January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ubora bidhaa za AFRICAB wavutia wengi Sabasaba

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar

UBORA wa vifaa vya umeme vinavyozalishwa na Kiwanda cha Kilimanjaro Cables (AFRICAB) vimetajwa kuchochea wananchi wengi kutembelea banda la kiwanda hicho liliopo kwenye Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Mwalimu Julius Nyerere maarufu kama Sabasaba yanayoendelea Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa na Mratibu na Msimamizi wa Mauzo wa Kiwanda cha AFRICAB, Mhandisi Johnson Mabesa, alipokuwa akizungumzia ubora wa bidhaa hizo jana kwenye banda la maonesho hayo.

Amesema mwitikio wa wananchi kutembelea banda la kampuni hiyo lililopo sabasaba umetokana na ubora wa bidhaa za kampuni hizo kukubalika kwa wananchi.

Mhandisi Mabesa amesema tofauti na kipindi cha nyuma kwa sasa kumekuwepo na mwamko mkubwa kwa Watanzania wanaojitokeza mahali hapo na maeneo mengine ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam kununua bidhaa zao, jambo linaloonesha wametambua ubora wake wakilinganisha na vifaa vya aina hiyo vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi.

“Hakuna ubishi Tanzania inazidi kupiga hatua kubwa katika sekta ya viwanda na hasa upande huu wa vifaa vya umeme, zamani Serikali ilikuwa inapoteza fedha nyingi kwa kuagiza vifaa kutoka nje ya nchi, lakini kwa sasa suala hilo halipo kwa kuwa viwanda vingi vya AFRICAB vinafanya vizuri kwa kuzalisha vifaa mbalimbali kwa ubora wa hali ya juu,” amesema.

Amesema ubora wa vifaa vinavyozalishwa na kiwanda hicho, siyo unatambulika na wananchi pekee, bali hata viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye hivi karibuni alitembelea kiwanda hicho hicho na kueleza kuridhishwa na ubora wa vifaa vinavyozalishwa, huku akitoa rai kwa Watanzania kuthamini bidhaa za ndani.

Amesema hata ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo miundombinu ya umeme na mengine inayoendelea kujengwa nchini kwa sasa inawezeshwa na vifaa vya umeme vinavyozalishwa na viwanda vya ndani, jambo linaloonesha wazi kuwa kwa sasa Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta hiyo tofauti na miaka ya nyuma.

Amesema kiwanda cha AFRICAB kinachozalisha nyaya, transfoma na aina nyingine ya vifaa mbalimbali vya umme, mbali na kuuza bidhaa zake hapa nchini pia hufanya biashara ya kuuza vifaa hivyo katika nchi mbalimbali ikiwemo Zambia, Malawi, Congo DRC na kwingineko katika Bara la Afrika.

“Tunazidi kuwahimiza na kuwakumbusha Watanzani kuwa kwa sasa hakuna ubishi bidhaa za hapa ndani zina ubora wa hali ya juu kushinda zinazotoka nje ya nchi.

Tunawakaribisha katika banda letu hapa Sabasaba waje kujionea na zaidi tumetoa punguzo maalumu kwa ajili ya sikukuu hii ya sabasaba, hatua hii imelenga kuonesha kuwa tunawathamini kama Watanzania wenzetu,” anasema Mhandisi Mabesa.