January 14, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tulia Trust yaandaa mashindano ya ngoma za asili msimu wa nane kufanyika Mbeya

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

TAASISI ya Tulia Trust imeandaa Tamasha la ngoma za asili msimu wa Nane(8) kutoka makabila mbalimbali ya Tanzania Bara na visiwani lengo likiwa kuenzi tamaduni na kuonyesha uzuri wa ngoma za jadi .

Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika kwa siku tatu mfululizo mwezi Septemba mwaka huu Jijini Mbeya.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 22,2024 Ofisa habari na mawasiliano wa Taasisi ya Tulia Trust,Joshua Mwakanolo amesema kuwa tamasha hilo litafanyika kuanzia Septemba 26 ,2024 mpaka 28 katika uwanja wa Ndege wa zamani uliopo kata ya Iyela Jijini hapa.

“Huu utakuwa msimu wa Nane (8) kufanyika kwa mashindano haya ya ngoma ambayo ni muhimu yenye lengo la kuenzi tamaduni zetu ikiwa ni pamoja na kuonyesha uzuri wa ngoma zetu za jadi Kutoka katika makabila mbalimbali ya Tanzania Bara na visiwani katika jukwaa moja”amesema Ofisa habari huyo .

Aidha Mwakanolo amesema kuwa tamasha hilo litakuwa fursa kubwa kiuchumi kwa vikundi vya ngoma na kusema kuwa katika tamasha hilo kutakuwa na zawadi mbalimbali kwa washiriki watakaofanya vizuri zitatolewa.

Hata hivyo Ofisa habari huyo amesema kuwa uwepo wa mashindano hayo ya ngoma ni fursa kwa wajasiliamali wadogo na wafanyabiashara ambapo wataruhusiwa kufanya biashara zao kwenye eneo la tukio kulingana na utaratibu utaratibu utakaopangwa kwa wajasiliamali wadogo na wafanyabiashara bila gharama yeyote.

Amesema kuwa kwa mwaka huu tamasha hilo
ni msimu wa Nane (8) toka kuanza kwa tamasha hilo la ngoma na kwamba dhumuni kubwa la tamasha hilo ni kuenzi tamaduni za jadi za makabila tofauti tofauti.

Akielezea zaidi Mwakanolo ameeleza kuwa vikundi vinavyotoka nje Mbeya mjini vitajigramia usafiri isipokuwa chakula na malazi ambavyo Taasisi ya Tulia Trust itandaa .

Taasisi ya Tulia Trust imekuwa ikijishughulisha na uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa wajasiliamali wadogo pamoja na mpango wa msaada kwa jamanii na kuandaa matamasha mbalimbali ikiwemo Tulia Trust traditional dancers festival, Mbeya Tulia Marathon,Tulia Trust cup, Tulia street talent competition,tuzo za umahili wa habari.

Mmoja wa wakazi wa Sinde Jijini Mbeya,Atu Sanga amesema kuwa uwepo wa matamasha mbalimbali yanayoandaliwa na Taasisi ya Tulia Trust umekuwa ukiwainua wajasiliamali wadogo kwa kufanya biashara mbalimbali katika eneo hilo .

“Tunamshukuru Mh.Mbunge wetu Dkt Tulia Ackson maana tunajua hii Taasisi ipo chini yake ,ametusaidia akina mama tulio tunaojishughulisha na biashara ndogo ndogo hapa uwanjani wakati matamasha yakiwa yanaendelea,hizi siku tatu za tamasha hili la ngoma litatuinua kiuchumi”amesema.