Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MAMLAKA ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Tabora (TUWASA) imetoa kiasi cha sh mil 30 ili kujengwa zahanati ya Kijiji cha Igambiro, kata ya Misha katika halmashauri ya manispaa ya Tabora ili kumaliza kilio chao cha kukosa huduma za afya kwa miaka mingi.
Taasisi hiyo imetoa mchango huo kwa awamu mbili, awali walitoa kiasi cha sh mil 16 ili kuwezesha mradi huo kuanza na sasa wametoa kiasi kingine cha sh mil 14 ili kuunga mkono juhudi za serikali na nguvu ya wananchi kumalizia mradi huo.
Akikabidhi mchango huo jana Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo Mhandisi Mayunga Kashilimu alisema wametoa fedha hizo ili kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Aliongeza kuwa mchango huo pia ni sehemu ya utaratibu wa Mamlaka hiyo kurejesha kile inachopata kusaidia huduma za kijamii huku akibainisha kuwa kijiji hicho ni muhimu kuwa na huduma hiyo kwa kuwa kiko jirani na chanzo kikuu cha maji cha Bwawa la Igombe.
Mhandisi Kashilimu alisisitiza kuwa dhamira yao ni kuona mradi huo unakamilika haraka ili wananchi waanze kupata huduma za matibabu karibu na makazi yao tofauti na hali ilivyo sasa ambapo hulazimika kutembea umbali wa zaidi ya km 6 kufuata huduma hizo katika zahanati ya Kijiji cha Itaga.Naye Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya manispaa hiyo Elias Kayandabila alimshukuru Mkurugenzi kwa kutoa mchango huo ili kufanikisha ujenzi wa zahanati hiyo.
Alisema ujenzi wa zahanati hiyo ni muhimu sana kwa kuwa wakazi wa kijiji hicho zaidi 1500 watanufaika na kubainisha kuwa wametenga kiasi cha sh mil 100 katika bajeti yao ya mwaka huu ili kukamilisha miradi ya kijamii ikiwemo zahanati hiyo.
Diwani wa kata hiyo Yasin Kushoka aliwashukuru TUWASA na Mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa hiyo kwa dhamira yao njema ya kufanikisha ujenzi wa zahanati katika kijiji hicho.
Aidha alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka zaidi ya sh mil 400 katika kata hiyo ili kufanikisha utekelezaji miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu na afya ili kuboreshwa huduma za jamii.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho Khalfan Shaban alisema ukosefu wa Kituo cha kutolea huduma za afya katika kijiji hicho umeshagharimu maisha ya baadhi ya wananchi ikiwemo akinamama wajawazito kujifungulia njiani.
Alibainisha kuwa katika kata hiyo yenye vijiji 4 ni vijiji 2 tu vyenye zahanati ambavyo ni Itaga na Misha huku Makao Makuu ya kata hiyo yakiwa na Kituo cha Afya, hivyo akaomba mradi huo kuharakishwa ili ujenzi wa Masagala nao uanze.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi