January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tusibeze, tumpongeze Rais Samia kufufua ndoto za wanaopata mimba

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline

MWAKA 2021 Serikali ilitangaza kuwaruhusu wanafunzi waliokatiza masomo yao kwa kwa sababu ya kupata mimba kurejea masomoni ili kuendelea na masomo.

Uamuzi huo ulitangazwa na aliyekuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako.

Novemba 29, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan, alitoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa suala hilo kwa wanafunzi waliopata mimba wakiwa shule za msingi na sekondari.

Alisema wanafunzi waliopata ujauzito wakiwa shule za msingi wana uchaguzi wa kurudi shule katika mfumo rasmi au kwenda katika elimu mbadala ikiwemo mafunzo ya ufundi stadi.

“Kwa kawaida mtoto wa kike akishakuwa mama, kama amekuwa mama darasa la sita hatarudi tena darasa la sita kuendelea na shule, hiyo ndiyo kawaida,” alisema Rais wakati wa uzinduzi wa Shule ya Msingi Museveni iliyopo Chato mkoani Geita.

“Si kawaida, tuna mifano mizuri nchi nyingine zimefanya hivyo, Zanzibar wamefanya hivyo. Na kawaida wote ambao wamepata (ujauzito) wakiwa msingi hawarudi shule wanakwenda kwenye mkondo mbadala,” alisisitiza Rais.

Mwanafunzi aliyekuwa akiishi kwenye nyumba ya kupanga kutokana na uhaba wa mabweni katika shule aliyokuwa akisoma akiandaa chakula baada ya kutoka shule. Wanafunzi wengi ambao wanaishi mazingira kama haya walikatisha ndoto yao kutokana na kupata ujauzito. Hata hivyo, Rais samia amerejesha tabasamu lao baada ya kuwaruhusu kuendelea na masomo.

Uamuzi huo wa Rais Samia ulimaliza shinikizo la wanaharakati na wadau wa elimu ambao walikuwa wakishinikiza wanafunzi wanaopata mimba wakiwa shule za msingi au sekondari waruhusiwe kurudi katika mfumo rasmi kwa sababu ni haki yao kuelimika.

Katika uamuzi mpya wa Serikali, Rais Samia amesema suala la kurudi shule haliwahusu wanafunzi walipata mimba pekee bali wanafunzi wote waliacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo utoro, ujauzito na nidhamu ili kutoa fursa kwa watoto wa Tanzania kupata elimu.

Amesema Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha utekelezaji wa uamuzi wa kuwarudisha wanafunzi shuleni huo hauathiri sekta ya elimu nchini.

Baada ya uamuzi huo wa Rais Samia wapo waliopongeza na wapo waliobeza kuhusiana na mabadiliko hayo.

Awali kabla ya mabadilikio hayo, Sheria ya elimu ilizuia watoto wote wa kike kuendelea na masomo yao baada ya kubainika wana mimba, hivyo walifukuzwa shule na kusababisha wakose haki yao msingi ya kupata elimu kama inavyobainishwa ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 11 vifungu vidogo vya (1) na (2).

Ibara hiyo inaeleza; “….(1) Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa haki ya mtu kufanya kazi, haki ya kupata elimu na haki ya kupata msaada kutoka kwa jamii wakati wa uzee maradhi au hali ya ulemavu,”

“Na katika hali nyinginezo za mtu kuwa hajiwezi. Na bila kuathiri haki hizo Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba kila mtu anaishi kwa jasho lake.”

(2) Kila mtu anayo haki ya kujielimisha, na kila raia atakuwa huru kutafuta elimu katika fani anayopenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake.”

Ni wazi kwamba uwepo wa Sheria ya elimu ya mwaka 2002 iliyokuwa ikiwazuia watoto wa kike kuendelea na masomo yao baada ya kupata mimba ilikuwa ni inapingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndiyo sheria mama.

Kila Mtanzania ambaye ni mdau wa haki za watoto ana wajibu wa kumshukuru Rais wa Serikali hii ya awamu ya sita kwa uamuzi wake wa busara wa kuifuta Sheria hiyo, tunayoweza kusema ilikuwa ni miongoni mwa Sheria kandamizi dhidi ya haki za watoto hapa nchini.

Wanafunzi wakipelekwa shule na bodabofa

Uwepo wa sheria hiyo ulikuwa ukiwaathiri watoto wengi wa kike hapa nchini ambapo kila mwaka watoto wa kike wengi walijikuta wakifukuzwa shule baada ya kukumbwa na masaibu ya kupata mimba na wengine waliokuwa wakikatishwa masomo yao na wazazi wao ili waolewe.

Baadhi ya takwimu ambazo huko nyuma zilitolewa na Mashirika au Taasisi mbalimbali zilionesha ukubwa wa tatizo la mimba kwa watoto wa kike hapa nchini ambapo kwa mujibu Takwimu za Elimu (BEST) takriban wasichana wapatao 4,000 waliacha shule kwa sababu za ujauzito kwa mwaka 2020 pekee.

Lakini pia taarifa zilizopatikana kutoka mkoani Iringa zikionesha zaidi wa watoto wa kike wapatao 3,000 wenye umri kati ya miaka 10 na 19 katika kipindi cha Januari hadi Oktoba 2020 waliacha shule baada ya kupata mimba, inaonesha wazi ukubwa wa tatizo, hivyo kutowarudisha shuleni ni kuongeza wigo wa Watanzania wasiokuwa na elimu.

Kwa takwimu hizo za BEST na za mkoani Iringa, tunapaswa kujiuliza ni watoto wangapi wa kike waliofukuzwa shule ndani ya kipindi cha nyuma baada ya kupata mimba ambao wameikosa haki yao ya kikatiba ya kupata elimu kwa kadri ya uwezo wao wa kiakili?

Tukumbuke kwamba wengi wa watoto wanaokumbwa na masaibu ya kupata mimba katika umri mdogo ni kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu masuala ya afya ya uzazi, lakini pia mazingira ya kimaisha ambapo wengi wao ukichunguza hutoka katika familia zenye maisha duni.

Takwimu za hapa nchini zinazohusu mimba za mapema zinaonesha watoto na vijana wa umri wa kubaleghe wanahitaji habari muhimu za kuwasaidia kujikinga dhidi ya mimba za mapema, ambapo mnamo mwaka 2017 Shirika la Human Rights Watch lilibaini wasichana wengi wanakosa habari za kimsingi kuhusu afya ya uzazi.

Kwa hali hii hatua ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia, kuruhusu watoto wote wa kike watakaopata mimba, utoro au kuozeshwa wakiwa na umri mdogo kurejea shuleni inastahili kupongezwa badala ya kubezwa kama baadhi wanavyofanya.

Kitendo cha wale wanaobeza maamuzi haya ya Serikali kinastahili kupingwa na kupigiwa kelele na kila mdau mtetezi wa Haki za watoto hapa nchini kwa vile inaonesha wazi jinsi gani wasivyoelewa mazingira yanayosababisha watoto hao kupata mimba katika umri mdogo.

Jambo la kushangaza hata baadhi ya wazazi wenye watoto wa kike mara baada ya Serikali kutangaza maamuzi haya wameonekana kupinga waziwazi kwamba Serikali haikupaswa kufuta Sheria kandamizi iliyokuwa ikiwazuia watoto wa kike wanaopata mimba kuendelea na masomo yao baada ya kujifungua.

Ni wazi kwamba wazazi wa aina hii na wengine wote wanaopinga maamuzi hayo ya Serikali wanakwepa jukumu lao la malezi kwa watoto wao na badala yake kujaribu kuliacha mikononi mwa walimu mashuleni, ambako watoto wengi walielewa wanapopata mimba watafukuzwa shule.

Nieleze jambo moja, kitendo cha kudai mara baada ya Serikali kuruhusu watoto hao kuendelea na masomo baada ya kujifungua “eti” itakuwa chanzo cha ongezeko la mimba kwa wanafunzi kwa vile hawatakuwa na hofu ya kufukuzwa shule hakistahili kuungwa mkono.

Haya ni mawazo finyu ambapo kwa mtu mwenye busara inaonesha wazi kwamba, baadhi ya wazazi walijiondoa rasmi katika ulinzi wa watoto wao wa kike na kuacha kuwafundisha maadili mema ili wasikumbwe na masahibu ya kupata mimba katika umri mdogo na badala yake jukumu hilo wakaliacha shuleni.

Wanapaswa wakumbuke kuwa Tanzania ni moja ya nchi duniani zilizoridhia na kusaini Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto (CRC) wa mwaka 1989 ambao katika Ibara yake ya tano inazungumzia wajibu wa malezi kwa watoto.

Ibara hiyo inaeleza, “….Serikali inapaswa kuheshimu wajibu na jukumu la wazazi na walezi kulea watoto kwa misingi na maadili mazuri ambayo yatawasaidia kukua, kujifunza na kukuza vipaji vyao. Ni lazima wazazi na Serikali wajenge mazingira mazuri ya kuwaongoza watoto kwenye mafanikio.”

Hivyo basi inapotokea mzazi ama mlezi anailaumu Serikali kwa hatua yake ya kuwaruhusu watoto wa kike wanaopata mimba kurejea shuleni, inaonesha kwamba wazazi ama walezi hao hawataki kutimiza wajibu wao malezi kwa watoto wao na badala yake jukumu hilo wanaliacha shuleni.

Inawezekana vipi tudai kuruhusiwa kwa watoto hao kuendelea na masomo baada ya kujifungua kutasababisha ongezeko la mimba kwa watoto, wakati wazazi na walezi wapo?

Tuelewe kuwa mtu wa kwanza kulaumiwa kwa mtoto wa kike kupata mimba ni mzazi ama mlezi maana wameshindwa kutimiza wajibu wa malezi kwa watoto wao.

Haingii akilini kuamini kwamba Sheria ya mtoto kufukuzwa shule pale anapopata mimba ndiyo ilikuwa kinga ya wao kutokupata mimba kwa hofu tu ya kufukuzwa shule, binafsi siamini kama shule ndiyo mlinzi wa watoto bali naamini wazazi ama walezi ndiyo wanaopaswa kuhakikisha watoto hao hawapati mimba kabla ya wakati.

Mzazi ama mlezi mwema daima huhakikisha anawapatia watoto wake malezi yenye maadili mema pamoja na kuwaelimisha madhara ya kufanya vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha wapate mimba katika umri mdogo na waogope kuadhibiwa na wazazi wanapopata mimba badala ya kuogopa kufukuzwa shule.

Kwa hali hiyo hatuna sababu za msingi kuitupia lawama Serikali kwa hatua yake ya kuruhusu watoto wetu kuendelea na masomo yao baada ya kujifungua na badala yake wazazi na walezi wote wahakikishe wanawapatia malezi mema watoto wao ili waepuke kufanya vitendo vyovyote vichafu katika umri walionao.

Mwanafunzi mwenye ujauzito

Lakini tunapaswa kuelewa na kufahamu kwamba si kila mtoto wa kike anayepata mimba katika umri mdogo alionao huwa amedhamiria kufanya hivyo bali yapo masahibu na sababu nyingi zinazoweza kuwakumba ikiwemo kubakwa pale wanapokwenda ama kutoka shuleni.

Baadhi ya shule zetu hasa zile za sekondari za kata katika maeneo mengi nchini zipo mbali na maeneo ya makazi kiasi cha watoto kulazimika kutembea umbali mrefu kwenda shuleni na hivyo njiani hukutana na mambo mengi ikiwemo kusumbuliwa na wavulana na hata wakati mwingine kubakwa.

Mazingira ya kimaisha ni miongoni mwa chanzo cha baadhi ya watoto wengi kujikuta wakishawishiwa na tamaa ya kupata vitu muhimu kwa ajili ya matumizi ya shuleni, ambavyo hushindwa kupatiwa na wazazi ama walezi wao kutokana na hali ya kipato ndani ya familia.

Hivyo wakati Serikali ikiruhusu watoto hao kuendelea na masomo ni jukumu la kila mzazi ama mlezi ikiwemo wadau wa Haki za watoto kuongeza nguvu katika suala zima la malezi na kuwafundisha maadili mema ili kuhakikisha hawapati mimba kabla ya wakati unaotakiwa.

Hatuna sababu ya kuamini kwamba kuruhusiwa kuendelea na masomo yao baada ya kujifungua itasababisha ongezeko la mimba kwa vile shule siyo mlezi wa kwanza kwa mtoto ye yote bali jukumu hilo ni wazazi wenyewe.

Nihitimishe makala hii kwa kuwaomba na kutoa wito kwa wale wote wanaopinga maamuzi haya ya Serikali wabadili mitizamo yao Hasi, wakae chini wajitafakari na kujiuliza ni kweli kwamba kila mtoto wa kike anayepata mimba akiwa shuleni hufanya kitendo hicho makusudi na kwa kudhamiria?

Je! Kuwafukuza shule ni adhabu wanayoistahili au ni uonevu wa hali ya juu unaowanyima haki yao ya kupata elimu kama Katiba ya nchi inavyoelekeza? na Je! Shule ni “muarobaini” wa kuzuia watoto wa kike wasipate mimba? Na kama jibu ndiyo, Je, nini wajibu wa mzazi ama mlezi katika suala zima la malezi ya mtoto?