November 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uamuzi wa Rais Samia kuifungua nchi kiabishara waleta kongamano la Kahawa

Na Iddy Lugendo,Timesmajiraonline,Dar

UAMUZI wa Rais Samia Suluhu Hassan kuifungua nchini kiabiashara umeipa nguvu Bodi Chama cha Kahawa Bora za Afrika (AFCA) kwa kushirikiana na Bodi Kahawa Tanzania (TCB) kuandaa kongamano la maonesho ya 21 ya Kahawa Bora Afrika litakalofanyika nchini Februari 26-28, mwakani 2025.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Bodi ya AFCA, Amir Hamza, wakati akizungumza kwenye mkutano ulioandaliwa na AFCA kwa kushirikiana na TCB uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo linakuja kufanyika nchini huku TCB kwa kushirikiana AFCA ikisema zao la kahawa limeendelea kuwa kivutio kikubwa duniani na kwamba kwa sasa uzalishaji wake nchini umefikia tani 85,000 kwa mwaka kutoka tani 50,000.

Mkurugenzi Mtendaji wa TCB, Primus Kimaryo katika mkutano huo ulioandaliwa na AFCA) kwa ajili ya maandalizi ya kongamano la maonesho ya 21 ya kahawa bora Afrika yanayotarajiwa kufanyika nchini Februari 26-28, mwakani 2025.

Alisema kupitia kongamano na maonesho hayo, wazalishaji, wafanyabiashara na wakaangaji wa kahawa duniani wamealikwa kushiriki kongamano na maonesho ya 21 ya kahawa bora Afrika, ambapo mpango wa kuendelea kukuza uzalishaji zao hilo na kufikia tani 300,000 kwa miaka mitano ijayo umeandaliwa.

Alisema zaidi ya wakulima wadogo 320,000 wanategemea kahawa ya hapa nchini, pia watu milioni mbili wanaitegemea kahawa katika maeneo mbalimbali.

“Kahawa imekuwa kivutio kikubwa duniani inaingiza dola milioni 200 ni chanzo kikubwa cha mapato katika nchi,” alisema.

Alisema jitihada wanayoifanya ni kushirikisha wadau katika mnyororo wa kahawa, pia kutengeneza mazingira wezeshi ili kila mtu awekeze, auze na kufurahia fursa zote zilizopo kwenye kahawa.

Kimaryo alisema kongamano hilo linatoa fursa ya pekee kwa nchi ya Tanzania baada ya kufunguka kibiashara.

“Tanzania sasa uzalishaji wetu wa kahawa unaendelea kuongezeka,imekuwa ni fursa kwetu kuona ni namna gani tunaileta tena dunia ya kahawa hapa nchini,” alisema.
Kauli mbiu ya Kongamano la 21 la AFCC&E ni;

“Kuhuisha Ongezeko la Thamani,” na litakuwa na orodha ya wazungumzaji maarufu kimataifa na kikanda.

Kongamano hilo pia litajumuisha maonesho yatakayoonyesha ubunifu na maendeleo ya hivi karibuni katika sekta ya kahawa, pamoja na warsha, vipindi vya kuonja kahawa (B2B cupping sessions), na ziara maalum zilizopangwa kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu kahawa.

Kongamano hili pia litajumuisha Mashindano ya watayarisha kahawa Afrika na Mashindano ya kahawa bora katika ukanda wa Afrika, ambayo yataonyesha vipaji bora na bidhaa za kahawa bora kutoka kote barani.