November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Ummy Mwalimu

Tusiendelee kuchelewa kuanzisha Baraza la Rufaa za Mazingira

Na Mwandihi Wetu,TimesMajira,Online Dar

MTU mmoja amewahi kusema kiwango cha werevu wa taifa hupimwa kwa namna taifa husika linavyo yashughulikia masuala ya mazingira.

Ibara ya 62 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 (Sura ya pili, toleo la mwaka 2005), ikisomwa pamoja na Ibara ya 64, inaeleza juu ya uwepo na Bunge la Jamhuri ya Muungano na Mamlaka yake ya kutunga sheria.

Kwa kutekeleza wajibu na mamalaka yake, Bunge la Jamhuri ya Muungano lilitunga sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 (Sheria ya Namba 20 ya mwaka 2004.) Pamoja na mambo mengine, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, chini ya kifungu cha 204, inaanzisha Baraza la Rufaa za Mazingira.

Mwanasheria kutoka Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) Clay Mwaifwani anasema kuwa Baraza la Rufaa za Mazingira ni chombo halali chenye mamlaka ya kupokea rufaaa iwapo mtu yeyote amegadhibika na maamuzi ya Waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa mazingira, maamuzi juu ya kuwekwa au kutowekwa sharti fulani lenye kuhusiana na usimamizi wa mazingira, ukomo au kizuizi kwa mujibu sheria ya mazingira/kanuni zake na pia kutoa ufafanuzi wa suala lolote lile lihusulo Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.

Pengine baadhi ya wasomaji wetu leo hii inaweza kuwa mara ya kwanza kwao kusikia chochote kuhusiana na Baraza la Rufaa za Mazingira.

Baraza la Rufaa za Mazingira ni chombo chenye mamlaka ya kimahakama ya kusikiliza shauri lenye kuhusiana na masuala ya mazingira na kulitolea uamuzi.

Karne ya 20 imeshuhudia uanzishwaji wa mabaraza ya namna hiyo sehemu mbalimbali duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamzi wa Mazingira(NEMC) Dkt.Samuel Gwamaka (kushoto) akitambulisha wafanyakazi na menejiment ya uongozi wa Baraza hilo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais(Muungano na Mazingira), Ummy Mwalimu alipotembelea kwa mara ya kwanza ofisi za Baraa hilo jijinni Dar es Salaam juzi.

Sehemu ya 17 ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira inaeinda mbele zaidi kwa kuainisha mamlaka ya Baraza la Rufaa za Mazingira ikiwa ni pamoja na kuendesha mashauri kwa mfumo wake, nguvu yake ya kufanya maamuzi, vyanzo vya mapato, kinga za watendaji wa Baraza, masijala na rufaa kwenda Mahakama Kuu.

Licha ya uwingi wa vifungu vyenye kuelezea juu Baraza la Rufaa za Mazingira, bado Tanzania haina Baraza la Rufaa za Mazingira. Yapo mambo ambayo sheria haiyasemi au inayasema kwa uchache mfano, mabadiliko ya tabia ya nchi, lakini hili la Baraza la Rufaa za Mazingira sheria imelijadili kwa upana wake.

***Ni kwanini Baraza hilo halijaanzishwa?

Licha ya uwepo wa mahakama za kawaida zinazopokea mashauri kila siku, yakiwemo mashauri ya kimazingira, bado kuna ulazima na umuhimu mkubwa wa kuwa na baraza mahususi lenye mamlaka ya kusikiliza mashauri ya mazingira na kuyatolea maamuzi pasipo kuingiliwa na chombo kingine chochote.

Mahakama za kawaida huwa na mrundikano mkubwa wa kesi mbalimbali. Uwingi wa kesi kwenye mahakama hizo ni kikwazo kikubwa kwa utatuzi wa mashauri ya kimazingira kwa wakati.

Wakati mwingine miradi mikubwa ya uwekezaji husimama kusubiri maamuzi ya mahakama juu ya shauri la kimazingira mfano, shauri juu ya tathmini ya athari za kimazingira.

Mbali na suala la muda, changamoto nyingine kubwa kwenye mahakama za kawaida ni uwingi wa vikwazo vya kisheria. Sheria zenye kueleza taratibu kama vile sheria ya mwenendo wa mashauri ya madai zina vipengele vingi vinavyoweza kuleta mkanganyiko iwapo mlalamikaji hakuvifuata ipasavyo.

Vikwazo vya namna hiyo havigusi kiini cha shauri lakini vinaweza kumaliza shauri kabisa bila kiini cha mgogoro kusikilizwa.

Wakati mwingine majaji/mahakimu wa mahakama za kawaida hukosa weledi mpana juu ya masuala ya mazingira. Kwa kukosa utaalamu mahususi wa masuala ya mazingira, mahakama za kawaida huyatizama masuala ya mazingira kwa namna nyepesi na wakati mwingine masuala muhimu ya kiikolojia hayapewi uzito stahili kabisa hivyo kukwamisha jitihada za uhifadhi.

Mwanasheria kutoka Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) Clay Mwaifwani.

Kwa kutambua umuhimu wa maendeleo dumivu, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, imeanzisha Baraza la Rufaa za Mazingira.

Pamoja na mambo mengine, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, chini ya kifungu cha 204, inaiinisha kuwa wafanya maamuzi wa Baraza watatakiwa kuwa na elimu, uzoefu na weledi mpana kwenye masuala ya sheria na mazingira.

Wafanya maamuzi wa aina hiyo ni suluhisho muhimu sana kwa kesho na kesho kutwa ya mazingira yetu.

Naye Mwansheria, Baraka Thomas kutoka LEAT anasema kutokuanzishwa kwa Baraza hilo ni kikwazo cha kiutawala, kwani Bunge lilikwisha kufanya kazi yake kwa kuandaa vitendea kazi yaani sheria inayoanzisha Baraza.

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 pia, chini ya kifungu cha 230, inampa Mamlaka Waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa mazingira kutunga Kanuni zitakazowezesha utekelezaji bora wa vifungu vya Sheria.

Ni jambo la kufaa na kupendeza sana iwapo nafasi hiyo ingetumika kutunga Kanuni za usimamizi na uendeshwaji wa mambo yote yahusianayo na Baraza la Rufaa za Mazingira ili mashauri yote yahusuyo Mazingira yaanze kusikilizwa mbele ya chombo maalumu chenye watendaji wenye weledi na uzoefu mahususi wa sheria na mazingira.

“LEAT inatoa wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, kuchukua hatua za dhati za kuanzisha Baraza la Rufaa za Mazingira,” anasema Thomas na kuongeza;

“Ni imani yetu kuwa miaka 16 ya uwepo wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 bila ya uwepo wa Baraza la Rufaa za Mazingira ni ukwamishaji wa jitihada za usimamizi bora wa mazingira.

Ni matumaini yetu kuwa huu ndio wakati tuliokuwa tunasubiri na muda wenyewe ni sasa.”

Mwisho