November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uendelezwaji miradi ya maji kudumisha huduma ya maji safi Nsimbo

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Nsimbo.

Miradi ya maji imetakiwa kuwa endelevu ili kufikia azima ya serikali ya kuhakikisha wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini wanapata huduma bora ya maji safi na salama kwa zaidi ya asailimia 85 ifikapo mwaka 2025.

Uendelevu wa miradi ya maji unahusisha kufanya jitihada za kujenga na kukarabati miradi ya maji pamoja na kupanua mitandao ya kusambaza maji na kuimarisha usimamizi wa huduma ya maji kwa wananchi wenye uhitaji zaidi.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Godfrey Mnzava amebainisha hayo leo Septemba 11, 2024 katika kijiji cha Ikondamoyo halmashauri ya Nsimbo mara baada ya kupokea taarifa ya mradi wa maji.

“Ninachotaka kuagalia kwenye mtandao wa maji ni miundombinu yenyewe ambayo inatoa huduma ya maji. Je kuna uendelevu wowote unafanywa? Mathalani kulikuwa na mita 700 lakini sasa tumeongeza mabomba kwa mita 300 zaidi”amesema Kiongozi huyo.

Mradi wa maji wa kijiji cha Ikondamoyo umetembelewa na kiongozi huyo wa mbio za mwenge wa uhuru ili kuona uendelevu wake katika kuwahudumia wananchi ambapo ni takribani mwaka mmoja tangu uzinduliwe na mbio za mwenge wa uhuru mwaka jana ukiwa na magati sita.

Mnzava amesema kuwa licha ya kuwepo kwa juhudi mahsusi za kupanua mtandao kwa mita 500 ni muhimu kazi hiyo ikafanywa kwa wakati kwani itasaidia kuondoa utengano na kujenga umoja na upendo ndani ya jamii yenye uhitaji wa maji na salama utakaosaidia kuepuka magonjwa ya mlipuko kwa kunywa maji yasiyo safi na salama.

Ni wazi kuwa wito uliotolewa na kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa 2024 kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kufanya miradi ya maji kuwa endelevu unakwenda sambamba na hotuba ya Waziri wa maji, Jumaa Aweso aliotoa akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na mtumizi ya fedha ya wizara hiyo mwaka 2024/25

Aweso alisema jitihada za uendelevu wa miradi ya maji unawezesha kuongezeka kwa hali ya upatikaji maji kutoka wastani asilimia 77 mwezi Disemba, 2023 kiwango kilichoongezeka kimetokana na kutekelezwa miradi mbalimbali nchini.

Awali Msimamizi wa mradi wa maji huo, Scholastica Mvungwa amesema ujenzi wa mradi huo ulianza Februari, 2022 na kukamilika Juni 30, 2022 kwa gharama ya fedha Mil 519.4 ukihusisha ujenzi wa kitega maji, uchimbaji mtaro, ulazaji na uunganishaji wa mabomba Km 10.2 na ujenzi wa vituo sita vya kuchotea maji.

Scholastica amefafanua kuwa mradi huo kwa sasa unanufaisha zaidi ya wananchi 2,603 wa kijiji cha Ikondamoyo sambamba na kutoa huduma hiyo umekusanya kiasi cha fedha Mil 1.31 na ifikapo Juni, 2025 chombo kitaongeza makusanyo kutoka wasitani wa Mil 1.31 kwa mwaka na kufikia Mil 6.

Mkazi wa Kijiji cha Ikondamoyo, Aisha Ramadhani ameiomba RUWASA kuongeza mtandao wa maji katika vitongoji vingine zaidi ili kusaidia upatikanaji wa maji safi na salama utakao wasaidia kuacha kwenda umbali mrefu kutafuta maji.

Aisha amesema kuwa upatikanaji wa maji safi na salama kwa umbali mrefu umekuwa chanzo cha wanawake na wasichana kupitia hali ngumu ya ukatili mbalimbali kama vile kipigo kutoka kwa waume zao kwa sababu ya kutumia muda mrefu kuteka maji.

Aidha Mwenge wa Uhuru ukiwa katika halmashauri ya Nsimbo Mkoa wa Katavi umefanikiwa kukimbizwa kwa urefu wa Km 139 na kupitia miradi 9 yenye thamani ya Bil 1.04 ambapo baadhi ya miradi hiyo miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu shule ya sekondari Mkaso, Ujenzi wa zahanati kijiji cha Iteka B na ujenzi wa daraja la upinde wa mawe katika kijiji cha Ibindi.