Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Mbozi.
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Songwe, Theopista Mallya, amewataka askari wa usalama barabarani kufanya kazi kwa kusimamia sheria, kanuni na taratibu, ikiwemo kujiepusha na vitendo vya rushwa vinavyoweza kuharibu taswira ya jeshi hilo.
Ametoa maelekezo hayo Novemba 30, 2023, alipokutana na kuzungumza na askari hao wa usalama barabarani katika kikao kikao kazi kilicholenga kuwakumbusha utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya sheria,taratibu, kanuni kulingana na miongozo ya kazi zao.
Pamoja na hayo, kamanda Mallya alikemea vikali vitendo vya ulevi uliopindukia kwa askari kwani ni utovu wa nidhamu na kunaweza kuharibu taswira ya jeshi la Polisi.
“Tunapaswa kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia haki, weledi na uadilifu ili kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani ambavyo vimekuwa vikisababisha ajali”.
“Lakini tunatakiwa kitenda haki kwa kuchukua hatua kwa yeyote atakayebainika kufanya vitendo visivyokubalika kisheria hasa kwa watumiaji wa vyombo vya Moto,” alisisitiza Kamanda Mallya.
Aidha, Kamanda Mallya alitumia kikao kazi hicho kutoa wito kwa wananchi na watumiaji wa vyombo vya moto, wakiwemo watembea kwa miguu kufuata kanuni, sheria na alama za barabarani, huku akiwataka kuwaripoti madereva wanaovunja sheria ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu