Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
JAMII Mkoani Tabora imeshauriwa kujenga utamaduni wa kutunza vizuri mazingira yanayowazunguka ili kuepuka athari za kiafya zinazosababishwa na uchafuzi wa mazingira.
Ushauri huo umetolewa na Afisa Afya wa Wilaya ya Igunga Mkoani hapa Mhoja Lubeja alipokuwa akitoa Elimu ya Afya na Mazingira kwa Wenyeviti na Wajumbe wa Serikali za Vijiji na Vitongoji katika kata ya Ndembezi Wilayani humo.
Alisema katika maeneo yote ambayo wananchi wametambua umuhimu wa kutunza mazingira na kushiriki kikamilifu kuyatunza hakuna magonjwa nyemelezi wala ya mlipuko ambayo yamejitokeza na hata yakitokea madhara yake ni madogo.
Alisisitiza kuwa utunzaji mazingira hupelekea jamii ya eneo husika kuwa na afya bora lakini uharibifu wa mazingira ni adui mkubwa wa afya ya jamii, hivyo akatoa wito kwa Viongozi wa Serikali za Vijiji kuhamasisha wananchi kupanda miti.
‘Kupanda miti kuna boresha mazingira na mazingira yakiboreshwa afya ya jamii inaimarishwa, hivyo tulinde afya zetu kwa kutunza vizuri mazingira yanayotuzunguka’, alisema.
Lubeja alibainisha kuwa miradi ya maendeleo inapotekelezwa katika maeneo mbalimbali suala la afya halina budi kupewa kipaumbele kwa kuhakikisha vifaa kinga vinapatikana na kuboresha mazingira kwa kupanda miti ya kutosha.
Alisisitiza kuwa kila Mkandarasi anayepewa kazi ya kutekeleza mradi wa maji au barabara anawajibu wa kulinda afya ya wananchi waliopo katika eneo la mradi ikiwemo kutumia kinga katika mahusiano yao ya kimapenzi.
Alibainisha kuwa miradi ya maendeleo ni fursa muhimu sana kwa wananchi lakini jamii inapaswa kuchukua tahadhari ya mazingira wakati wote ili kulinda afya zao, na hata miti inapokatwa wajenge utamaduni wa kupandwa mingine.
Kwa upande wake Afisa Misitu wa Wilaya hiyo Emanuel Manka aliwataka Viongozi wa Serikali za Vijiji kuwa mabalozi wazuri kwa kuhamasisha jamii kupanda miti ya kutosha ili kuepuka athari za tabia nchi na uharibifu wa mazingira.
Alifafanua kuwa misitu ni uhai, ikitunzwa vizuri jamii itapata mvua za kutosha, kuni, mkaa, mbao, hewa safi na ardhi itaendelea kuwa rafiki kwa shughuli za kilimo lakini wakikata miti ovyo shughuli nyingi za kimaendeleo zitakwama.
More Stories
Wenje:Tuwanadi wagombea bila kuchafuana
Mtoto darasa la tatu adaiwa kujinyonga kwa kukosa nguo ya sikukuu
Jeshi la Polisi Katavi laanika mafanikio 2024