November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanasheria wa Shirika la Wadada Solutions on Gender Based Violence Anitha Samson

‘Ukatili kingono hautakiwi kunyamaziwa unaathiri taifa’

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

KATIKA kukomesha vitendo vya ukatili kwa watoto hususani wa kingono ,wazazi kwa ujumla wametakiwa kutoa taarifa mapema katika vyombo husika ili hatua za kisheria zichukuliwe hali ambayo itasaidia mtoto kupata haki yake na kuwa na taifa lililo salama kwa ustawi wa maendeleo.

Kwani imeonekana ukatili wa kingono kwa watoto umekuwa ukianzia nyumbani huku familia zikishindwa kutoa taaarifa kwenye vyombo husika kwa kuogopa fedhea ambapo unakuta aliyefanya aidha ni baba,mjomba,babu,kaka na wengineo ambao ni ndugu wa karibu.

Mwanasheria wa Shirika la Wadada Solutions on Gender Based Violence Anitha Samson (kushoto) akizungumza na mwandishi wa majira/timesmajira online ofisini kwake Jijini Mwanza ambapo alitoa rai kwa jamii kutoa taarifa mapema ya vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto.

Akizungumza na Majira ofisini kwake Mwanasheria wa Shirika la Kutetea Watoto wa Kike la Wadada ‘Solutions on Gender Based Violence’ Anitha Samson,anasema changamoto ni jamii yenyewe ambayo inachelewa kutoa taarifa ambapo inakuja kutoa baada ya siku nyingi kupita pale watakaposhindwa kuelewana na yule aliyefanya kitendo cha ukatili kwa mtoto aidha wa kubakwa au kulawitiwa.

“Hivyo unakuta ushahidi au uthibitisho unakuwa umeshapotea,hali inayochangia kukwamisha jitihada za Serikali na mashirika katika kutokomeza ukatili wa kingono kwa watoto.

“Tumejikita kufanyakazi katika kata sita za Wilayani Ilemela mkoani hapa tukiwa na lengo la kuimarisha uwezo wa wasichana wadogo wenye umri kati ya miaka 11-25,kutetea haki zao ili waweze kuishi bila ukatili wa kingono na unyonyaji huku dira yetu ni kuona kwenye jamii wasichana wadogo wanaishi na kukua bila ukatili wa kingono na unyonyaji,”anasema Anitha na kiongeza kuwa

Pia anasema,kuripoti mapema vitendo vya ukatili wa kingono hususani kwa watoto itasaidia ujazaji wa PF3 kwa wakati ambao ni ushaidi muhimu katika kesi za namna hiyo ambao utasaidia mtoto kupata haki yake.

“Jamii ielewe kuwa inapaswa kutoa taarifa mapema Polisi ili wapatiwe fomu ya PF3 ambayo wataipeleka hospital kwa ajili ya daktari kuijaza kitaalamu baada ya kumpima mlengwa,pia tunawasisitiza kwamba mtu au mtoto akifanyiwa ukatili wa kingono kwa kubakwa asiogeshwe.

“Asitibiwe makovu au majeraha alioyapata baada ya kufanyia tukio hilo ,asibadilishwe nguo zaidi achukuliwe kama alivyo apelekwe Polisi kisha hospitali na kwa sasa Serikali imerahisisha kwa kuweka kituo cha One Stop Centre katika hospitali ya Mkoa ya Sekou-Toure ambacho unapata huduma zote kwa wakati mmoja,” anasema Anitha.

Mkurugenzi wa Miradi wa Shirika la HakiZetu Tanzania Gervas Evodius akizungumza na majira lilipomtembelea ofisini kwake Wilayani Ilemela ambapo anasema vitendo vya ukatili wa kingono havipaswi kunyamaziwa

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi wa Shirika la HakiZetu Tanzania Gervas Evodius,anasema ukatili wa kijinsia hususani kwa watoto hautakiwi kunyamaziwa kwani aumuathiri mtu mmoja bali bali wa taifa kwa ujumla.

Evodius anasema,vitendo hivyo vimekuwa vikitendeka lakini kwa sababu ya aibu watu wamekuwa wakivinyamazia hivyo kutokufika katika ngazi za sheria.

“Kesi tunazokuwa tunapokea zinazohusiana na vitendo vya ngono kwa mabinti ni nyingi,na mara nyingi kesi za ukatili wa kingono zinakuja pale matokeo yanapotokea mfano binti anapokuwa amepata mimba hasa baba wa mtoto akiacha kutunza mtoto au kuikana mimba ndio anakuja kusema ila tofauti na hapo jamii hairipoti inakua kimya,” anasema Evodius.

Naye Shekhe Rajabu Hassan wa Msikiti wa Kata ya Ngudu Wilayani Kwimba akizungumza na Majira kwa njia ya simu anasema,jamii inapaswa kuzingatia na kufuata taratibu za kidini zilizopo pamoja na za nchi ili kuacha kufanya vitendo vya ukatili ambao hata maandiko ya vitabu vya dini vinakataza matendo hayo.

Meneja wa Kitengo wa Shirika la Plan Internation Tanzania Mkoa wa Mwanza Dkt.Majani Rwambali anasema wametoa elimu na mafunzo ya kuwahamasisha vijana ambao yameleta hamasa kwa vijana kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa ukatili huku mipango na rasimali zao wamezielekeza katika kumlinda na kumwendeleza mtoto na kutekeleza sheria zote za nchi ili kuweza kufikia malengo mbalimbali yaliyowekwa.

Mwanasheria wa Shirika la Wadada Solutions on Gender Based Violence Anitha Samson

“Kwa nini idadi ya matukio yanaongezeka kwa sababu watoto wanaopata mimba ni wengi,baada ya kutoa elimu jamii imepata uelewa na ujasiri wa kutoa taarifa kwenye vyombo ambapo inawezekana huko nyuma kulikuwa na matukio mengi zaidi na watu hawakujua wapi pa kuyasemea lakini sasa wanatambua haki zao,”anasema Dkt.Rwambali.

Hata hivyo mmoja wa wananchi wa mtaa wa Mkudi Wilayani Ilemela Agnes Lucas anasema ukatili wa kingono kwa watoto ambapo kwa kipindi hiki watoto wa kiume wamejikuta wakilawitiwa kutokana na wazazi na jamii kutokuwa na utambuzi wa masuala hayo pamoja na ulinzi.

“Mfano anaweza kutokea mgeni wa kiume kaja kutembelea nyumbani kisha akaambiwa alale na mtoto mmoja wapo ambapo unakuta hawajui tabia yake hivyo kupelekea mtoto kufanyiwa ukatili huo na kushindwa kutoa taarifa mapema kutokana na hofu au kushindwa,” anasema.

Mjumbe wa Baraza la Watoto Mkoa wa Mwanza Mariam Daud anasema njia inayotakiwa kutumika kupunguza ukatili ni Serikali kuhakikisha kuwa inatoa elimu ya masuala ya kujitambua kwa watoto kuanzia elimu ya msingi, vijijini ambao wana athirika zaidi kutokana na kukosa sehemu ya kutoa taarifa dhidi ya ukatili hivvyo wadau kwa kushirikiana na Serikali ipeleke watu maeneo hayo ambao wataenda kuelimisha jamii kuhusiana na masuala ya kikatili.

Hata hivyo Tanzania kama nchi nyingine barani Afrika watoto bado wanakabiliwa na changamoto ya vitendo vya ukatili wa aina mbalimbali ikiwa ni ubakaji,ulawiti,utumikishwaji wa watoto katika ajira hatarishi,ukeketaji,ndoa na mimba za utotoni huku takwimu za Jeshi la Polisi nchini zinaonyesha kuwa vitendo vya ukatili vinaendelea kuongezeka kutoka matukio 14,491 mwaka 2018 hadi matukio 15,680 mwaka 2019.