December 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ujenzi uzio shuleni kuimarisha ulinzi na usalama wa mtoto


Na Joyce Kasiki,Dodoma


HALMASHAURI ya jiji la Dodoma imeanza ujenzi wa uzio wa shule ya Msingi Mlezi iliyopo
katika Jiji la Dodoma ili kuwalinda watoto hasa wale wenye mahitaji Maalum pamoja na
watoto wadogo wenye umri wa miaka minane kushuka chini na wanafunzi wote kwa ujumla.


Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Profesa Davis Mwamfupe anasema,ujenzi wa uzio katika
shule hiyo ambayo inapitiwa na barabara kubwa inayotoka mjini kwenda Hospitali ya Taifa
ya Afya ya Akili (Mirembe) na shule nyingine zinazopitiwa na barabara ni kipaumbele .


“Kama unakumbuka uliwahi kunihoji kuhusu ujenzi wa uzio wa shule hiyo ya Mlezi na
nikakwambia zipo shule nyingi zenye cgangamoto hiyo ikiwemo shule ya msingi Uhuru
nambayo nayo inapitiwa na barabara ambayo yanapita magari makubwa,


“Hapa ninavyokwambia shule ya msingi Uhuru tumeshajenga uzio kwa sehemu kubwa na
ujenzi unaendelea na shule ya msingi Mlezi tumeshaanza ujenzi .”anasema Prof.Mwamfupe
 
Profesa Mwamfupe anasema uboreshaji wa miundombinu ya shule ikiwemo ujenzi wa uzio
hasa katika shule zilizopo barabarani,ni kiupaumbele cha Halamshauri ya Jiji la Dodoma.
Anasema hatua hiyo inaenda kusaidia katika kudhibiti utoro na mwingiliano usio na afya
baina ya wanafunzi na jamii.


“Ujenzi unaweza kuchukua muda mrefu kutokana na shughuli nyingi za miradi ya maendeleo
zinazofanywa na mapato yetu ya ndani ikiwemo kujenga shule nyingine,hata hivyo
hatutaacha kujenga uzio kwa sababu tunapenda shule zetu ziwe na uhakika wa mipaka na
usalama wa watoto.”anasisitiza Mstahiki Meya huyo


Baadhi ya wazazi wameushukuru uongozi wa jiji la Dodoma kwa kuanza ujenzi katika shule
hizo ambao kwa namna moja ama nyingine unaenda kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto.
Aziza Bakari Mkazi wa Mtaa wa Mlezi Kata ya Hazina ,ameiomba serikali kupitia Jiji la
Dodoma kuongeza kasi ya ujenzi huo ili uweze kukamilika kwa haraka.


Christina Joseph Mkazi wa Mtaa wa Hazina Kata ya Hazina anasema kumalizika kwa ujenzi
wa uzio huo kunakwenda kuimarisha usalama wa watoto shuleni hapo lakini pia utoro nao
unakwenda kupungua kwa namna moja ama nyingine.


“Unajua shule hii ipo barabarani kabisa,na ni barabara kubwa ambayo inatoka mjini hadi
barabara ya Mirembe na kukutana na barabara kubwa ya Iringa,kwa hiyo uzio
utawahakikishia watoto usalama kwa kiasi kikubwa,maana watoto wakiingia shuleni
hawatatoka tena bali kwa ruhusa maalum na hgivyo hata kuzuia ama kupunguza athari za
ajali zinazoweza kuwapata.”anasema Christina

Baadhi ya wazazi na jamii kwa ujumla waishio jirani na shule hiyo wamekuwa wakiiomba
serikali kusaidia ujenzi wa uzio katika shule hiyo kwa ajili ya usalama wa watoto wakiwemo
wenye mahitaji maalum wanaosoma katika shule hiyo lakini pia na watoto wote kwa ujumla.

Ulinzi na usalama wa mtoto hasa wa umri wa miaka minane kushuka chini ni moja ya afua
muhimu katika kihunzi cha Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) ili athiriwe na
kitu chochote kwa lengo la kufikia ukuaji timilifu .