November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ujenzi Bandari ya Uvuvi Kilwa kukamilika Februari 2025

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko ambao mpaka sasa umefikia asilimia 63 na unatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2025.

Waziri Ulega amesema hayo leo alipotembelea kukagua maendelea ya ujenzi wa mradi huo unaofanyika wilayani Kilwa, mkoani Lindi leo Julai 30, 2024.

Amesema bandari hiyo ya uvuvi inayojengwa kwa fedha za ndani ni mradi wa kielelezo unaotekelezwa chini ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Mradi huu tuutazame kama mboni ya jicho letu ili uwe endelevu kwa maana ukikamilika utainua uchumi wa Kilwa, ukanda wa Kusini na Taifa kwa ujumla”, amesema

“Nimefurahi hatua ni nzuri, tumepiga hatua zaidi ya nusu, muhimu kuhakikisha kazi inakwisha kwa wakati ili Watanzania waweze kuona thamani ya pesa zao, shukrani nyingi kwa rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kuujenga mradi huu ambao ni wa kielelezo kwa taifa letu”, alifafanua