September 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TRA yatekeleza agizo la Rais Samia ukusanyaji kodi halali kwa W’biashara

Na Jackline Martin,Timesmajiraonline,Dar

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha inakusanya kodi halali kwa wafanyabiashara.

Aidha, TRA imekutana na wafanyabiashara mbalimbali na kujadiliana suala la utozaji wa kodi za ndani kwa bidhaa ambazo zimewekewa bei elekezi katika Idara ya Ushuru wa Forodha, lakini pia wale wanaoagiza mizigo kwa pamoja kisha kuja kugawana.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kikao hicho, Naibu Kamishna wa Walipa Kodi Wadogo, Edmund Kawamala, alisema lengo ni kutengeneza uelewa wa pamoja ili wanapotoka na kuanza kutekeleza kusiwe na misuguano isiyo na lazima.

“Tukikaa pamoja wao wakituelezea changamoto ya mfumo tukazioana basi tunakuja na njia ya kuzitatua lengo ni kila upande utimize wajibu wake ili tuweze kukusanya mapato ya nchi kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisema.

Kuhusu mapato, Kawamala alisema mwezi uliopita mapato yamezidi kuboreka na
kuvuka lengo kwa kukusanya asilimia 104 ya lengo.

“Suala siyo tu mapato bali suala ni mtu ajiskie analipa kodi halali isiyo ya dhuruma kama alivyotuelekeza Rais Sami kwamba tusikusanye kodi za dhuruma, bali tukusanye kodi ambayo mlipa kodi anaona anastahili kulipa na analipa kwa mujibu wa sheria,” alisema Kawamala.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Martin Mbwana, alisema kikao hicho kitapelekea kuwepo kwa ongezeko la watu kupenda kulipa kodi na watu wengi kuweza kuingia kwenye mfumo wa ulipaji kodi.

“Namshukuru Kamishna Mkuu kwa kikao hiki, lakini pia Rais Samia kwa maelezo yake aliyoyatoa ili kuiangalia jamii ya biashara na mfumo Mzima wa kodi,” alisema.

Naye Mwenyekiti Taifa wa Jumuhiya ya wafanyabiashara, Hamisi Livembe aliwashauri wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi halali ili kuepukana na
misukumano ya pande zote.