Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF)umesema katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita umewapatia mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Walimu 1585 kwa lengo la kuwajengea uwezo kutatua matatizo ya vifaa hivyo pindi vinapopata changamoto.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Machi 27,2025 na Mtendaji Mkuu wa UCSAF,Mhandisi Peter Mwasalyanda wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Mfuko huo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Mha.Mwasalyanda amesema elimu hiyo kwa walimu itawawezesha kuvielewa vifaa vya TEHAMA hata pale vinaposumbua wasipate usumbufu wa kuwatafuta mafundi kwa mambo ambayo wanaweza kuyafanya wenyewe na kuwafundisha wanafunzi kwa uelewa zaidi.
Aidha amesema kuwa kwa kutambua mchango wa TEHAMA shuleni wamefikisha vifaa vya TEHAMA shule za umma 1,121 ambapo kwa wastani shule hupata Kompyuta tano,Printa moja na Projecta moja na gharama za mradi huo wa kupeleka vifaa hivyo ni shilingi Bilioni 5.94
“Katika kipindi cha miaka minne ya Awamu ya sita shule 469 zimepelekewa vifaa vya TEHAMA lengo ni kukuza ujuzi wa TEHAMA kwa Wanafunzi na Walimu nchini,”amesema.
Vilevile amesema kila mwaka mfuko huo unaratibu maadhimisho ya siku ya wasichana na TEHAMA ambayo hufanyika mwezi April kila mwaka lengo ni kuhamasisha na kukuza uelewa wa masuala ya TEHAMA kwa wasichana
” Maadhimisho ni mpango ulioanzishwa na ITU na Mpaka kufikia sasa tumetoa mafunzo kwa wanafunzi takribani 1202.Awamu ya sita chini ya Mhe.Rais Dtk.Samia Suluhu imetoa mafunzo kwa wanafunzi takribani 490 kutoka shule 304 na kwa mwaka 2024/2025 Mwezi Aprili tunatarajia kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa kike takribani 248 mafunzo haya yanasaidia na kuhamasisha watoto wakike kupenda masomo ya Sayansi,”amesema.
Pia Mha.Mwasalyanda amesema kuwa wamepeleka vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya bil.1.8 katika shule 22 zenye watoto wenye mahitaji maalum.
Ametaja vifaa hivyo kuwa ni
TV, Braille Machine (Nukta Nundu) Orbit reader (Machine za Kisasa), Laptops, Embosser (Printa ya nukta nundu), Digital voice recorders, Magnifiers.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa Minara 758 ambao serikali katika kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za mawasiliano nchi mezi Mei 2023 iliingia mikataba na watoa huduma kwa ajili ya kufikisha mawasiliano maeneo ya vijijini.
Mradi huo wa ujenzi wa minara 758 ni mradi mkubwa kuwahi kutekelezwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote
Mha.Mwasalyanda amesema hadi kufikia tarehe 24 Machi 2025 minara 430 imejengwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo ya vijiji.
Kwa upande wa mradi wa kuboresha uwezo wa minara amesema Minara 304 imeongezwa nguvu kutoka 2G kwenda 3G/4G na ruzuku ya bil.5.51 imetumika na Minara 304/304 imekamilika.




More Stories
EWURA kinara uhusiano mwema na vyombo vya habari nchini
TANESCO yaibuka kinara tuzo za ubora za Mawasiliano na Uhusiano kwa umma 2024
Taasisi za uhifadhi zatakiwa kulinda maeneo ya hifadhi kwa teknolojia