November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tuhuma za eneo la TAMPERI kuhusu Mkurugenzi wa Mwanza zadaiwa kuwa siyo za kweli

Raphael Okello,Timesmajiraonline,Mwanza.

HIVI karibuni kumetokea taarifa katika mtandao wa kijamii zinazodai kuwa eneo la TAMPERI limeuzwa na mkurugenzi wa jijini la Mwanza Aroun Kagurumujuli na kwamba mkurugenzi huyo si mwaminifu jambo ambalo ni la upotoshwaji na linapaswa kupuuzwa.

Taarifa hizo zinadai kuwa Kagurumujuli amepangisha Pamba FC kinyume cha utaratibu jambo ambalo halina ukweli ndani yake.

Kwa mahojiano kadhaa kutoka vyanzo mbalimbali ndani ya halmashauri ya jiji la Mwanza yamebaini eneo la Bustani ya Tamperi iliyopo katika ufukwe wa Ziwa Victoria barabra Kuu ya Mwanza Mjini kwenda Airport haijawahi kuuuzwa kama ilivyodaiwa katika taarifa hizo.

Taarifa zinaeleza kuwa eneo hilo lilivamiwa na baadhi ya watu kwa lengo la kujimilikisha kinyume cha sheria lakini halmashauri la jiji liliingilia kati na shauri lake lilifikishwa mahakama kuu mwaka 2015 na kupewa no. 35/2015.

Katika shauri hilo upande wa serikali(jiji) lilishinda kesi na kutangazwa kama mmliki halali wa eneo la Tamperi ingawa walalamikiwa hawakuridhishwa na maamuzi hayo ya mahakama kuu.

Habari kutoka katika vyanzo vya kuaminika vinaeleza kuwa wakati wote wa sakata hilo ,Mkurugenzi wa sasa wa jiji la Mwanza Aroun Kagurumujuli alikuwa bado hajateuliwa kuwa mkurugenzi wa jiji la Mwanza.

Vyanzo vinaeleza kuwa Ndugu Kagurumujuli aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa jiji la Mwanza na Rais Dkt. Samia Suluhu Hssan mwaka 2023 akiwa anaaminiwa na Rais kuwa ni mtendaji mwaminifu katika nafasi hiyo.

Habari zinasema muda mfupi baada ya Kagurumjuli kuingia ofisini moja ya kazi aliyofanya miongoni mwa kazi zingine ni kuhakikisha kuwa eneo hilo linapimwa kwa ajili ya kuweka vitega uchumi vya halmashauri ya jiji .

Baada ya kupimwa viwanja saba vimepatikana katika eneo hilo la ufukweni mwa ziwa Victoria ambalo ni kivutio cha uwekezaji na kwamba halmashauri iko mbioni kutangaza eneo hilo ili wapatikane wawekezaji ambao wanaweza kuingia mkataba na jiji la Mwanza.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi wanasema kuwa wanampongeza Rais wa Awamu ya Sita Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyolitendea vyema jiji la Mwanza kwa kumleta Mkurugenzi wa Jiji , Aroun Kagulumjuli kwa madai kuwa anao uzoefu na maono ya maendeleo.

Wananchi hao wanaeleza kuwa Kagurumjuli anao msimamo na anafuata sheria na anayetumia muda wake vizuri bila kuchoka kutatua changamoto za wananchi hivyo wanaomtuhumu ni wale wenye maslahi binafsi.

Mkazi wa Mabatini Jijini Mwanza, Mabula Syenda alisema kuwa Mkurugenzi huyo ni msikivu na kwamba baada ya kukutana naye aliweza kutatua mgogoro wa kiwanja uliokuwa unamkabili.

KUHUSU MATUMIZI YA SHILINGI BILIONI MOJA.

Chanzo kimojawapo kimeeleza kuwa fedha za mauzo ya viwanja vya Rwegasore ziliingizwa katika akaunti ya halmashauri mwaka 2022/23 baada ya malipo kufanyika.

Kinasema nyaraka zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii ni zile zinazoeleza namna fedha za viwanja hivyo zilivyotumika baada ya kupitishwa katika vikao vya halmashauri ya jiji la Mwanza.

Kinaeleza vikao halali vya halmashauri za jiji la mwanza ndivyo vilivyoidhinisha matumizi ya fedha ambazo hata hivyo inadaiwa kuwa ilimng’oa madarakani aliyekuwa mkurugenzi wa jiji la Mwanza kabla ya Kagurumjuli.

SUALA LA UPANGAJI WA PAMBA FC

Ili lilitokea mwaka 2022 ambapo Kampuni ya DIMETOCLASA REAL HOPE LTD ya Jijini Dar Es salaam iliingia mkataba wa kupangisha nyumba zilizopo eneo la Lwanima wilaya ya Nyamagana kwa ajili ya watumishi wake.

Mkataba huo ulikuwa wa miaka mitatu ambao unafikia kikomo mwaka 2024 kwa mantiki hiyo Pamba Football Club iliingia mkataba wa upangaji na Kampuni ya Ditetoclasa Real Hope LTD na sio Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza kama ilivyodaiwa katika taarifa zilizambazwa mtandaoni.

Ikumbukwe kuwa mkataba baina ya pande hizo umeingiwa wakati Mkurugenzi hakuwa amehamia jiji la Mwanza.