November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Usindikaji bidhaa bora uzingatiwe kuleta ushindani soko la ndani na nje

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Ushindani(FCC), William Erio, ametoa elimu ya namna ya kuepukana na bidhaa bandia kwa wakulima, wafugaji na wavuvi jijini Dodoma ili waweze kutengeneza bidhaa bora zenye ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.

Mkurugenzi Mkuu huyo ameyasema hayo alipotembelea banda la FCC kwenye maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yanayoendelea Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Amesema katika kuepuka bidhaa bandia wadau mbalimbali wanapaswa kununua bidhaa zao kutoka kwa wazalishaji wenyewe au wale walioidhinishwa na wazalishaji ili wapate vitu vitakavyowasaidia kuwa na bidhaa bora.

“Kama tume tumeshiriki katika maonesho haya kwa kutoa elimu kwa umma kuelimisha kuhusu shughuli za taasisi kuwa ni pamoja na kulinda na kushajisha ushindani, kwa sababu watu wanatengeneza biashara zinazofanana

“Vile vile tumetoa elimu jinsi ya kumlinda mlaji. Kubwa tumewaambia wao kuhusu kuepukana na bidhaa bandia, kwa sababu wapo katika uzalishaji wanaweza wakaagiza bidhaa wanazitumia.

“Katika uzalishaji bidhaa hizo kama zitakuwa bandia, zitafanya bidhaa zao zikose ubora,” amesema.

Amesema kwenye kilimo wakulima wakipata pembejeo sahihi watazalisha vizuri, zikiwa bandia au za kughushi watakosa mapato mazuri.

“Tumewaeleza kuhusu vifungashio kwamba wahakikishe vinakidhi viwango wala hakuna anayeweza kughushi ili kuwaharibia soko,” amesema.