Serikali yatoa zaidi ya Bilioni 3.1 kupeleka umeme maeneo ya milimani
Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Wananchi wa vitongoji vya milimani katika wilaya ya Ludewa mkoani Njombe wanatarajia kuanza kunufaika na huduma ya umeme kufuatia utekelezaji wa mradi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaolenga kupeleka nishati hiyo katika maeneo ambayo awali hayakuwa na huduma hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Msimamizi wa Miradi wa REA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Danstan Kalugira amesema Serikali tayari imetoa zaidi ya shilingi bilioni 3.1 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji sita vya wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa Kalugira, utekelezaji wa mradi huo unafanywa na kampuni ya SUMA JKT, ambapo mara baada ya kukamilika kwake unatarajiwa kuwaunganisha wateja wa awali takribani 160.

“Mradi huu ni muhimu kwa sababu unalenga kufikisha huduma ya umeme katika maeneo ya milimani ambayo hapo awali yalikuwa hayajafikiwa. Hata kama kipindi hiki ni cha mvua nyingi, mkandarasi anaendelea na kazi kwa kasi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati,” amesema Kalugira.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya umeme vijijini ambayo imeanza kuleta mabadiliko katika maisha ya wananchi.

“Tumejionea kwa macho namna miradi hii inavyotekelezwa na jinsi itakavyowasaidia wananchi wa Ludewa kupata nishati ya uhakika kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na maendeleo,” amesema Balile.
Ziara ya TEF imelenga kutembelea miradi ya kimkakati inayotekelezwa na REA katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo miradi ya Awamu ya Pili B (HEP 2B) inayolenga kupeleka umeme katika vitongoji 9,009 nchini.



More Stories
BREAKING NEWS:Daraja la Mikumi lakatika,mawasiliano Mikumi,Ifakara yakwama
Kamati ya Kudumu ya Bunge Nishati ya Madini yaridhishwa na maendeleo ya kiwanda cha Nguzo za Zege
Wanawake vinara wapewa tuzo na Plan International kama sehemu ya kutambua michango yao