Na Zena Mohamed,TimesMajira Online
SERIKALI imesema kuwa nchi inaulazima wa kuwa na mpango wa kitaifa wa kupambana na umwagikaji mafuta baharini na maziwa makuu pale inapotokea ajali za meli za usafiri wa abiria na za mizigo, kwani umwagikaji wa mafuta hayo unaathiri uchumi wa nchi na kuua viumbe ambavyo vinaishi baharini.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Sekta ya Uchukuzi,Stella Katundu kwenye kikao cha Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na wadau kujadili mpango wa kitaifa wa kupambana na umwagikaji mafuta baharini.
Sambamba na maziwa makuu ambapo amesisitiza kuwepo mpango wa kusafisha mafuta baharini kwa haraka inapotokea dharura.
Amesema, Serikali imehuwisha mpango wa kitaifa wa kupambana na umwagikaji wa mafuta baharini utakaosadia kulinda mazingira na viumbe vingine ikiwemo samaki na kuimarisha uchumi wa bluu.
Mkurugenzi Katondo amesema, lengo la mpango huo wa kitaifa ni kusadia kupamba na umwagikaji wa mafuta bahari pamoja na maziwa makuu.
Amesema kuwa, mpango huo ulikuwepo toka mwaka 2016, lakini hivi sasa umehuwishwa kutokana na mabadiliko mbalimbali yaliyojitokeza katika sekta hiyo.
“Awali mpango huu ulikuwa chini ya SUMATRA, lakini kutokana na SUMATRA kuvunjwa Serikali iliamua kuuleta katika Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC) ili kuweza kuutekeleza kwa kushirikiana na wadau wengine,”amesema Katondo.
Pia amesema kuwa, Tanzania ni moja kati ya nchi zinazohusika katika usafirishaji baharini na kwenye maziwa makuu na vyombo hivyo vinatumia mafuta na vinabeba mizigo ya nishati hiyo mpango huo utasaidia kuwepo na namna nzuri ya kusafisha pale yanapovuja.
“Mpango huu utasaidia kuwa na vifaa ambavyo vitatumika kuondoa au kusafisha mafuta pindi yanapovuja baharini au katika maziwa makuu ili kuokoa mazingira pamoja na viumbe vilivyomo kama vile samaki,”amesema.
Vilevile amesema kuwa, kitendo cha kuvuja kwa mafuta bahari kina athari kubwa kwa viumbe vilivyomo hivyo ni lazima iwepo namna sahihi ya haraka kuyaondoa katika eneo hilo.
Akizungumzia hali ya umwagikaji wa mafuta baharini kwa hivi sasa amesema kuwa, siyo mbaya kutokana na udhibiti unaofanywa katika vyombo vya usafirishaji kama vile meli na boti.
Kaimu msajili wa meli, Mhandisi Alfred Waryana amesema kuwa, mpango huo utasaidia taifa kuwa na vifaa vya kisasa vya kusafisha na kuondoa mafuta yanapovuja baharini katika vyombo vya usafirishaji.
“Lakini mpango huu utawezesha kusadia kupata msaada kwa mataifa mengine yenye vifaa vya kisasa pale linapotokea janga kubwa la kuvunja kwa mafuta baharini ili kusaidia kuyaondoa kabla ya kuleta athari kubwa kwa viumbe, pia mpango huu utasaidia kujenga ushirikiano na mataifa mengine,”amesema.
Mhifadhi, ufundi na uwezeshaji wa hifadhi za bahari nchini, Clever Mwaikambo alisema, wanaishukuru Serikali kwa kufanikisha kupatikana kwa mapango huo ambao utakuwa mkombozi wa mazingira na kulinda uchumi wa bluu.
Amesema kuwa, ni lazima Taifa kuwa na vifaa vya kusafisha na kuondoa mafuta pale yanapovuja baharini ili mazingira kuendelea kubaki salama pamoja na viumbe vilivyomo.
“Pia tunaiomba Serikali kwa kuwa mpango huu hivi sasa unaratibiwa na TASAC, basi itenge fedha ili kununua vifaa vikubwa kwa ajili ya kusafisha mafuta yanapovunja wenzetu Kenya wamenunua mitambo mikubwa sana ukilinganisha na tuliyo nayo hapa kwetu,”amesema Mwaikambo.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa