Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amesema kitita kipya cha mafao cha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kinaenda kuboresha upatikanaji wa huduma bora za kibingwa na ubingwa bobezi karibu na wanachama.
Akizungumza Bungeni wakati akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025,Waziri Ummy amesema katika mwaka wa fedha 2023/24, Wizara iliidhinisha matumizi ya kitita kipya cha mafao cha NHIF cha mwaka 2023 ambacho kimeoanishwa na Orodha Muhimu ya Dawa (NEMLIT) pamoja na Mwongozo wa Tiba wa Taifa (STG).
Aidha amesema,kitita hicho kimezingatia maendeleo ya teknolojia ya tiba, hali halisi ya bei katika soko na uwezo wa Mfuko kugharamia huduma hizo huku ukiendelea kuwa endelevu kwa kuzingatia ushauri wa taarifa ya mapendekezo ya Tathmini ya Uhai na uendelevu kwa kipindi kinachoishia 30 Juni 2021.
Ummy ametaja mambo makubwa yaliyofanyiwa maboresho katika kitita cha mafao cha mwaka 2023 ni pamoja na kuongezeka kwa dawa mpya 254 zenye ufanisi ambazo awali wanachama walilazimika kutoa fedha taslimu kwa kuwa hazikuwa sehemu ya Kitita cha mwaka 2016 na dawa 178 ambazo hazikuwa kwenye orodha ya Dawa Muhimu ya Taifa (NEMLIT) zimeongezwa baada ya Wizara kufanya mapitio ya NEMLIT na kutoa nyongeza na hivyo kujumuishwa katika kitita cha NHIF cha mwaka 2023 .
Pia amesema kitita hicjo kimesaidia kuwaepusha wanachama kuendelea kutumia dawa zisizo na matokeo chanya hivyo kuwaepusha na magonjwa yasiyoambukizwa kutokana na usugu wa dawa husika ,kusogeza huduma za kibingwa na ubingwa bobezi karibu na wananchi kuanzia Hospitali za ngazi mkoa na Kanda na kuondoa usumbufu wa kukosa baadhi ya dawa na huduma nyingine kama matibabu ya saratani, upasuaji wa mifupa, upasuaji wa moyo ambazo awali zilikuwa zinatolewa katika Hospitali za ngazi ya Taifa tu,kuweka usawa wa ada ya usajili na kuwaona madaktari wenye elimu na taaluma zinazofanana kwa wanufaika wa NHIF.
Aidha amesema kwa kitita kipya Daktari Bingwa katika ngazi ya Rufaa Mkoa ada imeongezeka kutoka Shilingi 15,000 hadi Shilingi 25,000 ambapo ni sawa na ada ya kumuona Daktari aliyeko ngazi ya Kanda na Taifa. Hatua hii itavutia madaktari bingwa kufanya kazi katika Hospitali za Rufaa za Mikoa hususan ya pembezoni.
Vile vile amesema ada ya usajili na kumuona daktari kwa wanufaika wa NHIF kwa ngazi ya Wilaya imeongezeka kutoka Shilingi 5,000 hadi Shilingi 7,000,kwa ngazi ya Kituo cha Afya ada imeongezeka kutoka Shilingi 2,000 hadi Shilingi 7,000 na kwa ngazi ya Zahanati ada imeongezeka kutoka Shilingi 1,000 hadi Shilingi 3,000.
“Hatua hiyo itaongeza mapato katika vituo na motisha kwa watumishi wa Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya na hivyo kuvutia Madaktari kufanya kazi katika vituo hivyo 68. “amesema Ummy na kuongeza kuwa
“Mheshimiwa Spika, kwa kutambua kuwa huduma za afya zinabadilika mara kwa mara kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia na hali halisi ya soko, ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza na kukua kwa Sekta ya Afya ya umma na binafsi, NHIF itafanya mapitio ya kitita cha mafao yake kila baada ya miaka miwili “
Katika hatua nyingine Ummy amesema ,Serikali inakusudia kuanzisha chombo cha Kitaifa cha Udhibiti wa Bei za Huduma za Afya katika ngazi zote nchini kama inavyofanyika kwenye udhibiti wa gharama za maji, umeme na mafuta.
Amesema,lengo ni kudhibiti ukuaji holela wa gharama za afya kwa wananchi hususan wasio na bima ya afya
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi