Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar
UONGOZI wa Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa mstari wa mbele kusukuma ajenda za kumkomboa mtoto wa kike kwenye changamoto zinazo mkabili, ambapo chini ya utawala ameboresha upatikanaji wa elimu kwa wasichana na wavulana kufikia usawa wa kijinsia wa 1:1.
“Hilo liliwezekana kwa kuanzishwa kwa elimu ya msingi bila ada na kuongeza ufadhili wa elimu hadi asilimia 19 ya bajeti yote katika kipindi cha 2021/22 – 2023/24.
Pia Serikali yake imewekeza kwa viongozi wanawake kwa kujenga shule maalum za wasichana watakaochagua kusoma masomo ya sayansi na ameanzisha Programu ya Samia Scholarship, ambayo inatoa ufadhili wa asilimia 100 kwa wanafunzi wenye ufaulu mzuri wa masomo hayo.
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango alipokuwa akifungua mkutano wa masuala ya uongozi kwa wanawake kisekta jjiini Dar es Salaam.
Amesema, uwekezaji mkubwa umefanywa kwenye Sekta ya Afya, Maji, Elimu na Nishati zimekuwa jitihada za makusudi za kumuinua mtoto wa kike kutokana na baadhi ya changamoto zilizokuwa zinawakabili kwa kipindi kirefu ikiwepo mila potofu pamoja na mfumo dume uliokuwa umeshamiri miongoni mwa baadhi ya jamii.
“Jitihada hizo upande wa Sekta ya Afya, kupitia huduma inayotekelezwa na mpango wa M-mama umewezesha kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa sasa.” Amesema Dkt. Mpango
Kuhusu sekta ya maji, alisema Rais Samia amefanya jitihada za kumtua mama ndoo kichwani kwa kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa uhakika na kumpunguzia adha mama kufuata maji umbali mrefu, kwani ameongeza bajeti ya maji kutoka shilingi bilioni 709.4 kwa mwaka wafedha 2022/23 hadi kufikia shilingi bilioni 756.2 kwa mwaka fedha 2023/24”.
Dkt. Mpango amesema, Serikali imedhamiria kuwa na nishati safi na salama kwa mazingira salama kwa jamii, ambapo shabaha ya serikali nikuhakikisha ifikapo 2030 matumizi ya nishati iliyo safi na salama kwa mazingira inafikia asilimia 80 na hususan ni maeneo ya vijijini ambapo matumizi ya nishati isiyo rafiki imekithiri.
Kuhusu elimu Makamu wa Rais Dkt. Mpango, alisema zimekuwepo jitihada zenye tija kwa watoto wa kike kwa kuwajengea Shule Maalumu za Bweni ili waweze kuhitimu masomo yao na kufikia matamanio yao ya kile wanachotaka kufanya katika maisha yao.
“Wapo baadhi ya watoto wa kike walikuwa wamepata ujauzito na kujifungua watoto, Serikali ya Dkt. Samia imehakikisha, wanarudi shuleni hata baada yakujifungua na kuendelea na masomo,” alisema Dkt. Mpango.
Wakati wanawake wanaunda asilimia kubwa ya wafanyakazi wote katika sekta ya afya, ripoti za kimataifa zinakadiria kuwa, ni asilimia 25 tu ya nafasi za juu na asilimia 5 ya nafasi za juu za uongozi zinazoshikiliwa na wanawake.
Alisema changamoto zinazowazuia wanawake kushika nyadhifa za juu na za juu za uongozi katika sekta ya afya zinaweza kutofautiana kutoka mkoa mmoja hadi mwingine kulingana na mambo mengi.
“Changamoto hizi zinaweza kuanzia mgawanyo wa majukumu kati ya wanawake na wanaume na mivutano ya kusawazisha majukumu ya kazi na nyumbani; ukosefu wa wanawake waliofanikiwa au wachache wa kuwatia moyo wanawake wengine kama mifano ya kuigwa;
Ukosefu wa mitandao na washauri kwa wanawake; ukosefu wa kujiamini miongoni mwa baadhi ya wanawake; mila za uzalendo zilizotawaliwa na wanaume ambazo zinapendelea wanawake; unyanyasaji katika maeneo ya kazi, na uandikishaji duni wa wasichana shuleni kutaja wachache.”
Juu ya changamoto hizi kuna changamoto mpya zinazohusiana na maendeleo ya haraka ya teknolojia katika sekta ya afya, mabadiliko ya hali ya hewa, uchafuzi wa mazingira, na vikwazo vya kiuchumi,”amesema.
Akimkaribisha Makamu wa Rais kufungua mkutano huo, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, amesema mkutano huo imekuwa ni heshima kwa nchi kupokea, kwani ni kwa mara ya pili unafanyika katika bara la Afrika awali ulifanyika nchini Rwanda.
“Kutokana na Nchi kufanya vizuri katika vile viashira vikuu vyakupima afya Duniani kwani kama nchi tumeweza kupunguza vifo vya mama wajawazito kwa Zaidi ya asilimia 80 kwani mbali yakupunguza vifo vya zizazi hai lakini pia kwa upande wa vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano kutoka vifo 67 hadi vifa 45 kati vizazi 1000” amesema Ummy.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amesema, suala la Afya hakuna wakuachwa nyuma kwa wanawake na wanaume Ili tuweze kufanikiwa kwenye Afya”. Amesema Dkt. Jingu
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa