December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ujenzi daraja la Msangano watakiwa kuharakishwa

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,
Momba.

KATIBU Tawala (RAS) wa Mkoa wa Songwe, Happness Seneda, amemtaka Mkandarasi wa Lukolo Company Limited anaetekeleza mradi wa ujenzi wa daraja Msangano katika barabara ya Chindi – Msangano litakalo gharimu sh. Bilioni 3, kuhakikisha ujenzi huo unakwenda kwa kasi na kumalizika kwa muda uliopangwa kwa mujibu wa mkataba.

Seneda ametoa maelekezo hayo,leo Novemba 8, 2023 baada ya kutembelea na kukagua Barabara ya Chindi- Msangano ambayo inaunganisha Halmashauri tatu za Momba, Tunduma Mji na Mbozi, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku tatu katika Halmashauri ya Momba kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo baada ya serikali kupeleka fedha katika Halmashauri hiyo.

“Mkandarasi hakikisha unazingatia muda Kwani daraja hili lina umuhimu mkubwa katika kukuza uchumi wa Halmashauri zetu kama unavyojua Momba ndio wazalishaji wakubwa wa mazao ya kilimo na Tunduma ndio kitovu cha biashara hivyo ni lazima kuwarahisishia mawasiliano” .

Seneda amesema Serikali imeamua kutoa sh. Bilioni 3 ikiwa ni fedha toka tozo ya mafuta ( Fuel Levy) kwa lengo la kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao ya kilimo kwa kipindi chote cha mwaka ambapo wananchi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Momba wataweza kufikisha mazao ya katika Halmashauri ya Mji Tunduma ambako ni kitovu cha biashara.

Aliyataja manufaa mengine ya mradi wa ujenzi wa daraja hilo baada ya kukamilika kuwa ni kufungua mawasiliano kati ya Makao Makuu ya Wilaya ya Momba na Mji wa Tunduma, pamoja na Wilaya ya Mbozi, ikiwemo ongezeko wa vyombo vya usafirishaji hivyo kupunguza adha usafiri iliyopo kwa sasa.

Meneja wa Wakala wa barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Momba, Mhandisi Yusuph Shaban, akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Katibu Tawala wa Mkoa, alisema Halmashauri ya Wilaya ya Momba kupitia Tarura iliidhinisha bajeti ya kiasi cha sh. Bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Msangano katika barabara ya Chindi- Msangano.

Aidha, Mhandisi Shabani alisema baada ya kukamilika kwa hatua za usanifu wa daraja hilo, ikiwemo vipande vya barabara vinavyounganisha daraja gharama halisi ilifikia sh. Bilioni 3 na kuomba ongezeko la sh. Bilioni moja.

Mhandisi Shabani alisema utekelezaji wa mradi ni wa miezi 24 na ulianza Septemba Mosi 2023 na unatarajia kukamilika Septemba 1, 2025 na tayari Mkandarasi amelipwa malipo ya awali ya sh. Milioni 4.97 ambazo ni asilimia 15.