December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ujio wa DP World,kete bandari Dar

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imepongezwa kwa kuzingatia maoni ya wananchi kwenye mkataba wa uendelezaji bandari ya Dar es Salaam baina yake na Kampuni ya DP World ya Dubai, hatua ambayo itasaidia kuongeza ufanisi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana ikiwa ni siku moja baada ya kusainiwa kwa mikataba mmitatu muhimu ya uendelezaji bandari, baina ya pande hizo mbili, baadhi ya wananchi walipongeza Serikali kwa usivu.

Juzi, Rais Samia Suluhu Hassan, akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo, alisema;

“Tunafarijika kuwa DP world wameridhia mahitaji na matakwa yetu kama tulivyobainisha na matamanio ya wananchi wetu na maslahi mapana ya nchi yetu.”

Akizungumza na gazeti hili jana, mtaalam wa masuala ya bandari, Jacob Edward, amesema ingekuwa pigo kwa Watanzania, kama Serikali isingefikia muafaka na Serikali, kwani ufanisi wa bandari yetu upo
Alisema uzoefu ambao kampuni hiyo ya DP World ya Dubai inao kwenye shughuli za bandari utawezesha bandari ya Dar es Salaam kuhimili ushindani dhidi ya bandari nyingine.

Mmoja wa wananchi aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la jina lake kutochapishwa gazetini, alisema Watanzania wana kila sababu ya kujivunia uzoefu wa DP World kwenye shughuli za bandari,

Ametolea mfano uwekezaji DP World katika Bandari ya Dakar, nchini Senegal, ambapo ndiyo bandari pekee Magharibi mwa Afrika inayotoa huduma ya window berthing system ambayo imeondoa utaratibu wa meli kusubiri nje ya bandari na kupunguza muda wa magari kugeuza ndani ya bandari kuwa chini ya dakika 20.

Amesema DP World ina uwezo na uzoefu mkubwa katika kuendesha shughuli za bandari katika maeneo mbalimbali duniani, ambapo imewekeza mtaji na teknolojia katika uendeshaji wa shughuli za kibandari katika maeneo mbalimbali ya Bara
la Afrika na Nje ya Bara la Afrika.

Mtoa habari mwingine aliyezungumza kwa sharti la jina lake kutochapishwa gazetini amesema; “Watanzania hawana sababu ya kuwa na wasiwasi kwamba watapoteza ajira, kwani katika nchi ilikowekeza Kampuni hiyo pia, hutumia wafanyakazi wa ndani ya nchi husika katika uendeshaji wa shughuli za Bandari kwa kuwajengea
uwezo unaotakiwa ili kuendana na mahitaji ya kisasa ya uendeshaji wa bandari.

“Ndiyo maana Rais Samia (Suluhu Hassan) mara baada ya kusainiwa mkataba, alisema hakuna mfanyakazi atakayepoteza kazi, awe mwajiriwa wa bandari au wale wanaofanyakazi zao bandarini, wakiwemo wafanyabiashara,” amesema.

Mtoa habari wetu ambaye ni mtaalam wa masuala ya bandari anatoa mfano kuwa kwenye Bandari za nchi za Misri na Uingereza, ambazo DP World imewekeza na zaidi ya asilimia 90 ya wafanyakazi ni wazawa.

Mwananchi mwingine, Shaban Abdalla Ally, amempongeza Serikali kwa kuweka mkataba hadharani ambao umeonesha wazi kwamba una maslahi mapana kwa nchi.

Amesema shida haikuwa DP World, shida ilikuwa kwenye mkataba, lakini uwezo wa kampuni hiyo unajulikana vizuri kote duniani.

“Katika maeneo yote ambayo DP World imewekeza kumekuwa na ongezeko la shehena na ufanisi katika utendaji kazi ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya uwekezaji.

Mathalan, katika nchi ya Senegal uwekezaji uliofanywa na DP World katika Bandari ya Dakar, viwango vya utendaji kazi ikiwemo muda wa meli kusubiri nje ya bandari umetoka saa 35 hadi saa 1,” amesema.

Amesema mamlaka za Bandari za nchi mbalimbali duniani
kuanzia miaka ya 1990 zimefanya mabadiliko makubwa katika usimamizi wa shughuli za bandari kwa kubakiza jukumu la kuwa mmiliki wa bandari (landlord) huku Sekta Binafsi wakipewa jukumu la kuendeleza na kuendesha shughuli za bandari.

Amesema mabadiliko hayo yamewezesha kubadilisha mwelekeo wa huduma za bandari hizo kwa kuziongezea uwezo, matumizi ya kisasa ya mifumo ya TEHAMA na kuzifanya kuwa na ufanisi wa viwango vya
kimataifa.

Amesema huduma za bandari zimekuwa zikitolewa katika mwelekeo wa kuwezesha sekta nyingine za uchumi na kukusanya mapato ya
Serikali wakati bandari ikitoa huduma ambayo inalenga kuwezesha sekta hizo kutimiza azma ya maendeleo.

Ally amesema hiyo ni kwa sababu DP World imekuwa ikitumia pia mikakati Madhubuti ya kimasoko (aggressive marketing techniques) inayohusisha mawasiliano ya moja kwa moja na wamiliki wa mizigo hivyo mikakati yao ya kimasoko haina utegemezi wa Mawakala wa Meli;

Akizungumza katika utiaji saini huo, Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Kampuni Tanzu za DP World, Sultan Ahmed Bin Sulayem, amesema:

“Ni heshima kubwa kwetu kushirikiana na Serikali ya Tanzania
kuiboresha Bandari ya Dar es Salaam. Hatua hii inaendana na mipango ya kimkakati ya maendeleo inayopangwa na Tanzania na ni uthibitisho wa uongozi mahiri wenye maono wa Rais
Samia Suluhu Hassan.

“Jambo hili litatoa fursa nyingi kwa eneo hili la Afrika kwa kuliunganisha na masoko ya dunia, kutengeneza ajira nyingi zaidi, kuongeza upatikanaji wa huduma na bidhaa, na kuongeza tija kwa wadau wote.

Mkataba huu ni mwendelezo wa dhamira ya DP World kuunganisha
watu na biashara kwa lengo la kukuza uchumi wa dunia. Pamoja na bandari nyingine tunazofanya nazo kazi, uwekezaji huu ni hatua nyingine kwenye jitihada zetu pana za kushirikisha wataalamu wetu wa kimataifa na wazawa wa nchi husika kukuza mnyororo wa usafirishaji ili kukuza uchumi wa bara zima
la Afrika”.