Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (Mb) amesema Serikali imeweka ulinzi katika malango ya kutokea ya viwanja vya ndege, bandari, barabara na mipaka ya nchi ili kuhakikisha hakuna wanyamapori hai/nyara zinazosafirishwa nje ya nchi bila kibali/leseni.
Ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Angelina Adam Malembeka ambaye alitaka kujua aina ya wanyamapori wanaoruhusiwa kufugwa na utaratibu unaotumika kuwapata na mikakati ya Serikali ya kuhakikisha wanyama hao hawasafirishwi nje ya nchi.
Ameongeza kuwa mwaka 2016 Serikali ilitoa tamko katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu zuio la biashara ya usafirishaji wa wanyamapori hai nje ya nchi na kwamba leseni zote zinazohusu usafirishaji wa wanyamapori hai nje ya nchi zilizuiliwa.
Akifafanua kuhusu upatikanaji wa wanyamapori kwa ajili ya kufugwa katika ranchi, mashamba na bustani za wanyamapori, Mhe. Masanja amesema mwananchi anayehitaji kufuga atapaswa kuwa na leseni inayotolewa na Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kufuata vigezo vilivyowekwa kwenye Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka, 2009 na Kanuni za Usimamizi wa Maeneo ya Ufugaji Wanyamapori za Mwaka, 2020.
Aidha, amesema Wanyamapori aina zote wanaruhusiwa kufugwa kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa katika jedwali la sita (6) la Kanuni za Usimamizi wa Maeneo ya Ufugaji Wanyamapori za mwaka 2020 akitolea mfano aina ya mnyamapori, ukubwa wa eneo, na upatikanaji wa chakula na bei zake.
Katika hatua nyingine, Mary Masanja amejibu swali la Mbunge wa Singida Kaskazini, Mhe. Abeid Ighondo Ramadhani kuhusu hatua za Serikali za kupandisha hadhi Msitu wa Mgori kuwa Hifadhi ya Taifa.
Amesema kuwa rasimu ya kwanza ya Tangazo la Serikali imetolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali tarehe 4/2/2022 ambalo litatoa idhini kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kusimamia msitu huo.
Ametaja faida za msitu huo kwa wananchi kuwa ni pamoja na kusaidia kuweka hali ya hewa nzuri kwa mkoa wa Singida, kuwezesha upatikanaji wa mvua hivyo kusaidia kwenye ukuaji wa sekta nyingine kama kilimo, ufugaji na maji na kutunza mazingira na vyanzo vya maji.
Faida nyingine ni amesema ni kuwepo wa baioanuai nyingi za mimea ya asili na makazi ya wanyamapori kama Tembo na wengine hivyo kuchochea shughuli za utalii; na kuwepo kwa fursa za ufugaji nyuki kwa wenyeji ili kuwaongezea kipato.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango