Na George Mwigulu,Timesmajiraonline,Katavi.
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi UVCCM Mkoa wa Katavi umeanza kukusanya ushahidi utakao wezesha kuwashughulikia walioanza kampeni.
Ambapo CCM imewataka vijana wa chama hicho kuwashughulikia wale wote walioanza kampeni mapema kwani kufanya hivyo ni kinyume na utaratibu.
Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Hemed Suleiman Abdulla amenukuliwa Agosti 4, 2024 Mkoani Pemba akionya baadhi ya makada wanaotangaza kugombea nafasi kabla ya muda.
Akiwa kwenye kongamano la vijana la kuonesha mafanikio, fursa na maendeleo ya serikali ya Tanzania Bara na Visiwani alimwagiza Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohammed Ali Kawaida kuchukua hatua za kimaadili dhidi ya wanaokwenda kinyume na chama hicho.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Katavi, Amir Katalambula Said akizungunza Jumatatu Julai 5, 2024 amesema, Kuwa na nia moyoni ya kugombea sio kosa bali kinachokatazwa ni kuanza kampeni mapema kinyume na utaratibu.
Said amesema UVCCM imepokea maelekezo na wakiwa vijana wanajukumu la kukilinda chama kwa maadui wa ndani na nje ya chama hicho.
Maadui wa ndani ameeleza ni watu wanaoweza kuzua taharuki mbalimbali zitakazo dhorotesha umoja na mshikamano wa CCM ambapo jukumu lao ni kuhakikisha kanuni, taratibu na misingi ya katiba inaendelea kuheshimika na kufuatwa.
“Huo ni wajibu wetu kikatiba na niwajibu wetu kikanuni za Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi kinatutaka sisi kuwa walizi wa chama chetu kwahiyo maelekezo ni sehemu ya kukubushwa wajibu wetu” Amesisitiza Said.
Mwenyekiti huyo wa UVCCM Mkoa wa Katavi ameweka wazi kuwa wameongeza mfumo wa kiuchunguzi kwa ajili ya kubaini wote ambao wanafanya kampeni kabla ya muda.
Mfumo ambao utawasaidia pia kukusanya ushahidi wa kutosha ambao utatumika kuwawajibisha wakiukaji wa maadili “Hatuwezi kufanyia kazi maneno ya kusikia huko nje…kama hakuna ushahidi je tutadhibitishaje?” Ameuliza Said.
Amesema baada ya kuwabaini watapeleka taarifa kwenye vikao halali vya chama ili hatua sitahiki ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
“Tunafahamu tunazo kamati za udhibiti za ngazi mbalimbali kwenye maeneo yetu, tunazo kamati za maadili ambazo zinatokana na kamati za siasa za ngazi mbalimbali za uongozi zinauwezo wa kuonya au adhabu” Amesema Mwenyekiti huyo wa UVCCM.
Ametoa wito kwa watu wenye nia ya kugombea uongozi kwa sasa kuheshimu miongozo mbalimbali ya CCM ya kanuni,taratibu na Katiba kwa kutoa ushirikiano kwa viongozi ambao kwa sasa wanadhamana ya kutekeleza ilani ya chama hicho ya uchaguzi wa mwaka 2020.
Said ameeleza Madhara ya kujitangaza kugombea mapema kuwa ni kujitengenezea makundi mapema, na kwa yule ambaye bado yupo ndani ya uongozi ataacha kufanya wajibu wake wa msingi wa kuhakikisha katika kipindi kilichobaki ilani inatekelezwa naye ataanza kutizama nafasi yake na kuanza kufanya kampeni mapema kinyume na utaratibu.
Katika hatua nyingine amewaondoa shaka vijana wenye nia ya kugombea kuondoa hofu ya kuwa viongozi kwani chama hicho kimejipanga wakati wa uchaguzi kuteua watu ambao jamii inawahitaji.
Said amesema uongozi hautokani na utajili wa fedha kwani mtu yeyote mwenye sifa njema anafaa kuwa kiongozi hivyo rushwa si kitu na CCM imejipanga kuweka wagombea wanaokubalika ndani na nje ya chama hicho.
Sophia Anthony, Mkazi wa Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi amesema kama mifumo ya udhibiti na kamati za maadili zikifanya kazi kwa kuzingatia katiba na miongozo mbalimbali viongozi wenyewe uwezo wa kuwatumikia wananchi watapatikana.
Amesema anatarajia mabadiliko makubwa ya kiutendaji yatakayo kuwa mwanzo wa vijana wengi kujitokeza kugombea nafasi za uongozi kwani vijana kwa sasa wanahofu ya kukosa mitaji ya kisiasa ambayo inatajwa ni fedha.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best