December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ufaransa yatoa ufadhili vyuo vikuu nchini

Na David John, Timesmajira online

UBALOZI wa Ufaransa Nchini Tanzania umtoa ufadhili wa mradi wa ubunifu wa ‘Innoversity Project’ kwa miaka miwili unaolenga wanafunzi wa vyuo vikuu vitatu vya Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia.

Baadhi ya vyuo ambao vimefaidika na ufadhili huo ni chuo cha Nelson Mandela (Arusha,) Chuo kikuu cha Sokoine (SUA,) na Chuo Kikuu cha Iringa kwa ruzuku ya Euro 570, 000 kwa malengo ya kuimarisha Taasisi na nyenzo za elimu ya juu Tanzania, kusaidia safari ya ujasiriamali ya wanafunzi pamoja na kukuza ujasiriamali na ajira.

Akizungumza na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini Balozi wa Ufaransa hapa Tanzania Nabil Hajloui JIjini Dar Es Salaam amesema Mradi huo wa ubunifu na uvumbuzi uliofadhiliwa na Ubalozi wa Ufaransa nchini unatekelezwa na kampuni ya Sahara Ventures ambao ni wataalam wa biashara na kilimo Kwanzaa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH.)

Ameongeza kuwa mradi huo wa uvumbuzi unaunga mkono juhudi za Serikali katika kuvipa vyuo vikuu maarifa, zana na rasilimali za kukuza ubunifu, ujuzi wa kujiajiri na ujasiriamali na wanategemea matokeo chanya kwa kunufaisha Tanzania na nchi nyingine za Afrika.

” Pamoja na kudumisha mahusiano bora yaliyopo baina ya Ufaransa na Tanzania pia tunatambua jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika masuala ya ujasiriamali na uvumbuzi na hata alipotembelea Paris alitembelea sehemu nyingi na kuzungumza namna ya kuleta ujuzi hapa nchini kwa manufaa ya watanzania hasa vijana.” Amesema balozi Hajloui

Afafanua kuwa ndani ya miaka miwili ya utekelezaji wa mradi huo vijana watumie kujijenga kimaarifa na kuweza kutengeneza biashara zitakazonufaisha taifa na jamii kwa kuzalisha ajira nyingi zaidi.

Naye Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH,) Samson Mwela amesema, mradi huo wenye lengo la kuwezesha wabunifu na wajasiriamali umeweka mkazo katika sekta ya kilimo na ujasiriamali kwa vijana wa vyuo vikuu ili kutatua changamoto ya ajira.

”Serikali inatoa fedha nyingi kusaidia tafiti na bunifu kupitia COSTECH, mwaka huu imetoa bilioni 3.5 na mwakani tunategemea kupokea bilioni 5 zaidi niwatake vijana na wabunifu kutoka vyuo nufaika vya mradi huu wajitokeze kupitia mradi huu na miradi mingine mingi inayosimamiwa na COSTHECH.” Amesema.

Pia amesema kuwa, kwa sasa Serikali inatekeleza mradi wa miaka mitano wa maendeleo uliolenga kutengeneza ajira nyingi zaidi kupitia ubunifu na uvumbuzi na mradi huo utaongeza nguvu zaidi katika kutatua changamoto ya ajira na kutengeneza biashara nyingi zitakazosaidia kukuza pato la taifa kupitia kodi.

”Mradi huu utanufaisha zaidi ya wanafunzi vijana 300 pamoja na wahadhiri na watafiti kutoka vyuo vikuu vitatu Tanzania, huu ni mradi wa kihistoria kwa kuwa kutakuwa na ubadilishanaji wa ujuzi kwa watanzania kwenda Ufaransa na vijana wa Ufaransa kuja Tanzania kujifunza zaidi.” Amesema.

Mwela ameshukuru Serikali ya Ufaransa kwa kuendeleza ushirikiano wenye tija na Tanzania na kuahidi ushirikiano katika kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa asilimia 100.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Sahara Ventures Jumanne Mtambalike ambao ni watekelezaji wa mradi huo amesema kuwa,wamekuwa daraja la kuiweka Serikali na Ubalozi kupitia mawazo ya ubunifu kutoka kwa wanafunzi na wahadhiri ili kuhakikisha mawazo hayo yanafanyiwa kazi na kuleta tija kwa jamii ya sasa hasa kwa vijana na kuwataka wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza na kuunga mkono jitihada hizo.

Mradi huo utafanya kazi na vituo vya uvumbuzi vya vyuo vikuu na ofisi za kuhamasisha teknolojia ili kuhimiza zaidi uvumbuzi, ujasiriamali, uhamishaji wa teknolojia na biashara ya utafiti ili kuunda suluhisho jipya na fursa za ajira.

Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajloui akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari (hawamo pichani) kuhusu ufadhili wa Mradi wa miaka miwili wa ‘Innoversity’ katika makazi yake leo Mei 24, 2022 Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Samson Mwela (kushoto) akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (hawamo pichani) alipokuwa akielezea juu ya Mradi huo, Jijini Dar es Salaam. (kulia) Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajlaoui
Afisa Mtendaji Mkuu wa Sahara Ventures Jumanne Mtambalike (katikati) akizungumza katika mkutano huo leo Jijini Dar es Salaam. (kulia) ni Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajlaoui, na (kushoto) ni Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Samson Mwela
Picha za waandishi wa habari kutoka katika vyombo mbalimbali vya habari wakiwa katika mkutano huo.