Na Penina Malundo,Timesmajira,Online
TANZANIA ni kati ya nchi zinazohitaji kupiga hatua ili kuhakikisa uwepo wa usalama barabarani unazingatiwa kulinda watembea kwa miguu na watumiaji wengine wa barabara.
Kutozingatia sheria za barabarani kunatajwa kuwa chanzo mojawapo cha ajali za barabarani kwa asilimia kubwa hapa.
Miongoni mwa sheria zisizofuatwa ni pamoja na madereva kuendesha magari kwa mwendokasi bila kujali watembea kwa miguu na wale wanaovuka kwenye vivuko vya barabarani.
Hali hii kwa asilimia kubwa inasababisha ajali kwa watembea kwa miguu au watu waliopo ndani ya magari kwa kuwasababishia vifo au hata ulemavu utokanao na ajali.
Hakuna ubishi kwamba ajali nyingi zinaweza kuzuilika iwapo madereva watahakikisha wanafuata taratibu na sheria za usalama barabarani, hasa kutoendesha kwa mwendokasi magari,kuvaa kofia ngumu kwa waendesha pikipiki na abiria wao, kutoendesha vyombo vya moto huku wakiwa amelewa.
Tafiti mbalimbali zilizofanyika zinadhibitisha kwamba mwendokasi kwa kilometa 50 hadi 46 kwa saa unaweza kupunguza asilimia sita ya vifo vinavyotokana na ajali maeneo ya mijini.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takribani watu milioni 1.35 hufa kila mwaka kutokana na ajali za barabarani, hivyo kupungua kwa mwendokasi kwenye maeneo ya mijini kunaweza kuwalinda watumiaji barabara.
Miongoni mwa watu ambao waliohataria ni pamoja na watu wanaotembea kwa miguu, wapanda baiskeli, watoto,wazee na watu wenye ulemavu.
Takwimu za Jeshi la Polisi zinaonesha makundi yaliyoathirika na ajali za Barabarani mwaka 2019/2020 katika makundi mbalimbali ikiwemo madereva, abiria, waendesha pikipiki, baskeli, watembea kwa miguu na waendesha mikokoteni.
Kwa mwaka wa takwimu za 2019 zinaonesha madereva takribani 153 walifariki dunia, huku 280 wakijeruhia, ambapo kwa mwaka 2020 waliofariki madereva walikuwa 151 na majeruhi 183.
Katika kundi la abiria waliopoteza maisha mwaka 2019 kwa ajali ni 469 na majeruhi wakiwa 1,608. Kwa mwaka 2020 hali ilipungua na abiria takribani 502 walifariki dunia na 1,355 walijeruhiwa.
Aidha, takwimu hiyo inaonesha kuwa katika kundi la waendesha pikipiki kwa mwaka 2019 vifo vilikuwa 309, majeruhi 437, huku mwaka 2020 vifo vya kundi hilo vilikuwa 236 na majeruhi 288.
Kundi la waendesha saiskeli takwimu zinaonesha vifo vilikuwa 111 na majeruhi 55 kwa mwaka 2019, huku kwa mwaka 2020 katika kundi hilo vifo vilikuwa 65 na majeruhi 30.
Kwa upande wa Watembea wa miguu takwimu za mwaka 2019 zinaonesha kuwa waliofariki walikuwa 381 na majeruhi 450, huku kwa mwaka 2020 vifo vya kundi hio vilikuwa 311 na majeruhi walikuwa 265.
Aidha, katika kundi la waendesha mikokoteni takwimu za mwaka 2019 zinaonesha vifo vilikuwa 17 na majeruhi wanne, huku kwa mwaka 2020 vifo vilikuwa vitano na majeruhi watano katika kundi hilo.
Akizungumza hivi karibuni mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Mary Kessy anasema katika muongo wa pili wa Decade of Action for Road Safety 2021/2030 unasema miongoni mwa lengo lililopo ni pamoja na kupunguza vifo na majeruhi wa ajali za barabarani zipungue angalau asilimia 50 kwa mwaka 2021 hadi 2030.
Anasema muongo huo umesema nchi wanachama wanapaswa kuendelea kuchukua hatua hadi mwaka 2030 juu ya malengo yote yanayohusiana na masuala ya usalama barabarani na kuhakikisha yanaenda sambamba na malengo ya maendeleo endelevu hususani katika lengo la 3.6.
“Lengo namba moja katika kufikia malengo ya kupunguza ajali za barabara ifikapo mwaka 2030 ni kuhakikisha kila nchi inakuwa na mpango kazi wa kitaifa na mtambuka katika kukabiliana na jamga la ajali,”anasema
Anasema ajali za barabarani zinasababishwa na vyanzo vingi moja wapo ni mwendokasi, hivyo ni vema kukawa na spidi ambayo ni salama kwa watoto na jamii kwa ujumla ili kufanya watembea kwa miguu kutembea ipasavyo.
“Tunasisitiza madereva wanapokuwa maeneo ya shuleni na mtaani kupunguza mwendo na kutumia spidi 30 ili kuwafanya watumiaji wa barabara wengine kutumia kwa uangalifu mzuri,”anasema.
Naye Mwakilishi Hospitali ya Taifa Muhimbili Kitengo cha Dharura, Dkt. Patrick Shao, anasema wagonjwa wanaofikishwa katika hosptalini kwao asilimia 75 utokana na ajali.
Anasema kati ya hao asilimia kubwa ni wanaume ambao ni nguvu kazi kati ya miaka 19 hadi 38, huku katika ajali zote asilimia 63 ni waendesha bodaboda.
Naye Meja wa Polisi Kitengo cha Elimu kwa Umma kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabara, Happiness Mdeme anasema suala zima la usalama barabarani ni jukumu la watu wote kuhakikisha madereva wanafuata sheria bila shuruti.
Anasema watembea kwa miguu wao ndio waanga wa ajali za barabarani ni muhimu kuwa kuangalia sehemu sahihi za kuvuka barabarani ili wasipate madhara.
“Madereva wapo tofauti, wapo wenye misongo ya mawazo ukiamini kuwa dereva atakuona yamkini ana tatizo lingine linamtatiza kichwani kwake na hawezi kukuona kwa wakati,hivyo mtembea kwa miguu anapokuwa anatembea anapaswa kutembea upande wa kulia kwa pembeni utaweza kumuona dereva vizuri,”anasema
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika