January 26, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Unapodai huduma ya maji, jenga utamaduni wa kutunza vyanzo vya maji’

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imeweka nguvu katika miradi mbalimbali ambayo inagusa maisha ya kila Mtanzania katika kufanikisha kazi za kila siku. Kati ya miradi hiyo muhimu katika maendeleo ya wananchi ni uwekezaji katika sekta ya maji, maeneo ya mijini na vijijini.

Hata hivyo, katika baadhi ya maeneo wananchi wenyewe, kwa makusudi au kutokujua wanaharibu maeneo muhimu ambayo ni sehemu mahsusi yamsingi katika kuwafikishia huduma ya majisafi na salama katika makazi yao. Hali hii inasababisha adha kwa jamii, na kuhatarisha uendelevu wa vyanzo vya maji.

Sophia Hussein (49) mkazi wa Waranga, Katesh wilayani Hanang Mkoa wa Manyara anasema ni lazima kuamka mapema na kufunga safari kwa umbali wa zaidi ya kilomita tano ili kuwahi maji katika mashimo ya kuchimba katika mabonde.

Sophia, mama mwenye familia inayomtegemea kwa kazi za nyumbani kama mama, anasema endapo unachelewa kuwahi mapema, basi unajiandaa kupambana na mifugo ili kupata maji, maji ambayo sio salama.

Anasema ukichelewa unakuta mifugo imeshatumbukia na kutibua maji katika mashimo.Maisha katika nchi zinazoendelea hususan katika suala la majisafi na salama inawezekana jambo hili likawa uhalisia kwa baadhi ya wanafamilia.

Hapa nchini, Serikali imeweka nguvu kubwa katika kuhakikisha wananchi ambao ndio wadau wake wakuu wanapata huduma hii muhimu ya majisafi na salama karibu na makazi na sio kutembea umbali mrefu.

Maji ni rasilimali muhimu kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya kiuchumi, na rasilimali hii haina mbadala. Tafiti zinaonyesha kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa na rasilimali za maji juu ya ardhi zenye kilomita za ujazo 92.27 na chini ya ardhi kilomita za ujazo 38.

Kupitia rasilimali hii nia na lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha wakazi wa vijijini wanapata huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 95 itakapofika mwaka 2020.

Ni wazi kuwa rasilimali za maji zinahitaji kulindwa na kutunzwa kwa sababu hazina mbadala. Wakati wananchi wengi wanaelewa umuhimu wa kutunza mazingira, baadhi yao ni wazito au kwa ukaidi wamekua waharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji.

Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso akiangalia maji yanayochotwa kwa ajili ya matumizi ambayo si salama mara baada ya kukagua chujio la mradi wa maji wa Katesh, Babati kabla ya kuweka jiwe la msingi. Mradi huo umefanikishwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Babati (BAWASA),na unatarajiwa kutoa huduma ya majisafi na salama kwa miaka 40 ijayo.Mpigapicha Wetu

Wapo ambao ni viranja na vinara wa kufanya shughuli mbalimbali katika vyanzo vya maji, bila kujali mahitaji ya wananchi wengine. Hali hii inazua maswali mengi, anayelima katika chanzo cha maji na kufuga mifugo kudai huduma ya majisafi na salama wakati anashiriki kuharibu chanzo cha maji.

Mkuu wa Wilaya ya Babati Elizabeth Kitundu ambaye asilimia 63 ya wakazi wa wilaya anayoiongoza wanapata majisafi na salama anasema moja ya changamoto katika miradi ya maji ni uvamizi na uchafuzi wa vyanzo vya maji.

Pamoja na hilo, Wastani wa upatikanaji maji mjini Babati utaongezeka siku za usoni na kufikia asilimia 95 baada ya mradi wa maji wa Bonga unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Babati (BAWASA) kukamilika.

Mradi huo utazalisha kwa saa moja lita 40,000. Aidha, vijiji vya jirani vitaunganishwa katika mradi huo. Juhudi hizi ni vizuri zihusishe wananchi katika kutunza vyanzo vya maji ili miradi ya maji iwe endelevu.
Hata hivyo, Diwani wa Minjingu Michael Milao anasema jambo la msingi ni kwa watalaam kuwashirikisha wananchi katika masuala ya maji.

Anaongeza kuwa wananchi wakishirikishwa na kupewa elimu ya kutosha kila jambo litakaa sawa. Anaongeza kuwa kutokua na elimu na taarifa za kutosha kunasababisha baadhi ya wananchi kufanya mambo wanavyoamini.

Suala hili la elimu linaungwa mkono na Mwenyekiti wa Kijiji cha Tsamas Jumanne Selemani anayesema kutoshirikishwa kwa wananchi na kupewa elimu ni tatizo. Anasema hawawezi kukabidhiwa mradi tu, bila kushirikishwa toka mwanzo na kujua mbinu za utunzaji vyanzo vya maji.

Shughuli za kibinadamu zinasababisha kwa kiwango kikubwa vyanzo vya maji kukauka kabisa au kutoa maji kwa msimu. Ni muhimu kutoa elimu ya utunzaji vyanzo vya maji kuepusha miradi ya maji kuvamiwa kwa shughuli mbalimbali. Kwa mfano, mkoa wa Manyara vyanzo vyake vikuu vya uchumi ni kilimo na ufugaji kwa kuajiri asilimia 83 ya wakazi.

Shughuli nyingine zimeajiri asilimia 17 ikiwamo utalii,uchimaji madini, uvuvi, biashara, viwanda vidogo na kazi za ofisi. Ni jambo la msingi wananchi wa mkoa huu wapewe elimu kila wakati kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji.

Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso akiongea na wakazi wa Waranga, Katesh anasema hivi karibuni ni jambo la msingi kulinda vyanzo vya maji ili kuwa na uhakika wa huduma endelevu ya majisafi na salama. Wakazi hao wameambiwa ukweli mchungu kuwa bila kuwa na chanzo cha uhakika cha maji, kufanikisha mradi wa maji ni uongo, kama miundombinu ya maji imewekwa itakosa maji.

Aweso anaeleza kuwa kulinda vyanzo vya maji ni jukumu la kila mwananchi kwa sababu maji hayana mbadala, na kila mtu anayahitaji kila siku, kila wakati, iwe nyumbani, ofisini, shuleni au katika shughuli nyingine ikiwemo kilimo, ufugaji na ujenzi.

Hata hivyo,Waziri Aweso akiongea na wananchi wakati akifungua na kuweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Katesh uliofanikishwa na BAWASA, kasema hatamvumilia mkandarasi anayedanganya wananchi kwa kuweka miundombinu ya maji wakati hajafanya utafiti wa kina kupata chanzo cha maji cha uhakika. Mradi wa Katesh unatarajia kutoa huduma kwa miaka 20 ijayo kwa wakazi 40,000 na unavisima vinavyotoa lita za maji 150,000 kwa sasa.

Waziri Aweso anasema hadi Septemba 2018 takwimu zinaonyesha katika mkoa wa Manyara upatikanaji wa maji vijijini ulikuwa asilimia 52 na Babati mjini asilimia 75, ilhali mkoa huo una vyanzo vya maji mbalimbali ikiwamo visima virefu 296, visima vifupi 320, chemchemi 93 na mabwawa 123.

Wakati wa ziara ya mradi kwa mradi Waziri Aweso amebaini baadhi ya vyanzo vya maji kuvamiwa kwa shughuli mbalimbali, ikiwamo kilimo, ufugaji na kazi za kufyatua tofali hali inayohatarisha upatikanaji wa maji kuwa endelevu, na hivyo kukuza adha ya upatikanaji majisafi na salama.

Kuhusu hili Waziri Aweso amewaelekeza viongozi na wananchi mkoani Manyara kulinda na kuelimisha kuhusu umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji kwa maendeleo ya kila mwananchi. Hairuhusiwi kufanya shughuli yoyote ndani ya mita 60 kutoka chanzo cha maji, kila mkazi wa Manyara anatakiwa aelewe.

Pamoja na hilo, Waziri Aweso antumia wasaa huo akiwa katika mradi wa maji wa Gehandu mkoani Manyara kuwaelekeza watalaam wa maji kote nchini, kuacha mara moja kuweka miundombinu ya maji wakati bado hawajatafiti kupata chanzo cha uhakika cha maji.

Waziri Aweso anasema hili,ni ubabaishaji, sio weledi bali kuchezea raslimali za wananchi, na wakati huduma ya majisafi hawapati pamoja na gharama kubwa kutumika kuweka miundombinu ambayo inakosa maji.

Anaongeza kuwa haiwezekani mtaalam aruhusu malipo kwa mkandarasi aliyefanya kazi kijanjajanja, Mkandarasi huyo kampuni ya Vest Tanzania Ltd ametakiwa kurudi katika eneo la mradi mara moja.

Pamoja na hilo, Waziri anawaelekeza wataalam wa rasilimalimaji kanda ya kati ndani ya siku saba kwenda katika eneo la Gehandu, wilayani Hanang’ na kufanya utafiti ili kupata chanzo cha maji cha uhakika chenye maji yakutosha. Aweso anasema wananchi hawawezi kukaa kusubiri mradi wa maji kwa muda mrefu kiu yao ni maji sio maneno.

Kuhusu kulinda vyanzo vya maji, Lazaro Msengi, Afisa Rasilimalimaji kutoka Bonde la kati anasema kila mwananchi anatakiwa kuelewa kuwa maji ni uhai, lazima kutunza vyanzo hivyo na kuvilinda kwa kuweka mipaka ili kuepuka shughuli za aina yoyote katika maeneo hayo.

Msengi anawaambia Wanamanyara siri iliyowazi, pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, rasilimali maji inaisha kwa kasi ya kutisha. Hivyo, endapo wataendelea kuingiza mifugo katika vyanzo vya maji na kulima mazao, ni dhahiri kuwa haitachukua muda mrefu wataomba huduma ya majisafi na salama wakati vyanzo vya kutoa maji hayo wameshavimaliza wenyewe kwa tamaa ya kufuga mifugo au kufanya kazi za kilimo.

Kazi za kilimo na ufugaji zimeonekana kushamiri katika mkoa huo ingawa wakazi wake wanahitaji sana huduma ya majisafi na salama karibu na makazi yao.

Kufuatia hilo, Mkuu wa Wilaya ya Hanang’ Joseph Mkirikiti anasema kuwa shughuli zote katika vyanzo vya maji, ndani ya mita 60 zikome mara moja. Anasema ametoa muda huo kwa kila mwananchi anayejua yupo ndani ya chanzo cha maji, kwa kuweka mifugo, kufyatua matofali au kilimo awe amejiondoa mwenyewe kabla ya kuondolewa kwa nguvu.

Mkirikiti akiongea na wananchi katika mkutano uliofanyika katika mradi wa maji Endasaboghechan na Waranga anasema rasilimali fedha ya serikali inayotumika katika miradi ya maji ni kubwa, na hawezi kuvumilia kumuona mtu anaingia katika eneo la chanzo cha maji kwa tamaa ya kulima au kufanya kazi yoyote, kwa kusema hilo haliruhusiwi na hatavumilia.

Waziri Aweso anasema timu ya watalaam wa maji kutoka Wizara ya Maji itatumwa mara moja kuchunguza miradi yote isiyokidhi mahitaji ambapo anasema lazima tatizo la maji liishe ila atakayehujumu miradi ya maji lazima Sheria ichukue nafsi yake.

Waziri Aweso, katika mikutano mbalimbali na wananchi mkoani Manyara ameainisha kuwa Jumuiya za Watumia Maji lazima zisajiliwe, na makusanyo ya fedha yapelekwe benki na sio kugawana. Fedha hizo ni kwa ajili ya kuhakikisha mradi unakua endelevu, na huduma ya majisafi na salama inakua ya uhakika kwa wananchi.

Katika kuhakikisha majisafi na salama yanawafikia wananchi wa Simanjiro mkoani Manyara Waziri Aweso ameipa siku tano, hadi mwishoni mwa wiki ya kwanza ya mwezi Novemba 2018, Wakala ya Uchimbaji wa Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) kukamilisha kazi ya majaribio ya pampu katika mradi wa maji Mirerani.

Hatua hiyo itasaidia kujua kiwango na ubora wa maji kabla hayajasambazwa kwa wananchi. Kukamilika kwa kazi hiyo, kutafuatiwa na hatua ya usanifu wa mradi itakayofanywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Babati (BAWASA).

Hatua hizo zinazochukuliwa, pamoja na kulinda vyanzo vya maji kwa kuzuia kazi mbalimbali zinazofanyika, hakika Mkoa wa Manyara utaongeza wastani wa upatikanaji maji na kulinda vyanzo. Ni jukumu la wananchi, na viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuelimisha na kutoa taarifa endapo chanzo cha maji kinavamiwa au kuwa katika hatari yoyote ili watalaam wachukue hatua na kushauri.

Bila wananchi kulinda vyanzo vya maji, watabaki kudai huduma ya maji wakati vyanzo vya maji vinavyowazunguka wamevimaliza wao wenyewe kwa tamaa ya kilimo au kazi nyingine za biashara.

Kuhakikisha miradi ya maji inafanyika vizuri, Mkurugenzi Mtendaji wa BAWASA Mhandisi Yazidi Msuya anasema ni vizuri wataalam wakishirikiana kwa sababu itasaidia kuondoa makosa ya kitalaam na kukamilisha miradi mapema zaidi.

Anaongeza kuwa ni vigumu kwa mtaalam mmoja kusimamia na kuratibu kila jambo katika mradi wa maji bila kushirikisha wataalam wengine kwa sababu miradi inahusisha masuala mtambuka.

Tusiangamie kwa kukosa maarifa, tuelimishane na kujifunza kutoka kwa wengine. Kila mmoja atimize wajibu wake. Wananchi wote, ikiwemo Manyara, tulinde na kutunza vyanzo vya maji kwa maendeleo yetu sote, kwa sasa na vizazi vijavyo.