Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Dodoma
HALMASHAURI ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida ni moja ya halmashauri ambazo wananchi wake wanafaidika na uvuvi wa samaki, na kuweza kupata kipato kinachowasaidia kujiendeleza kimaisha.
Kwa wastani tani 960 za samaki zinavuliwa katika kata za Mgungira, Mwaru na Iyumbu. kupitia Bwawa la Wembere,pia kuna ufugaji wa kutumia mabwawa ambapo wafugaji takribani 20 wanaendelezwa.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Agosti 7, 2024 Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Dkt. Antony Mwangolombe wakati anazungumza na mwandishi wa habari hizi kwenye banda la mifugo na uvuvi la halmashauri hiyo katika Maonesho ya Nanenane ya kitaifa mkoani Dodoma.
“Shughuli za uvuvi zinafanyika katika Bwawa la Wembere ambapo samaki wanaovuliwa ni perege, kambale na kamongo. Kwa mwaka wastani wa tani za samaki zinazovuliwa kwa mwaka ni 960 katika Kata za Mgungira, Mwaru na Iyumbu. Pia kuna ufugaji wa kutumia mabwawa, ambapo wafugaji takribani 20 wanaendelezwa. Pia tuna bwawa la Muyanji ambamo uvuvi wa kujikimu unafanyika” amesema Dkt. Mwangolombe
Dkt. Mwangolombe amesema halmashauri hiyo ina ukubwa wa kilomita za mraba 8,860 ambapo kati ya hizo, kilomita za mraba 3,737 zinafaa kwa ufugaji. Na aina na idadi ya mifugo ni ng’ombe wa asili 417,746, ng’ombe wa maziwa 6,512), mbuzi wa asili 221,355, nguruwe 843, kuku wa asili 913,773 na kuku wa kisasa 28,122.
Dkt. Mwangolombe alizitaja faida zitokanazo na ufugaji na uvuvi kuwa ni chanzo cha lishe bora kwa wananchi wa Wilaya ya Ikungi na maeneo mengine Tanzania. Chanzo cha kipato kwa wakulima na wavuvi, na chanzo cha Mapato ya Ndani ya Halmashauri na maduhuli ya Serikali Kuu
Amesema Miundombinu ya Mifugo iliyopo, wilaya ina jumla ya Majosho 38, kati ya hayo Majosho 16 yanafanya kazi, tisa yapo kwenye ukarabati na 13 ni mabovu kwa kiwango kikubwa. Mabanda ya ngozi yapo saba, minada mitano (Sepuka, Njiapanda, Mtavira, Kaugeri na Ilolo), vituo vya afya ya mifugo vinne (4) (Ikungi, Ihanja, Sepuka na Mungaa),
“Makaro ya kuchinjia tisa (Issuna, Njiapanda, Ihanja, Sepuka, Ikungi, Mungaa, Mgungira, Ighombwe na Puma), Malambo / mabwawa 35 ambayo yote ni mabovu na mbuga moja ya Wembere kama sehemu ya uvuvi, vibanio vya kudumu vya mifugo viwili (Mwaru na Mkiwa), na Mabirika ya kunyweshea maji mifugo 16” amesema Dkt. Mwangolombe
Dkt. Mwangolombe amesema katika malengo ya kupunguza vifo vya mifugo, kupitia Sekta ya Mifugo, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi imekuwa ikitoa huduma za mifugo katika msimu wa mwaka 2022/2023 na 2023/2024. Halmashauri imefanikiwa kukinga magonjwa ya mifugo kwa kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Mapele Ngozi (Lumpy Skin) ngombe 49,628, Mbwa 7,832 dhidi ya Kichaa cha Mbwa (Rabies), kuku 518,703 dhidi ya ugonjwa wa Kideri (Newcastle), kuku 362,927 dhidi ya ugonjwa wa Gumboro na kuku 72,472 dhidi ya ugonjwa wa Ndui (Fowl pox),.
“Kuogesha mifugo kuzuia usambazaji wa magonjwa, ng’ombe 283,173, mbuzi 137,082, kondoo 89,361, mbwa 4,920, na nguruwe 6,284 wameogeshwa na madawa yakuua wadudu wanaokaa kwenye ngozi za mifugo, Mifugo kupewa dawa za minyoo, ambapo ng’ombe 238,073, mbuzi 109,836, kondoo 47,261, kuku 579,362, mbwa 5,973 na nguruwe 4,284 wamenyeshwa dawa za minyoo, na kutoa huduma ya matibabu imetolewa kwa mifugo iliyopata magonjwa na kupona kwa asilimia 97” amesema Dkt. Mwangolombe
Dkt. Mwangolombe amesema kwenye Sekta ya Uvuvi, Wilaya ya Ikungi ina jumla ya Mialo mitatu kwa ajili ya shughuli za uvunaji samaki kukiwa na wavuvi wapatao 507, Mitumbwi 198 na kuna ofisi tatu za usimamizi wa rasimali za uvuvi ambazo ni ofisi za wataalamu wa mifugo wa kata husika kwa kushirikiana na watendaji wa vijiji, kata na halmashauri.
“Wastani wa mavuno kwa mwezi ni tani 80 ambazo hutofautiana kulingana na majira, wakati wa mvua uzalishaji unakua juu ukilinganisha na kiangazi ambapo sehemu kubwa ya Bwawa hukauka. Pia tuna wafugaji wadogo wa samaki kwa njia ya mabwawa takribani wafugaji 20 ambao wanaendelea kupatiwa elimu ya ufugaji wa kisasa kwani bado wanafuga kienyeji na upatikanaji wa mbegu bora za vifaranga wa samaki. Shughuli za uvuvi pia hufanyika katika Bwawa dogo la Muyanji linalopatikana katika kata ya Makiungu na Mungaa japokua uzalishaji wake bado ni mdogo” amesema.Dkt. Mwangolombe.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best