Joyce Kasiki
ELIMU ya darasa la awali kwa muda mrefu imekuwa ikichukuliwa ndivyo huku ikionekana kama ni sehemu ya watoto kwenda kucheza bila faida yoyote.
Huko nyuma wanafunzi wa darasa la elimu ya awali wao ndio walikuwa wa kusomea madarasa mabovu au chini ya miti kunapokuwa na uhaba wa vyumba vya madarasa kwa kuonekana kwamba wanachokifanya hakikuwa na maana.
Ilisahaulika kwamba wakati huo ndio muda ambao mtoto anapaswa asome katika mazingira mazuri ili ubongo wake ukae sawa kwa ajili ya kupokea anayojifunza na hivyo kumjengea msingi mzuri tangu mwanzo.
Hata hivyo ukweli ni kwamba darasa la awali ambao wengi huita chekechekea ni eneo muhimu ambalo mtoto anaanza kujifunza mambo mengi kupitia nyimbo,hadithi na michezo mbalimbali.
Ingawa wazazi wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu ujifunzaji wa mtoto kupitia michezo na nyimbo lakini ukweli ni kwamba kupitia hiyo michezo ,nyimbo na hadithi na kuona vitu mbalimbali mtoto anaanza kujifunza na ubongo wake kuendelea kuchangamka na kukua vizuri.
Sasa mtoto anawezaje kujifunza katika darasa hilo la awali ambalo anapaswa kuona kitu,namba,wanyama na vitu vingine vingi kama darasa halina miundombinu ya kutosha ya kumwezesha kujifunza pasipo hata kushika kalamu na karatasi.
Ni muhimu kuboreshwa kwa madarasa ya watoto hao na kuyafanya kuwa changamshi na ya kuvutia ili wawe na darasa zuri lenye zana za kutosha za kumwezesha mtoto kujifunza lakini pia kupenda shule na hivyo kupunguza utoro darasani.
Mtaalam wa Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto kutoka shirika lisilo la kiseriali la Children in Cross Fire (CiC) Frank Davis anasema Miundo mbinu kama madarasa, inapokuwa ya kutosha inapunguza wingi wa watoto kwenye chumba kimoja au kuondoa changamoto ya chumba kimoja kutumika na madarasa zaidi ya moja huku akitolea mfano awali na darasa la kwanza.
Vilevile anasema zana za kutosha hurahisisha tendo la ujifunzaji na ufundishaji kwa watoto hasa kupitia michezo na shughuli mbalimbali zinazotendwa na mtoto lakini pia madarasa changamshi yaani yaliyosheheni zana yanachochea dhana ya ujifunzaji kwa njia ya vitendo (michezo) ambayo ndio bora kwa Elimu ya Awali ili kumjengea umahiri mtoto.
Aidha anasema Madarasa changamshi huvutia watoto kwenda Shule na hivyo kupunguza utoro kwasababu watoto wanapenda michezo.
Meneja Mradi wa WatotoWetuTunuYetu wa Shirika lisilo la Kiserikali la Children in Crossfire Faraji Paragha anasema kutokana na umuhimu wa elimu ya darasa la awali ,Shirika hilo limefanya uboreshaji wa madarasa ya elimu ya awali zaidi ya 900 kwa mkoa mzima wa Dodoma.
Anasema CiC ilianza uboreshaji huo kwa awamu ya kwanza na ya pili kwa wilaya mbili za Kongwa na Chamwino ambapo madarasa 232 yaliboreshwa kwa kuwekewa miundombinu ya ujifunzaji wa watoto wa darasa hilo.
Paragha anasema wamefanya uboreshaji wa miundombinu hiyo kwa awamu ya tatu kwa shule moja kila kata katika halmashauri za Chemba ,Bahi,Mpwapwa ,Kondoa Mji,Kondoa Vijijini na Dodoma Jiji ambapo shule 146 zilifanyiwa uboreshaji wa madarasa hayo ya awali.
Kwa mujibu wa Paragha ,pia umefanyika uboreshaji wa awamu ya nne ambapo mkoa mzima wa Dodoma shule 576 uboreshaji umefanyika.
Akizungumza Bungeni hivi karibuni,Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Seriali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa anasema Serikali imetenga fedha wa ajili ya ununuiz na vifaa viivyoboreshwa vya kufundishia na kujifunzia kwa elimu ya awali kwenye shule 4,500 pamoja na ununuzi wa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule 130 za msingi na sekondari.
Kadhalika, Serikali inatarajia kutoa mafunzo endelevu ya walimu kazini (MEWAKA) kwenye shule za awali na msingi kwenye halmashauri 140, kutekeleza mpango wa shule salama kwenye shule za awali na msingi.
Agnes Peter mkazi wa Swaswa Dodoma Jiji anasema anafahamu umuhimu wa elimu hasa kwa darasa la awali huku akisema ueewa huo ameupata katika wilaya ya Chamwino ambako huwa anaenda kuwatembelea ndugu zake.
“Kule Chamwino huwa naona ndugu zangu wakienda shuleni kushiriki katika utengenezaji wa vitu vya watoto darasani kama vile vitu vya kuhesabia na michezo mbalimbali,lakini elimu hii bado haijafika vizuri kwa jamii ili iweze kuona kwa darasa la awali siyo la kubeza.”anasema Agnes
Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prisca Myalla akizungumzia mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa miaka mitatu anasema uboreshaji wa Miundombinu ya elimu unaoendelea kufanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umekuwa chachu ya ongezeko la uandikishwaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza na awali Jiji la Dodoma kuongezeka kutoka asilimia 98 hadi 115 kwa mwaka 2024.
Anasema kupitia mradi wa BOOST na EP4R Serikali imeendelea kujenga miundombinu ya darasa la elimu ya awali ambapo Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeweza kujengewa madarasa mapya na kuboreshewa miundombinu, hali iliyopelekea wazazi na jamii kuona fursa ya kuwapeleka watoto wao kupata elimu.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Dodoma English Medium, Evodius Kanizio anaishukuru serikali kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 458 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Mtaala wa kingereza jijini Dodoma.
Anasema shule hiyo ina wanafunzi 267 kuanzia darasa la awali hadi darasa la tatu.
Kutekelezwa kwa Programu Jumuishi ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto in kutatua changamoto za malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa watoto wenye umri wa miaka sifuri hadi minane ili watoto wote hapa nchini wafikie ukuaji timilifu na hivyo kuwa na tija kwao wenyewe na Taifa kwa ujumla.
More Stories
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya