January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utafiti wa GST waongeza kasi ukataji leseni Mtwara

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam.

SERIKALI kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST), imefanya utafiti wa awali na kuainisha madini yanayopatikana katika Mkoa wa Mtwara hatua iliyosaidia wananchi kukata leseni kwa ajili ya uchimbaji wa dhahabu, ambao unawapatia kipato hasa katika maeneo ya Nanyumbu na Masasi mkoani humo.

Hayo yameelezwa leo, Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, kwa niaba ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde wakati akijibu swali namba 38 la Mbunge wa Viti Maalum, Tunza Issa aliyeuliza ni lini Serikali itafanya utafiti wa uwepo wa Madini Mkoani Mtwara.

Katika majibu yake, Dkt. Kiruswa amesema Serikali kupitia GST imefanya utafiti wa awali na kuainisha madini yapatikanayo katika Mkoa wa Mtwara.

“Mheshimiwa Spika, Miongoni mwa madini hayo ni kinywe, vito aina ya ruby, sapphire, rhodolite, Amazonite na Green tourmaline, metali aina ya dhahabu, shaba, manganese na chuma.

Madini ya viwanda kama marble na chokaa. Aidha, madini mengine ni mchanga wenye madini mazito yaani heavy minerals kama rutile, titanium, ilmenite, zircon na magnetite,” amesema Dkt. Kiruswa.

Aidha, akijibu swali la nyongeza la Malapo aliyetaka kujua kama wananchi wa Mtwara wanafahamu kuhusu uwepo wa madini hayo, Dkt. Kiruswa amesema baada ya kufanya utafiti huo, GST ilitoa mrejesho kupitia Afisa Madini Mkoa Mtwara na kukabidhi machapisho ya madini kwa Mkuu wa Mkoa na Wilaya zote za Mkoa huo.

Ameongeza kuwa, wananchi wamepata mwamko wa kukata leseni za utafiti na uchimbaji ikilinganishwa na kipindi kabla ya utafiti hasa katika madini kama graphite, pia maeneo yenye dhahabu yamepelekea wananchi kujihusisha uchimbaji ambao unawapatia kipato hasa katika maeneo ya Nanyumbu na Masasi.