December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tume ya Tehama yaleta kongamano kubwa la usalama wa mitandao

*Yatangaza ufadhili kwa wanawake 100 nchini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Na Mwandishi Wetu
SIKU chache baada ya Tanzania kung’ara katika usalama wa mitandao na kutangazwa nchi ya pili barani Afrika, Tume ya Tehama (ICTC) imeandaa kongamano kubwa la usalama wa mitandao litakalofanyika mapema mwezi ujao jijini Arusha.

Aidha, katika juhudi za kuunga mkono uwezeshaji wanawake katika eneo hilo, Tume hiyo imetangaza kufadhili wanawake 100 waweze kushiriki katika kongamano hilo la siku mbili.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama nchini, Dkt. Nkundwe Mwasaga wakati alipokutana na kuzungumza na wanahabari kuhusiana na ujio wa na Kongamano kubwa la Usalama Mtandaoni kati ya Aprili 4 na 5.

Alisema kongamano hilo ni sehemu ya mikakati ya Tume ya Tehama na Serikali kwa ujumla kuimarisha usalama mtandaoni ili uchumi wa Tanzania uweze kupaa na kuwa endelevu.

“Lengo la mkutano huo ni kuimarisha usalama wa mtandao wa Tanzania kupitia ushirikiano, ubadilishanaji wa maarifa, na uvumbuzi…Nchi yetu kwa sasa ipo katika mikakati ya haraka sana ya kufanya mapinduzi ya kidigitali ili tuweze kupata faida ya mambo mengi ambayo yapo duniani na yanaletwa na teknolojia hii ya Tehama,” alisema Dk. Mwasaga.

“Duniani ili uwekezaji uweze kukua, usalama mtandaoni ni suala muhimu sana kujadiliwa,” alisisitiza na kubainisha kuwa, kongamano hili litashirikisha zaidi ya wataalamu 300, kati yao 100 kutoka katika mataifa mbalimbali yenye kujikita katika Tehama ikiwamo Estonia.

Alisema pamoja na kuwa Tanzania ni ya pili kwa usalama mtandaoni Barani Afrika ikitanguliwa na Mauritius ni lazima kuendelea kuhakikisha kwamba usalama unaendelea kutokana na kuibuka kwa teknolojia mpya zinazofungamanishwa na teknolojia ya tehama.

Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) kupitia Global Cybersecurity Index limeiweka Tanzania katika nafasi ya pili Afrika baada ya kukidhi vigezo zaidi ya 150. Tanzania pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la ITU.

Dkt. Mwasaga aliongeza kuwa, kongamano hilo ambalo litakutanisha wataalamu, watunga sera, na wabunifu kujadili changamoto muhimu na kukuza suluhu kwa ajili ya mazingira salama zaidi ya mtandao, linafanyika wakati Tehama nchini Tanzania inachangia zaidi ya dola bilioni moja za Marekani kwa kila mwaka.

Aliongeza kuwa, Tume ya Tehama yenye majukumu kadhaa, yakiwemo uratibu wa utekelezaji wa sera na kukuza tehama nchini, imesema kwamba itadhamini wanawake 100 kutoka miongoni mwa wanafunzi wa tehama na wale ambao wana kampuni ndogo zinazoshughulika na usalama mtandaoni ili kuhakikisha kwamba hawaachi mtu nyuma katika masuala hayo.

Jukwaa hilo ambalo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye linafanyika wakati taifa lipo katika mapinduzi ya kidigitali ambapo masuala muhimu matano yanastahili kuzingatiwa kuhakikisha kwamba tunaelekea eneo sahihi ya maendeleo ya kidijiti.

Dk Mwasaga alitaja masuala hayo kuwa ni upatikanaji wa ujuzi Tehama kwa ajili ya matumizi ya Watanzania, kuhakikisha usalama wa mtandao, kuona kunakuwapo na huduma jumuishi, kuwa ndani ya uchumi wa kidijiti na kuendeleza ubunifu.

Alisema kongamano linagusa suala la usalama ambapo wanatakiwa kujadiliana na wataalamu wa Tanzania na nje masuala yote ya mtandao.

Alisema suala la usalama linapokuwa sio zuri masuala yanayofanywa katika mapinduzi ya kigitali hayatakwenda vyema.

Dhima ya kongamano hilo ambalo mwaka huu ni la tatu ni kutengeneza dunia ya mtandao iliyo jumuishi na vile vile iliyoshirikishi.

Alitaja mambo matano yakataoyojadiliwa kwa makini kuwa ni namna ya kuongeza umadhubuti katika sekta za uchumi, kuangalia jinsi gani mambo usalama mtandao yanafanya sekta ya uchumi kuendelea kufanya vizuri zaidi.

“Hili tunaliangalia vizuri kwa sababu vitu vikienda vibaya mambo hayatakwenda vyema,” alisema na kuongeza kuwa mada ya pili ni kulinda dunia ya mtandao katika kipindi cha teknolojia ibukizi ikiwamo akili bandia na `big data’ ambapo wataangalia namna gani umadhubuti unaweza kuwepo katika mitandao wakati wa kutumia teknolojia ibukizi.

Mada ya tatu katika kongamano ni kuwezesha dunia ya kimtandao ambayo itakuwa salama na endelevu na jumuishi kwa kujenga uelewa wa wananchi wa kawaida kuelewa wautumie vipi mtandao kwa manufaa yao na ya taifa.

Mada ya nne ni kufanya dunia mtandao kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi.

“Hapa tutaangalia masuala ya uchumi yanayochagizwa na mambo ya usalama mtandaoni. Masuala ya kimtandao kuona ukuzi unaendelea vyema na pia tutaiangalia mada ya tano ya kuondoa vishawishi ambavyo vinafanya wafanye makosa mtandaoni.”

Mkurugenzi mkuu huyo alisema nafasi zipo wazi kwa washiriki kujiandikia kushiriki kongamano hilo ambalo litakuwa endelevu kutokana na mahitaji ya sasa ya mapinduzi ya viwanda.

Aidha alishauri wataalamu kuingia katika tovuti ya tume hiyo (www.ictc.go.tz) na kujisajili Tanzania Cybersecurity Forum ili kujifunza zaidi.

Tume ya TEHAMA ni taasisi yenye jukumu la msingi la kukuza maendeleo ya TEHAMA hapa nchini.

Pamoja na majukumu mengine, Tume ya TEHAMA ina jukumu la kujuza ujuzi wa masuala ya TEHAMA hapa nchini.

Kwa upande wa masuala ya usalama wa mitandao, Tume ya TEHAMA ina wajibu wa kutathmini utekelezaji wa mikakati mbalimbali na kutoa ushauri pamoja na mwelekeo wa matumizi salama ya mitandao ya kompyuta na huduma za kielektroniki kwa ujumla .