Na Na Reuben Kagaruki,TimesMajira,Online, Dar
WAZAZI na walezi wameshauriwa kulinda watoto wa kike na kuwasimamia katika suala zima la matumizi ya mitandao ili waweze kuepukana madhara ya matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ambayo wakati mwingine husababisha vitendo vya ukatili wa kimtandao.
Ushauri huo umetolewa jijini Dar es Salaam juzi na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis, kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Kimataifa.
Maadhimisho hayo ufanyika kila mwaka Oktoba 11, kwa lengo la kukumbushana upatikanaji wa haki za msingi za mtoto wa kike na kujadili namna bora ya kuweza kutatua chagamoto mbalimbali ambazo wamekuwa wakikumbana nazo watoto hao.
Maadhimisho ya mwaka huu yalibebwa na kauli mbiu isemayo; “Kizazi cha Kidigitali Kizazi Chetu.”
Naibu waziri huyo amesema kumekuwepo na matumizi yasiyosahihi ya mtandao pamoja na vifaa vya kidigitali ambavyo vimekuwa vikichangia unyanyasaji na ukatili kwa vijana na watoto wa kike.
“Kauli mbiu ya mwaka ya mwaka huu inatukumbusha na kuhimiza jamii kuwa dunia inapitia mapinduzi makubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano, ambayo inawezesha na kutoa fursa mbalimbali za maendeleo na ustawi wa kizazi kilichopo ambapo zaidi ya watu nusu yake ni watoto pamoja na vijana,”amesema
Khamis amesema unyanyasaji huo umekuwa ukifanywa kwa kutumia picha zenye maudhui ya kigono, ulaghai au kudanganywa pamoja na ngono vitisho.
” Vijana balehe wamekuwa wakirubuniwa ili kushiriki usafirishwaji haramu ambao mara nyingi uhusishwa na matukio ya kiuhalifu,”amesema Khamis
na kuongeza; “Mbali na kurubuniwa pia ufanyika vitendo vya uonevu wa kimtandao ambapo waathirika wakubwa ni watoto wa kike.”
Amefafanua kwamba tafiti za awali za nchi zinaonesha kuwa takribani watoto watano kati ya 10 wa shule za sekondari za mijini wanamiliki simu, huku nane kati ya 10 utumia simu nyumbani na wengine watano kati 10 wapo katika mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa naibu waziri huyo utafiti huo umeonesha kuwa ukatili wa kimtandao unatokana watoto wenzao, huku wengine wakiwa watu wazima wanaowafahamu na wasiowafahamu.
Kuhusu madhara ya ukatili wa kimtandao kwa watoto, Khamis amesema ni pamoja na kuzorotesha elimu kwa mtoto wa kike, kwani uweza kusababisha kukatisha masomo yake jambo ambalo huathiri mfumo mzima wa maisha yake .
Mbali na hilo pia amesema ukatili wa Mtandao usababisha madhara ya kisaikolojia pamoja na kihisia. “Kwa mujibu utafiti unaonesha kuwa asilimia 32 ya watoto wa kike walifanyiwa uonevu mtandaoni wanakuwa na msongo wa mawazo,” amesema
Amesema Serikali ikumekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kitaifa, kikanda kuwalinda watoto na vijana balehe dhidi ya ukatili wa mitandao
Amefafanua kuwa kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali imetunga Sheria nzuri zinazohusu matumizi ya mtandao, huku sera ya Taifa ya mwaka 2019 ikielekeza wazi kuweka mazingira salama katika matumizi mazima ya tehama na mitandao.
Aidha, ametoa wito kwa wadau wote kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu juu ya masuala mazima ya mitandao.
Akizungumzia hali ya ukatili mtandaoni, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mtoto, Sebastian Kitiku, amesema Serikali tayari imeunda kikosi kazi cha Taifa cha kuzuia ukatili wa watoto katika mtandao.
Amefafanua kwamba kikosi kazi hicho kinajumuisha wataalamu kutoka Serikali na wadau na kinajadili mara kwa mara masuala ya ukatili kwa watoto na kuyashughulikia mara moja.
Ametoa mwito kwa wazazi na walezi kukabiliana na ukatili mtandaoni kwa watoto kwa kuhakikisha wanaweka mipaka ikiwa ni pamoja na kuepuka kuwa waratibu wa mitandao hiyo kwa lengo la kutoharibu malezi na makuzi yao.
Mwakilishi wa watoto ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la watoto, Nancy Kasebo, ameiomba Serikali kuboresha huduma za Kidigitali ili mtoto wa kike aweze kushiriki kikamilifu kujifunza sambamba na kutoa elimu ya madhara ya kimtandao ili kuweza kuepukana na ukatili wa mitandaoni.
“Tunaiomba Serikali itoe adhabu kali kwa watu wanaoshiriki kudhalilisha watoto wa kike kupitia mitandao,”amesema Aloyce na amewaomba wazazi na walezi kutokufumbia macho vitendo vya ukatili na badala yake watoe taarifa kwa mamlaka zinazohusika ili kuwaokoa watoto wa kike.
Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Wanawake (UN-Women), Hodan Addou amesema ni muhimu wadau kwa pamoja kushirikiana kuhakikisha watoto wa kike wanalindwa dhidi vitendo vya ukatili wa mitandaoni na kuhakikisha wanaitumia vizuri kwa mustakabari wa maisha yao ya baadaye
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Bright Jamii, Irene Fugara kwa niaba ya wadau wa maendeleo amesema wanatambua kuwa moja ya changamoto kwa watoto wa kike ni kutokuwa na fursa sawa ya manufaa ya teknolojia.
Ameongeza kuwa wadau wataendeleza jitihada za Serikali za kuwasaidia watoto wa kike kuweza kufikia fursa hizo kwa kuwawezesha kusoma masomo ya sayansi.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapatoÂ