December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Umoja wa Mataifa waidhinisha pendekezo matumizi ya bangi

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online

BARAZA la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya, kwa pamoja limeidhinisha pendekezo la Shirika la Afya Duniani (WHO), la kuondoa bangi katika orodha ya dawa hatari zaidi duniani na kutambua kuwa mmea wenye manufaa kitiba.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Utangazaji la Uingereza, baraza hilo limekubaliana kuondoa bangi pamoja na utomvu wa bangi katika orodha ya kundi la mihadarati (dawa zinazohitaji kudhibitiwa). Dawa hizo ambazo zinalevya na kumfanya mtu kuwa tegemezi zinajumuishwa katika kundi la Scheduled IV, ambazo hutambuliwa kuwa hatari kwa matumizi ya tiba japo kwa athari ndogo.

Baraza hilo lenye wanachama kutoka nchi 53, waliopiga kura kuunga mkono ni nchi 27 huku 25 wakipinga kutambua bangi kama ina manufaa, huku nchi moja tu ndio haikupiga kura (Ukraine).

Kati ya nchi zilizopiga kura kuidhinisha bangi ni pamoja na Marekani na nchi, huku China, Misri, Nigeria, Pakistan na Urusi zikiwa miongoni mwa nchi zilizopinga kuhalalisha.

Kwa hatua hiyo mmea wa bangi utatambulika rasmi na kukubalika kwa kuondolewa katika kundi la dawa za kulevya jambo ambalo litaufanya mmea huo kuwa dawa na tiba na kutoa fursa kwa watafiti kufanya tafiti zaidi za bangi.

Bangi imekuwa katika kundi la dawa zinazodhibitiwa kwa zaidi ya miaka 59. Wanaharakati kutoka sehemu mbalimbali duniani wamekuwa wakipigia mmea huo kuhalalishwa ikiwa ni pamoja na wasanii maarufu duniani pamoja na muziki wa reggae ambao asili yake ni Jamaica.

Baadhi ya wasanii waliopiga debe kali ni pamoja na Marehemu Bob Marley na Peter Tosh, huku moja ya nchi za Ulaya zilizoidhinisha bangi kuvutwa hadharani kwa muda mrefu zaidi ni Uholanzi.