January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ukuaji Teknolojia ,Mgonjwa yasiyoambukiza,hii ni lishe inayofaa

Na Aveline Kitomary,TimesMajira Online,Dar es Salaam.

Magonjwa yasiyoambukiza ni aina ya magonjwa yasiyo na vimelea vinavyoweza kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.

Miongoni mwa magonjwa hayo ni saratani, kisukari, magonjwa ya moyo, mishipa ya damu, selimundu, magonjwa ya akili, magonjwa sugu ya njia ya hewa, magonjwa ya figo, dawa za kulevya, ajali na magonjwa ya meno na macho.

Magonjwa haya anaendelea kuongezeka siku hadi siku kadiri miaka inavyosonga mbele Hata hivyo wataalamu wameainisha sababu mbalimbali ya kuongezeka kwa ugonjwa huo ikiwemo mtindo mbaya wa maisha na kutokufanya mazoezi.

Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto zinaeleza kuwa magonjwa yasiyoambukiza(Non-Communicable Diseases) yanaendelea kuongezeka nchini ambapo jumla ya vifo 134,600 viliripotiwa sawa na asilimia 33 mwaka 2017.

Kwa mujibu wa shirika la Afya Duniani (WHO) Kati ya vifo milioni  56.9 vilivyotokea duniani kote 2016, vifo  milioni 40.5 sawa na asilimia  71 vilitokana na magonjwa sugu yasiyoambukiza (NCDs).

Magonjwa makuu  4 yanayoongoza ni magonjwa ya moyo na mishipa, saratani, ugonjwa wa sukari na magonjwa sugu ya mapafu.

Tafiti zinaonyesha kuwa kunaongezeko la uzito wa magonjwa yasiyoambukiza  haswa miongoni mwa nchi zinazoendelea hii ni kwa mujibu wa ripoti ya WHO ya mwaka 2016.

Mnamo 2016, zaidi ya robo tatu ya vifo  vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukiza  milioni 31.5  vilitokea katika nchi  zinazoendelea.

Uvutaji wa tumbaku unaua zaidi ya watu milioni 8 duniani kila mwaka.

Tafiti zilizofanywa  na WHO mwaka 2020 iligundua kuwa wavutaji sigara wana uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa hayo na pia ugonjwa wa COVID-19, ikilinganishwa na wasiovuta sigara.

Magonjwa ya moyo na mishipa  yamekuwa yakiongoza kwa kusababisha vifo vingi zaidi Duniani ambapo hugharimu maisha ya watu milioni 17.9 sawa na asilimia 44.

Ugonjwa wa Saratani husababisha vifo vya watu milioni 9 sawa na asilimia 22 ,Magonjwa ya njia ya hewa hugharimu maisha ya watu milioni 3.8 sawa na asilimia tisa na Ugonjwa wa kisukari watu milioni 1.6.

Tafiti zinaonyesha  kuwepo ongezeko la magonjwa sugu yasiyoambukiza.

Shirika la afya duniani (WHO) mwaka 2011 lilikisia kuwa asilimia 27 ya vifo hapa nchini vilitokana na magonjwa sugu yasiyoambukiza.

watu wakifanya mazoezi ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza

UKUAJI TEKNOLOJIA YACHANGIA

Miongoni mwa sababu kubwa zinazotajwa katika kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza  ni ukuaji wa teknolojia ambao umebadilisha mtindo wa maisha ya watu waliowengi Duniani.

Wataalamu wa afya wanabainisha aina za kazi,kutokufanya mazoezi na ulaji mbaya unachangia hali hiyo.

Kwa miaka ya nyuma watu wamekuwa wakifanya kazi za nguvu na kula vyakula ambavyo vinaweza kutumika ipasavyo mwilini huku vyakula hivyo vikiwa vya asili zaidi.

Lakini kwa sasa watu hasa waliko mjini hawatumii nguvu kufanya kazi badala yake hukaa ofisini muda mrefu na kula vyakula vya kukaanga zaidi au vya kusindikwa.

“Utakuta mtu anaenda ofisini akiwa na gari lake ,akishuka anapanda lifti kama ni ghorofani na ofisini anakaa kiti za kuzunguka kwa muda mrefu anaaletewa chakula au anashuka na lifti kufata.

“Kuna mwingine asubuhi kifungua kinywa ni soda,mchana soda,jioni juisi yenye kemikali hanyiwa mji aina hii ya maisha si nzuri,”anaeleza Prof Mohammed Janabi ,Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI).

 Gharama zaidi ni pale uelewa unavyokuwa m mdogo kwa jamii kuhusu aina ya lishe inayohitajika na ufanyaji mazoezi.

Utaojia wa taarifa zinazokinzana katika mitando ya kijamii  kuhusu afya huenda ikiwa kikwazo katika kukabiliana na magonjwa hayo.

Wataalamu wa afya wanashauri kuwa na kiasi katika kufanya kila kitu kama vile lishe, kazi na mazoezi, lakini je ni wangapi elimu hiyo inawafikia na kuelewa.

MAMBO YA KUZINGATIA  KWA WAGONJWA     

Adeline Munuo ni Afisa lishe Mtafiti katika Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania anasema yapo mambo muhimu ya kuzingatia hasa pale ambapo tayari mtu ameashapa magonjwa yasiyoambukiza.

“Mmoja wapo ni Kuendelea kutumia dawa kama ilivyoshauriwa na daktari ,Kula chakula mchanganyiko chenye virutubishi mbali mbali ili kuimarisha kinga ya mwili.

“Anatakiwa kufanya mazoezi na kujishughulisha  na Kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu.

UKIWA NA SHINIKIZO LA DAMU FANYA HAYA.

Adfeline anasema mgonjwa wa shinikizo la damu anastahili kupata lishe bora ikiwa ni pamoja na  Kula matunda na mbogamboga kwa wingi katika kila mlo.

”Anashauriwa kupunguza chumvi, tumia viungo kama vile ndimu na tangawizi kuongeza ladha ya chakula,Pima shinikizo la damu mara kwa mara na kutumia dawa kama inavyoshauriwa na daktari.

WAGONJWA WA KISUKARI

Kwa mujibu wa munuo lishe inayotakiwa kwa wagonjwa wa kisukari  ni Kula mlo kamili ukizingatia aina mbalimbali za vyakula.

Anasema Ni mgonjwa wa kisukari kula mbogamboga kwa wingi na kiasi kidogo cha nafaka.

”Atumia nafaka isiyokobolewa kama vile dona, ata n.k kwani vina makapi mlo kwa wingi na apunguze kuongezeka kwa sukari mwilini,”anabainisha Munuo.

Anasema kwa wale wenye kisukari aina ya pili wanatakiwa Kula vyakula vya jamii ya kunde kama (sehemu ya mlo).

”Kwa kwa mfano maharage, njegere, mbaazi, kunde, choroko na mengine,Sukari iliyopo kwenye matunda ni kidogo na kiasi kikubwa cha sukari hiyo ni fructose ambayo haihitaji kichocheo cha insulini katika kumeng’enywa,”anaeleza.

LISHE KWA WAGONJWA WA MOYO

Munuo anasema ni muhimu wagonjwa kufuata taratibu za matibabu kama walivyoshauriwa na mtaalam wa afya

”Aina ya lishe wanayotakiwa ni kula chakula mchanganyiko kama vile mbogamboga, matunda na vyakula vya jamii ya kunde na nafaka  zisizokobolewa kama mfano dona.

“Punguza matumizi ya mafuta na epuka mafuta yatokanayo na wanyama, pamoja na nyama yenye mafuta; maziwa yenye mafuta mengi jibini na mengine.

“Punguza ulaji wa nyama hususan nyama nyekundu iliyosindikwa mfano soseji na nyama za makopo ,Punguza vyakula vyenye lehemu kwa wingi kwa mfano mayai, maini, moyo, figo, mafuta yenye asili ya wanyama na nyama nyekundu.

Anaeleza kuwa wagonjwa hao wanapaswa kuepuka vyakula na vinywaji vinavyosababisha ongezeko la uzito, ikiwa ni pamoja vyakula vyenye sukari nyingi au mafuta mengi, soda na juisi bandia.

”Punguza kiasi cha chumvi unachotumia na epuka vyakula vyenye chumvi nyingi,”anasisitiza.

MTINDO UNAOFAA KWA SARATANI

Munuo anaeleza kuwa wagonjwa wa saratani wanapaswa kufuata maelekezo ya daktari na wataalamu wa afya, pamoja na utumiaji wa dawa na kumuona daktari kwa tarehe zilizopangwa.

“Kwa wale wagonjwa wanaopata tiba za mionzi kinga ya mwili huathirika zaidi hivyo msisitizo kuhusu ulaji wa vyakula vinavyoboresha kinga ya mwili zaidi ni muhimu kama vile mbogamboga, matunda, vyakula vya asili ya wanyama.

“kula mbogamboga na matunda mabali mbali kila siku,  tumia pia mbogamboga zisizopikwa, kama vile saladi, nyanya, matango na mengine .

“Tumia nafaka zisizokobolewa kama vile unga wa mahindi wa dona, unga wa ngano usiokobolewa, pia ulezi, mtama au uwele kwani vina makapi-mlo kwa wingi, vyakula mbalimbali vya jamii ya kunde kama vile maharagwe, kunde, njugu mawe, dengu, choroko na mbaazi,”anabainisha.

Anasema ni muhimu kufanya  mazoezi kulingana na afya ya muhusika.

“Utumiaji wa nyama nyekundu kwa wingi umeonekana kuongeza uwezekano wa kupata saratani hasa za utumbo mpana, kinywa, koo, mapafu na kongosho

“Epuka matumizi ya nyama zilizosindikwa kwani huongeza uwezekano wa kupata saratani hasa zile za utumbo mpana, kinywa, koo, mapafu na tezi ya kiume,”anashauri Munuo.