December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UDOM yaja na mfumo wa kuonesha mwanafunzi akiwa kwenye mazoezi ya vitendo

Na Penina Malundo, timesmajira

CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM), kinatarajia kukamilisha mfumo ambao utakuwa unaonesha wakati wote mwanafunzi wa Chuo hicho anayesomea fani ya daktari na nesi akiwa katika mazoezi ya vitendo kwenye Hospitali.

Akizungumza jijini Dar es salaam juzi,Makamu Mkuu wa Chuo Cha UDOM, Profesa. Lughano Kuziluka amesema kuwa Programu hiyo inaonesha ni kitu gani mwanafunzi anatakiwa kukifanya akiwa kwenye kitanda anachomuhudumia mgonjwa.

Prof. Kuziluka amesema uzuri wa programu hiyo inawarahisishia kujua kila mwanafunzi anapohudhuria mafunzo hayo lazima awepo anapotakiwa kuwepo kwa wakati unaotakiwa.

Aidha amesema kuwa chuo hicho kina programu ya utunzaji wa kumbukumbu za afya, namna ya kufuatilia wanafunzi ambao wanasoma masomo ya udaktari, nesi wanapokuwa katika mafunzo yao hospitalini.

“Chuo cha UDOM tupo hapa kwa sababu ni wadau wakubwa wa maonesho haya tumekuja kuwafahamisha Watanzania kuwa Chuo chetu ni moja ya Vyuo vikuu vikubwa nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika Mashariki mtu akiingia atapata programu zetu zote,” amesema.

Ameongeza kuwa kumbukumbu za kwenye karatasi wakati mwingine ufuatiliaji wake unakuwa mgumu ambapo programu hiyo inatoa taarifa zote za mwanafunzi na kuwasaidia walimu kujua mwanafunzi huyo anafanya nini.

Pia amesema chuo hicho kinafanya Utafiti,Ubunifu na Uvumbuzi zikiwamo za kutunza mazingira kwa kutengeneza mapambo ya nyumbani kupitia chupa zinazotupwa lengo likiwa ni kupunguza uchafu unaoharibu mazingira.

Prof. Kuziluka amesema kuwa ni matumizi mazuri ya rasilimali ambazo zimetumika kukwekea vimiminika na baadae kutupwa na kuchafua mazingira.

“Tunatamani kuwa na nchi yenye mazingira mazuri na watu wanaishi katika mazingira safi hivyo nawakaribisha Watanzania kuja kuona Ubunifu huu wa chupa na kuzinunua kwa ajili ya kuzitumia nyumbani,” alisema Prof. Kuziluka.

Prof. Kuziluka amesema katika maeneo mbalimbali changamoto inayokuwepo ni kujua mazao yaliyopo yanapata unyevunyevu, joto la kutosha na maji ya kutosha huku akisema wataalam wao wamefanya Utafiti na kujua mfumo ambao wakati wowote unawezakusaidia kupunguza au kuongeza, joto, unyevunyevu kulingana na mahitaji ya mazoa husika.

Akizungumzia programu za masomo wanayoyatoa chuoni hapo amesema kuwa chuo kina toa programu kuanzia ngazi ya shahada, shahada ya kwanza, shahada za umahiri hadi shahada za Uzamili na Uzamivu na kwamba wapo wataalam wanaotoa taarifa hizo kwa ufasaha.