January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ujenzi wa mabomba ardhini kuanza kufanyika rasmi

Na Angela Mazula,TimesMajira Online.

KAZI za ujenzi wa miundombinu kwenye mikuza (mabomba yanayopita ardhini), sasa kuanza rasmi kufanyika hapa nchini ili kulinda usalama wa wananchi na kulinda miundombonu iliyojengwa chini ya ardhi.

Hayo yamesemwa Dar es Salaam leo na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Zena Said wakati wa makubaliano kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Mawasiliano (TTCL), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) pamoja na wasambazaji wote wa gesi hapa nchini.

Amesema majukumu ya wizara ni kutunga sera na kutoa miongozo inayofaa katika kusimamia rasilimali ya gesi asilia, kutokana na kutathmini utendaji wa tasnia ya gesi hiyo hususan katika uhifadhi, usafirishaji na usambazaji.

Katibu Mkuu huyo amesema, matarajio makubwa ya serikali ni kuongeza usimamizi madhubuti wa pamoja katika miundombinu yote iliyopo chini ya ardhi kwenye mikuza, ili kuzuia uharibifu wa miundombinu iliyopo chini ya ardhi.

Naye Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Uthibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Injinia Godfrey Chibulunje amesema ongezeko la gesi asilia katika shughuli za utunzaji wa mabomba kwenye mikuza inayotumiwa na watoa huduma mbalimbali, zikiwemo bomba za usambazaji wa gesi asili.

‘’Shughuliza za uchimbaji na kutandaza mabomba kwenye mikuza, haziepukiki kwani mahitaji ya huduma zinazotolewa na makampuni mbalimbali yanazidi kuongezeka kila siku,” amesema Injia Chibulunje.

Hata hivyo amesema kushirikiana na kuitunza mikuza ili kutoa huduma mbalimbali ni jambo lisilokwepeka, kwani linaboresha matumizi bora ya ardhi na uhifadhi wa mikundombinu.