Ulenge: Samia anafanya kazi kubwa kuboresha huduma za jamii
Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa katika kuboresha huduma za jamii na yeye kama mdau wa maendeleo ni lazima achangie jitihada hizo.
Ameyasema hayo Julai 24, 2024 alipofika Shule ya Sekondari Mfundia iliyopo Kata ya Kerenge, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, ambapo pamoja na mambo mengine, alikagua ujenzi wa bweni katika shule hiyo ambapo bweni hilo tangu limeanza kujengwa mwaka 2015 halijakamilika
Mhandisi Ulenge alifika Shule ya Sekondari Mfundia mwaka 2022 na kutoa sh. 600,000 kwa ajili ya kuweka milango miwili ya chuma bweni la wanafunzi na kisha kufanya harambee ambapo katika harambee hiyo, wanawake wa UWT walichangia sh. 200,000 zilizoweka madirisha mawili kwenye bweni hilo, lakini tangu wakati huo hakuna kingine kimefanyika kwenye bweni hilo, kwani ujenzi umesimama.
Ujenzi wa bweni hilo ulianza mwaka 2015, lakini umeishia kwenye kupaua na kuwekewa milango miwili na madirisha mawili. Na ili kukamilika kunahitajika sh. milioni 50. Ulenge ametoa mifuko 20 ya saruji ili kuweka sakafu.
“Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa katika kuhakikisha anaboresha huduma za jamii kwenye Taifa letu. Lakini anafanya jitihada kubwa za kuinua uchumi wa Taifa letu kwa mtu mmoja mmoja, na Taifa kwa ujumla hivyo, mimi kama Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nawiwa kuchangia maendeleo hayo.
“Mwaka 2022 nilikuja hapa nikachangia ujenzi wa bweni na nikatoa fedha (sh. 600,000) kwa ajili ya milango miwili kwenye bweni hilo. Lakini pia nikafanya harambee, na wanawake wa UWT wakachangia fedha (sh. 200,000). Na kwenye mkutano huu wanafunzi wamenieleza na kuweza kunitoa machozi, kuwa bado bweni hilo halijakamilika, na hata mimi nimelikagua, ni kweli halijakamilika. Sasa natoa saruji mifuko 20 ili liwekwe sakafu” amesema Mhandisi Ulenge.
Mhandisi Ulenge ambaye pia ni Mbunge wa Bunge la Dunia (IPU),amesema yupo tayari kuwa mlezi, lakini kwa sharti moja, wanafunzi waweze kufanya vizuri kwenye masomo yao kwani, matokeo aliyooneshwa ya kuanzia mwaka 2022 na 2023 sio mazuri, hivyo akata ushirikiano wa wazazi, walimu na wanafunzi kuweka nguvu za pamoja kuona wanafuta sifuri na daraja la nne (division four).
“Nipo tayari kuwa mlezi wenu lakini kwa sharti wanafunzi waweze kufanya vizuri sababu matokeo ni mabaya ili kufikia hatua hiyo ni lazima kuwe na ushirikiano kati ya wazazi, walimu na wanafunzi. Na nataka kwa kuanzia tufute division zero, na division four. Nia yangu ni kuona wahandisi, madaktari na watu wenye taaluma mbalimbali wanatoka Mkoa wa Tanga,”amesema Mhandisi Ulenge.
Diwani wa Kata ya Kerenge Abdallah Robo alimueleza Mhandisi Ulenge kuwa bweni hilo ambalo ujenzi wake umeanza mwaka 2015 na likiwa limepauliwa na kubaki usafi (finishing) ikiwemo sakafu, milango, madirisha na samani, kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 imepangiwa kiasi fulani cha fedha, lakini ili kukamilisha kabisa bweni hilo kunahitajika sh. milioni 50.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Ulenge ametoa sh. 600,000 kwa ajili ya kununua saruji tani mbili kuendeleza ujenzi wa Msikiti wa Kijiji cha Mavuno, Kata ya Shume wilayani Lushoto. Hiyo ilikuwa ni ahadi yake aliyotoa akiwa kwenye moja ya ziara zake mkoani Tanga.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja