December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uingizaji Nguruwe Mbarali wapigwa marufuku baada ya kuibuka mlipuko wa ugonjwa

Na Esther Macha, Timesmajira, Online, Mbarali

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imepiga marufuku usafirishaji wa nguruwe kutoka eneo moja hadi lingine kutokana na kuibuka mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nguruwe kutoka Mji makambako mkoani Njombe na Mafinga Mji katika mkoa wa Iringa
,pamoja na Jiji la Mbeya .

Akizungumza leo wakati wa akitoa taarifa za ugonjwa huo kwenye kikao cha baraza la madiwani cha kawaida ,Mkuu wa Idara ya kilimo na mifugo na uvuvi ,Dkt.Anania Sangwa amesema kuwa katika
maeneo ambayo yanazungukwa na wilaya ya mbarali kumetokea mlipuko wa
ugonjwa wa homa ya Nguruwe .

‘’Tumepata taarifa kuwa majirani zetu Mji Makambako , Mafinga, pamoja na Jiji la Mbeya kuna mlipuko wa ugonjwa wa homa ya Nguruwe na ukiangalia kwa Jiografia tuliyopo ni rahisi sana kupata ugonjwa huu
kwa namna unavyosambaa kwa kasi wito wangu kwenu tusaidiane kupeleka taarifa hii kwenye maeneo yetu kwasasa haturuhusu tena usafirishaji wa Nguruwe kutoka eneo moja hadi linguine , wanyama wote watakaguliwa wakiwa hai kwanza na baada ya kuchinja tena watakaguliwa kwa umakini
mkubwa ,tunashauri wafugaji wetu wasipeleke mifugo kupandisha kwenye sehemu zingine ni vema kujitegemea ‘’amesema Dkt. Sangwa.

Akielezea zaidi Dkt. Sangwa amesema pia waepuke kubeba makombo kupeleka nyumbani mara baada ya kula nyama hiyo kwa lengo la kulisha nguruwe kwani unaweza ukawa umebeba virusi vya homa ya nguruwe na kusambaza zaidi hivyo waepuke hilo , pia amewataka wamiliki wa wa
Nguruwe wahakikishe wanafanya usafi kwenye mabanda kwa kutumia dawa ili wote wapate elimu namna ya kujikinga na ugonjwa huo.

Aidha amesema kuwa kupitia kamati ya usalama wilaya tayari imeanza kulifanyia kazi kwa kuhakikisha kuwa vituo vyote vya mipakani kuwa kila Nguruwe anayepitishwa mipakani , barabarani wanafanyiwa ukaguzi na kama wafugaji wanasafirisha nguruwe wahakikishe wanakuwa na vibali kutoka kanda kwa ofisa mfawidhi mkoa wa Iringa ambao wanachukua sampuli za nguruwe.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali Twalib Lubandamo amesema kuwa mlipuko wa ugonjwa huu si mzuri hivyo ni vema wananchi kuchukua tahadhari.

‘’tusiache nguruwe hawa wakisambaa ovyo kuwe na sehem u ya kufugia ili kuepuka kusambaa kwa ugonjwa huu ambao tayari upo kwa majirani zetu Mji makambako,Mafinga na Jiji la Mbeya’’amesema Mwenyekiti huyo.

Katibu Tawala wilaya ya Mbarali amesema ,Michael Semindu amesema kuwa hatua zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya ugonjwa huo katika maeneo mbali mbali ya Wilaya hiyo pamoja na kusimamia
uingizaji kiholela wa nguruwe ikiwa ni pamoja na kusimamia kwenye maeneo ya mipaka.

Mkuu wa Idara ya Kilimo mifugo na uvuvi2, Dkt,Anania Sangwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali,Twalib Lubandamo.
Baadhi ya madiwani wakisikiliza taarifa ya idara ya Kilimo mifugo na uvuvi