November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TTCL yazidi kusambaza mkongo wa mawasiliano kwa nchi jirani 

Na Penina Malundo, Timesmajira 

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania TTCL   limesema mpaka sasa linaendelea na mchakato wa kufikisha huduma za mkongo wa taifa kwa  nchi ya  Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) ikiwa ni muendelezo wa kupeleka huduma hiyo kwa nchi za jirani. 

Ambapo  mpaka sasa huduma hiyo imefikishwa katika nchi nne ikiwemo Burundi,Rwanda,Zambia na Malawi.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika maonesho ya 48 kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba,Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Tanzu ya TTCL,(T-PESA),Lulu Mkudde wakati akiongea na waandishi wa habari,alisema 

“Tunaposema tunafungua milango ya kidigitali inamaanisha kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi katika kutumia huduma za Interneti katika kutekeleza huduma mbalimbali kwa watu wengine,”amesema na kuongeza 

“Mpaka sasa shirika limefanya mambo mbalimbali ikiwemo huduma  ya TTCL – Pesa ambapo katika Sabasaba hii tumekuja na huduma ya Akaunti Pepe inamuwezesha mteja kufungua akaunti yake bila hitaji ,mteja anauwezo wa kutumia akaunti yako masaa 24 kwa siku,”amesema.

Amesema mpaka sasa,Shirika  limesambaza Mkongo wa Taifa katika mikoa yote nchini ambapo  zaidi ya wilaya 98 zikiwa nazo zimefikishiwa Mkongo wa mawasiliano.

Mkudde amesema juhudi hizo zote zinalenga kuhakikisha juhudi za huduma za Elimu, Afya na Maendeleo ya kiuchumi ambayo  yanatekelezeka kidigitali katika maeneo yote nchini.

“Niwahakikishie TTCL ,itahakikisha huduma za mawasiliano inakuwa nzuri ili kuwapa fursa wananchi kupata huduma mbalimbali za kujipatia shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato kupitia fursa hii ya Interneti kwa gharama nafuu,”amesema

Akizungumzia Huduma ya T-cafe,Mkudde amesema huduma ya T -Café  ni huduma ya WiFi  ambayo ina waondolea  adha wafanyabiashara, waandishi wa habari na wataalamu wa masuala ya ushauri katika kufanya kazi zao wakiwa nje ya ofisi.

Amesema ni huduma ambayo inasaidia mtu yoyote  kufanya kazi nje ya ofisi kwa kupata  uwezo wa kutumia huduma zao  katika kutekeleza huduma zake .

“Shirika limeanzisha huduma hii ili kuwawezesha wateja wote kufanya shughuli zao kwa haraka na gharama nafuu,ambapo  kwa  kipindi hiki cha Sabasaba  tumeshuhudia huduma hii  inavyofanya kazi kwa speedi ya hali ya juu na wananchi kwa wakati wote walikuwa wakitumia   katika maonesho hayo,”amesema.

Aidha amesema kupitia  maonesho haya,TTCL imepata  fursa ya kutoa elimu na kujenga uelewa kwa wananchi  kuhusu huduma hiyo wanayoitoa  ambayo inamfikia  mwananchi moja kwa moja .

“Tumepokea maombi mengi kwa wateja wanahitaji huduma hii,kwani yameleta mapinduzi ya kuisha haraka kwa vifurushi vya kawaida, shirika limeleta huduma hii kumuwezesha mwananchi kutumia Internet bila kikomo,”amesema.