Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MAABARA ya Veterinari hapa nchini (TVLA) ,katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2017/2018 hadi Septemba 30, 2022,imezalisha jumla ya chanjo dozi 282,492,549 zikiwemo za mdondo wa kuku na kusambazwa nchini.
Mtendaji mkuu wa wakala ya maabara ya veterinari tanzania, Dkt. Stella Bitanyi akizungumza na waandishi wa habari jijini dodoma kuhusu utekelezaji na vipaumbele kwa mwaka 2022/23 huku akisema mwaka 2021/2022 uzalishaji wa chanjo ulifikia dozi milioni 65 ambapo uwezo kamili wa uzalishaji wa chanjo ni zaidi ya dozi milioni 100 kwa mwaka.
“Hata hivyo uzalishaji huo bado haujafikiwa kutokana na uhitaji wa soko kuwa chini. “amesema Dkt.Bitanyi
Ametaja chanjo zinazozalishwa na Wakala ni pamoja na chanjo stahimilivu joto ya kukinga kuku dhidi ya ugonjwa wa Mdondo, chanjo ya ugonjwa wa Kimeta, chanjo ya ugonjwa wa Chambavu, chanjo ya homa ya mapafu ya ngombe, chanjo ya ugonjwa wa kutupa mimba; chanjo mchanganyiko wa kimeta na chambavu na chanjo ya homa ya mapafu ya mbuzi.
.
Kwa mujibu wa Dkt.Bitanyi ,lengo la Wakala katika kipindi cha muda mfupi ni kuongeza chanjo mbili dhidi ya magonjwa ya kichaa cha mbwa na sotoka ya mbuzi na kondoo ambapo utafiti wa kuzalisha chanjo hizi upo katika hatua mbalimbali.
Aidha alisema, uzalishaji wa chanjo hizi unategemewa kuanza mwaka 2022/2023 na ukikamilika utaifanya Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) kufikia idadi ya aina tisa za chanjo kutoka chanjo saba zinazozalishwa na taasisi hiyo .
Akizungumzia malengo ya Taasisi hiyo,Mtendaji Mkuu huyo amesema,ni kuongeza idadi ya chanjo kufikia chanjo 13 za kimkakati kutokana na mkakati wa Serikali unaolenga kudhibiti magonjwa 13 ya kipaumbele.
Aidha amesema,pamoja na mambo mengine , Wakala umefanikiwa kuongeza mapato ya ndani yanayotokana na utoaji wa huduma na usambazaji wa bidhaa zake kutoka Shilingi Milioni 220 mwaka 2013/2014 hadi kufikia Shilingi bilioni 3.1 mwaka 2021/2022 sawa na ongezeko la asilimia 1,409.
Amesema,Wakala ilianza kuzalisha chanjo moja ya Mdondo Mwaka 2013/2014 na hadi sasa inazalisha aina saba za chanjo. Kiwango cha uzalishaji kimepanda kutoka dozi Milioni 21 mwaka 2013/2014 kufikia dozi milioni 65 mwaka 2021/2022.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba