Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania na Idara ya Uhamiaji ya Jamhuri ya Watu wa China imesaini Hati ya Makubaliano (MoU) inayolenga kuimarisha ushirikiano wa masuala ya Kidiplomasia kati ya pande hizo mbili.
Akizungumza katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) Mkoani Kilimanjaro leo Desemba 18, 2023 mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa makubaliano hayo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) alisema kuwa, Wizara itahakikisha kuwa makubaliano yaliyoingiwa leo yanatekelezwa kwa pande zote mbili.
Alisema wanatarajia kunufaika na manufaa kutoka nchini China kwani nchi hiyo ni nchi ambayo imeendelea kuwa na mafanikio makubwa.
“Kutokana na nchi ya China kuwa mbele kimaendeleo pamoja na Kisayansi na Teknolojia tunatarajia Idara yetu ya Uhamiaji nchini, Maafisa na Askari watapata nafasi ya kubadirishana uzoefu katika nyanja mbalimbali za kimafunzo na vitendea kazi na wenzetu wa Jamhuri ya watu wa China”.Alisema Sagini
Naye Naibu Kamishna wa Idara ya Uhamiaji wa Jamhuri ya Watu wa China Mr. Li Junjie alisema kuwa, utiaji wa saini wa Mashirikiano hayo ni fursa nzuri kwa nchi hizo katika kukuza maendeleo na kujenga msingi mzuri wa kiusalama kwa wote katika nyanja za Uhamiaji.
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji nchini Dkt. Anna Makakala amebainisha kuwa moja ya makubaliano hayo ni kubadilishana uzoefu na kupeana mafunzo hususani katika kipindi hiki cha Sayansi na Teknolojia.
Aidha, hafla hiyo ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano kati ya Idara hizo mbili imehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Kaspar Kaspar Mmuya pamoja na Maafisa Waandamizi wa Idara ya Uhamiaji nchini.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â