December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tumuenzi Maalim Seif Kwa vitendo

Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online

KATIBU Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amewahimiza Wanachama wa Chama cha ACT Wazalendo kumuenzi aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad kwa kutekeleza kwa vitendo misingi ambayo aliwaachia.

Akizungumza hayo leo katika ziara ya kuwatembelea na kuwajulia hali wazee na wagonjwa katika kata ya Tuangoma,Ado alisema Maalim Seif alifariki dunia Februari 17,2021 na alikuwa mtu ambaye anajali watu.

“Leo tumefanya ziara ya kuwatembelea na kuwajulia hali Wazee na Wagonjwa kwenye Kata ya Tuangoma,huu ni urithi aliotuachia kipenzi chetu Maalim Seif Sharif Hamad. Maalim alitufunza kuwa Chama ni familia. Ni lazima tuishi kwa upendo na kujaliana wenyewe na jamii yetu kwa ujumla  “,Amesema Ado

 Shaibu ameongeza kuwa Maalim Seif alikuwa kiongozi mwenye kuona mbali, mpenda haki na aliyetanguliza mbele maslahi ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

“Leo Vyama vyote vinazungumza umuhimu wa maridhiano na meza ya mazungumzo. Sisi ACT Wazalendo, mapema baada ya Uchaguzi Mkuu 2020, Maalim alituongoza kwenye meza ya mazungumzo na maridhiano ili kuhakikisha yale yaliyojitokeza kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020 hayajirudii tena. Tunafurahi kuwa licha ya changamoto, kebehi na dhihaka tuliyopitia wakati huo, Sasa kila mmoja anaona umuhimu wa kuliponya Taifa ili kufungua ukurasa mpya wa kisiasa Nchini”- Amesisitiza Ado.