January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tuzingatie miongozo ya Corona-Serikali

Na Hadija Bagasha,TimesMajira Online

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesisitiza miongozo yote iliyotolewa kwa umma kujikinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona (COVID-19) izingatiwe ili kuepuka kasi ya maambukizi zaidi.

Pia Serikali imejiwekea malengo ya kuhakikisha hadi ifikapo 2025 kiwango cha ugonjwa wa malaria kinakuwa chini ya asilimia 3.5 ambapo hivi sana ni asilimia 7.5.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Kinga wa wizara hiyo, Dkt.Leonard Subi wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa huduma za kinga juu ya matumizi sahihi kutumia dawa za viuatilifu vya magonjwa yanayoenezwa na wadudu kutoka halmashauri 62 za Tanzania Bara na Visiwani yanayofanyika wilayani Muheza mkoa wa Tanga.

Dkt.Subi amesema kuwa, hali na mwenendo wa ugonjwa wa Covid-19 duniani bado ni kizungumkuti hususani sasa katika nchi za Afrika zipo kwenye maambukizi makubwa na kueleza kuwa Tanzania kuna maambukizi ya virusi hivyo ambavyo tayari vimeshaweza kuleta athari duniani, hivyo ni muhimu kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga.

“Tanzania ugonjwa upo na baadhi ya mikoa kama Arusha, Dar es Salaam, Shinyanga na Dodoma kumeripotiwa uwepo wa wagonjwa hivyo cha muhimu ni kuchukua tahadhari kama ambavyo miongozo iliyotolewa na wizara inavyoelekeza,”amesema Dkt.Subi.

Hivyo amewataka wataalamu hao wa afya kwa kushirikiana na wizara kuendelea kuhimiza wananchi kujikinga dhidi ya COVID-19 ikiwemo kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono, kuvaa barakoa, kukaa umbali, kufanya mazoezi, lishe bora.

Akizungumzia ugonjwa wa malaria, Dkt.Subi amesema kuwa, pamoja na ugonjwa huo kuwepo kwa miaka mingi, lakini ugonjwa huo bado upo hivyo wamekubaliana hadi ifikapo 2025 kiwango cha malaria kiwe asilimia 3.5.

“Kwa nini tusiwe chini ya asilimia 3.5 tumekubaliana na ndio kipimo cha programu inapofika 2025 kwa mbinu zozote zile piga ua lazima ushike na nyinyi mnapaswa kuonyesha nia na kutekeleza wajibu wenu kwenye eneo hili la malaria,”amesistiza Dkt.Subi.

Sambamba na hayo aliwataka wataalamu hao kuhakikisha watu wanapinga malaria, lakini wahakikishe hawawi wezi wa vitendanishi vya malaria na kupeleka kwenye maduka ya watu binafsi.

“Kila kitendanishi lazima tujue kimempima nani tarehe ngapi saa ngapi na kiko wapi, nyinyi lazima mjue kwenye kijiji gani wanatoka wagonjwa na kwa nini watoke huko tunapaswa kutumia sayansi tuliyonayo twendeni kwenye maeneo ya watu tukawaelimishe na kuwaambia ni namna gani tuondosha ugonjwa wa malaria,”amebainisha.

Hata hivyo, msimamizi wa mafunzo hayo, Charles Dismas amesema kuwa, katika kufikiwa lengo la Serikali ni ifikapo 2030 tuwe tumeweza kutokomeza magonjwa kama Malaria ambayo bado ni tishio katika Taifa letu kwa kuendelea kuleta athari ikiwemo vifo.

Mkurugenzi na Mtafiti Mkuu Kiongozi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kituo cha Muheza, Dkt. William Kisinza akizungumza wakati wa kuwajengea uwezo Wataalamu wa Afya wa huduma za Kinga juu ya matumizi sahihi kutumia dawa za viuatilifu vya magonjwa yanayoenezwa na wadudu kutoka Halimashauri 62 za Tanzania bara na Visiwani yanayofanyika wilayani Muheza mkoa wa Tanga. (Picha na Hadija Bagasha Muheza).

Nae Mkurugenzi na mtafiti mkuu kiongozi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu NIMR kituo cha Muheza, Dkt.William Kisinza amesema kuwa, licha ya Tanzania kupiga hatua kubwa za utafiti wa magonjwa bado kumekuwepo na maeneo ambayo yamekuwa na changamoto ya uwepo wa magonjwa yanayoenezwa na wadudu kama Malaria.

“Ni imani yetu kwa kupitia tafiti ambazo tunaendelea kuzifanya tutaendelea kuhimiza matumizi ya viuatilifu kwa usahihi ambavyo vimefanyiwa utafiti hapa nchini na kuweza kutoa matokeo bora ili kumaliza changamoto ya magonjwa hayo,”amesema Dkt.Kisinza.

Mafunzo hayo yameratibiwa na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani kupitia USAID (RTI) ambao ni wadau wa maendeleo waliosaidia serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, lakini kupitia taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu ambayo ndio taasisi pekee kwa Tanzania inayofanya tafiti za afya na kuzisajili.