November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uhamiaji yakemea wanaoajiri wahamiaji haramu

Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online. Shinyanga

IDARA ya Uhamiaji mkoani Shinyanga, imekemea tabia ya baadhi ya watu wanaowaajiri kinyume cha sheria wahamiaji haramu, kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo uchungaji wa mifugo na kwamba yeyote
atakayekamatwa sheria itachukua mkondo wake.

Hali hiyo imetokana na idara hiyo wiki iliyopita kukamata wahamiaji haramu 24 ambao baadhi yao, walikutwa wameajiriwa maeneo ya
vijijini kufanya shughuli za kilimo na wengine kwenye uchungaji wa mifugo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari juzi mjini hapa na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uhamiaji mkoani Shinyanga, Rashid Magetta kukamatwa kwa wahamiaji hao haramu kunatokana na msako maalumu uliofanyika mkoani Shinyanga ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Magetta amesema miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa, walifikishwa mahakamani na kati yao tisa walihukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka miwili gerezani na w engine 15, walirejeshwa nchini kwao Burundi baada ya kubainika walikuwa na umri chini ya miaka 18.

“Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Shinyanga, tunawaonya wananchi wajiepushe na tabia ya kupokea na kuwahifadhi wahamiaji haramu wanaoingia hapa nchini kinyume cha sheria, maana kwa yeyote atakayebainika aelewe
mkondo wa sheria utafuatwa na wanaweza kupata adhabu kubwa.

“Ni vyema wananchi wakaelewa kuwa wahamiaji haramu daima wapo kwa maslahi yao na ya watu waliowaleta hapa nchini, maana wanaweza kufanya lolote baya bila kuweka maanani maslahi ya nchi yetu na ikizingatiwa kuwa katika kipindi hiki ni cha uchaguzi hapa nchini, wanaweza kusababisha kuvuruga uchaguzi kwa matakwa ya matajiri wao,” amesema.