November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uchimbaji madini ya Kinywe mbioni kuanza Mtama

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online

WAZIRI wa Madini Dkt. Doto Biteko amewataka wananchi wa Kijiji cha Namangale katika Halmashauri ya Mji wa Mtama Mkoani Lindi kutoa ushirikiano kwa mwekezaji wa madini ya Kinywe ili aweze kulipa fidia kwenye maeneo yatakayo jengwa mgodi.

Dkt. Biteko amesema hayo Juni 18, 2023 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Namangale Mkoani Lindi ambapo amesema mgodi huo utasaidia kuongeza ajira na kuchochea maendeleo kwa wananchi wa Kijiji hicho kupitia shughuli za uchimbaji madini.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Biteko amesema Kampuni ya Volt Resources Limited kutoka nchini Australia inatarajiwa kawekeza zaidi ya Dola za Marekani milioni 40 katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa mgodi huo ambapo inakadiriwa kuwa na hifadhi ya zaidi ya tani milioni 461 za madini ya Kinywe katika kijiji cha Namangale Mkoani Lindi.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ameiomba Wizara ya Madini kuisimamia kwa karibu Kampuni ya Volt Resources Limited ili kuhakikisha mradi wa uchimbaji wa madini ya Kinywe katika kijiji cha Namangale unaharakishwa ili wananchi wa Mkoa wa Lindi wapate ajira.

Pamoja na mambo mengine, Nnauye amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameufungua mkoa wa Lindi ambapo kwa sasa Taifa linashuhudia miradi mingi ya maendeleo ikifanyika mkoani humo ukiwemo mradi wa uchimbaji madini ya Kinywe unaotarajiwa kujengwa katika kijiji cha Namangale.

Katika ziara hiyo Dkt. Biteko ameambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) ili kusisitiza mradi huo unaanza kulipa fidia kwa wananchi ili uanze uzalishaji kwa wakati.