December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ummy atoa miezi sita kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Songwe

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Songwe.

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amewaagiza watendaji wa Wizara hiyo kuhakikisha ndani ya miezi sita iwe imekamilisha ujenzi wa majengo matatu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe ili ianze kutoa huduma na kukamilisha muunganiko wa huduma katika Hospitali hiyo ya rufaa ya Mkoa .

Ametoa agizo hilo leo Septemba 13, 2023 wakati  akizungumza na watumishi , ikiwa ni hitimisho la   ziara yake ya siku tatu Mkoani hapa iliyolenga  kukagua hali ya utoaji huduma za afya katika vituo vya afya na Hospitali zilizopo kwenye  Halmashauri na Wilaya, pamoja na ile ya rufaa ya Mkoa wa Songwe.

Waziri Ummy amesema kuwa, kwa mwaka wa fedha 2023/ 24 tayari serikali imetenga fedha,  hivyo hakuna sababu ya Hospitali hiyo kukamilika na kuanza kutoa huduma kama ilivyokusudiwa , ikiwemo wananchi kupatiwa matibabu kwa mujibu wa rufaa wanazopatiwa kutoka katika hospitali za chini.

“Hatuwezi kuboresha huduma za afya ikiwa miundombinu ya majengo haijakamilika… ndio maana kuna baadhi ya vifaa tiba na mitambo haijaweza kufungwa kutokana na miundombinu  kutokamilika,”amesisitiza Waziri Ummy.

Mkurugenzi mtendaji (Moi) wa Hospitali hiyo ya rufaa ya Mkoa wa Songwe,  Dkt. Lukombodzo Lulandala amesema majengo matatu yaliyoagizwa ujenzi wake  kukamilika  kuwa ni jengo la Mama na Mwana ambalo linahitaji kiasi cha shilingi bilioni 4 ili kukamika na litagharimu kiasi cha shilingi bilioni 9.7.

Ameyataja majengo mengine ambayo yanatakiwa kukamilika kwa agizo la Waziri Ummy kuwa  ni jengo la dharura na mahututi ambalo gharama yake ni shilingi bilioni 3.1.

Dkt.Lulandala amesema jengo kingine ni  la wagonjwa wa nje ( OPD) ambapo linahitaji kukamilisha mfumo wa gesi tiba, pamoja na lifti na kwamba kukamilika kwake kutagharimu kiasi cha shilingi bilioni 7.4.

Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Songwe ambayo tayari imeanza kutoa huduma mbalimbali inajengwa na serikali kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 20.