Na Joyce Kasiki,Timesmajira,Dodoma
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Anjela Kairuki amesema,Programu ya Jukwaa la kizazi chenye usawa inatekeleza kwa asilimia 45 hadi 50 masuala ya malezi makuzi na maendeleo ya awali mtoto ili kumwezesha mtoto kukua vyema na kujitambua na hivyo kujengeka vizuri hata katika masuala ya kiuongozi.
Akizungumza hivi karibuni katika Mkutano wa Kitaifa wa wadau watekelezaji wa Programu Jumuishi ya Kitaifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) Waziri Kairuki amesema,Programu ya kizazi chenye usawa inatekelezwa kwa miaka mitano kuanzia 2021/25 hadi 2025/26 huku akisema utekelezaji wa Programu hiyo unaenda sambamba na utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Kitaifa ya Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ya miaka mitano (PJT-MMMAM 2021/22-2025/26.
Lengo la programu hiyo ni kuongeza kasi ya jitihada za Serikali katika kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi na kiuongozi pamoja na suala zima la Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.
“Kwa mujibu wa programu yetu ya Jukwaa la kizazi chenye usawa inachukua nafasi kubwa sana kwa kuweza kuona ni kwa namna gani pia tutaipatia uzito Programu ya MMMAM inayowalenga watoto wenye umri wa kuanzia sifuri hadi miaka minane programu ambayo ni muhimu kwa Taifa katika kuleta tija kwa watoto hao na kuleta mabadiliko mbalimbali yakiwemo ya usawa wa kijinsia kwani watakuwa ni watu ambao walilelewa na kufikia utimilifu wao.”amesema Kairuki na kuongeza kuwa
“Lakini pia nipende kuwahakikishia kwamba Rais Samia Suluhu Hassan Programu ya Malezi na Makuzi ipo karibu kabisa na moyo wake,ni programu ambayo ukienda kuangalia katika programu ya Jukwaa la kizazi chenye usawa utaona namna programu hizi mbili zinavyoenda pamoja hivyo kuleta uhakika wa mtoto kuwa na mwanzo wa uhakika hata katika kujitambua.”
Kwa mujibu wa Waziri huyo, hapa duniani tafiti zilizofanyika zinaonyesha unapowekeza dola moja kwa mtoto wa umri wa sifuri hadi miaka minane kwenye uwekezaji huo una uhakika wa kupata siyo chini ya dola nyingine 13, na kusema kuwa upo uhakika hapo baadaye katika kuwekeza kwa kundi hilo la watoto.
“Kwa hiyo ninachopenda kusisitiza katika PJT MMMAM katika yale maeneo machache yaliyochaguliwa ya kipaumbele ni eneo la Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto imo katika maeneo 11 ambayo kama nchi pia tumeweka ahadi za nchi Kimataifa kupitia Umoja wa Mataifa,na humo ndani asilimia 45 mpaka asilimia 50 itawekezwa katika eneo hili la malezi makuzi na maendeleo ya mtoto ,
“Kwa hiyo hii inaonyesha kabisa kupitia Jukwaa la kizazi chenye usawa ,eneo la MMMAM pia lipo karibu kabisa na Rais wetu,ukiacha mambo mengi aliyofanya katika nchi hii katika kipindi chake cya uongozi ,ukisema uguse maeneo matatu makubwa ya msingi yaliyo karibu kabisa na moyo wa Rais ambalo pia ataacha alama katika Taifa letu ni pamoja na eneo hili la MMMAM .
Aidha kupitia Programu ya Jukwaa la Kizazi chenye usawa Wizara ya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum imekamilisha Kanzidata inayolenga kuwezesha ukusanyaji na utunzaji wa taarifa zinazohusu wasifu, ujuzi na utaalam wa Wanawake katika nyanja mbalimbali hapa nchini.
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari