Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imepokea tuzo 3 za ushindi kwenye maonesho ya Nanenane kwa kanda 3 ambazo imeshiriki maonesho hayo.
Tuzo ya kwanza imetolewa Dodoma na Mgeni rasmi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo TVLA imeshika nafasi ya kwanza katika kundi la Wakala wa Serikali zinazotoa huduma pamoja na Uzalishaji kwenye kilele cha Maonesho Nanenane Kimataifa yaliyofanyika katika viwanja vya Nzuguni mkoani Dodoma Agosti 8, 2024.
Tuzo ya pili imetolewa Bariadi Simiyu na Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Mtambi ambapo TVLA imeshika nafasi ya pili katika kundi la Taasisi za Serikali zilizoshiriki kwenye maonesho ya Wakulima (Nanenane) Kanda ya Ziwa Mashariki yaliyofanyika katika viwanja vya Nyakabindi
Tuzo ya tatu imetolewa Mkoani Lindi na Mhe. Kapt George Mkuchika Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu Kwenye maonesho Kilimo (Nanenane) kanda ya Kusini ambapo TVLA imeshika nafasi ya 3 kwa Taasisi zinazotoa huduma pamoja na utafiti
Akitoa salamu za shukrani Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi ameushukuru uongozi wa Wizara pamoja na kamati zote za maandalizi kwa ushirikiano walioutoa kuanzia kipindi cha maandalizi ya maonesho hayo hadi siku ya kilele.
“Mwaka huu TVLA tumepokea tuzo 3 za ushindi katika utoaji wa huduma kwa wafugaji na wadau wa mifugo, kipekee ninawapongeza watmishi wote wa Wakala kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kwamba wafugaji nchini wanapata huduma iliyo bora siku zote.”
“Kama Wakala tunaahidi kuendelea kutoa huduma bora zaidi ili kuboresha afya za mifugo na kuongeza pato la mfugaji mmoja mmoja na pato la Taifa kwa ujumla” Alisema Dkt. Bitanyi.
Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania imeshiriki maonesho ya kilimo kwa kanda zote nane kwa kutoa huduma pamoja na elimu katika masuala ya Uchunguzi na Utambuzi wa magonjwa ya Mifugo, Uzalishaji na Usambazaji wa Chanjo za Mifugo, Uhakiki wa ubora wa vyakula vya Mifugo, Usajili na Uhakiki wa ubora wa Viuatilifu vya Mifugo, Utafiti wa magonjwa ya Wanyama pamoja na Huduma ya Ushauri na Mafunzo.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango