanyika Wilaya ya Korogwe. (Picha na Yusuph Mussa).
Mgombea ujumbe wa wa Baraza Kuu UVCCM Taifa kutoka Mkoa wa Tanga Bi-Umrah Sekiboko akijinadi mbele ya Wajumbe kwenye Uchaguzi wa UVCCM Mkoa wa Tanga uliofanyika Wilaya ya Korogwe Novemba 16, 2022. Bi.Umrah ni mwenyeji wa Wilaya ya Lushoto, na alishinda nafasi hiyo. (Picha na Yusuph Mussa).
Mwenyekiti mpya wa UVCCM Mkoa wa Tanga Ramadhan Omar. (Picha na Yusuph Mussa).